Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Simbachawene wakiangalia sehemu wanaponapochinjia mifugo Vingunguti jijini Dar es Salaam jana. Na Mpigapicha Wetu
Dar es Salaam. Kasi ya Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano jana ilichukua sura ya aina yake wakati mawaziri watatu walipoibuka kwenye machinjio ya Vingunguti, na kutoa maamuzi magumu kutokana na kukithiri kwa uchafu, ubadhilifu wa makusanyo ya fedha za ushuru.
Wakiwa katika eneo la machinjio hayo mawaziri hao, Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Dk Hamisi Kigwangalla (Afya), na George Simbachawene (Ofisi ya Rais-Tamisemi), walishuhudia hali ya uchafu wa eneo hilo na baadaye kubaini ubadhilifu mkubwa.
Baada ya kufanya ziara hiyo iliyoanza saa 4:47 asubuhi na kumalizika saa 5:32, mawaziri hao hawakuridhishwa na hali ya usafi kwenye maeneo ya kuwekea nyama. Mbali na hayo walisikiliza kero za wadau ambao ni wachinjaji na wauzaji wa mifugo, waliodai wanatozwa ushuru mkubwa kama malipo ya Sh11,000 kwa ng’ombe mmoja, fedha ambazo hulipwa mnada wa Pungu (sh6,000) na Vingunguti (Sh5,000).
Catherine Severine, ambaye ni mchuuzi aliyekuwa zamu usiku wa Desemba 24 mwaka jana, aliwaambia mawaziri hao kuwa kumekuwepo udanganyifu wa utoaji wa vibali kwenye mnada wa Pugu. Alidai kuwa siku hiyo walifikishwa mbuzi 1,407 huku wenye vibali wakiwa 300 , ng’ombe 700 lakini wenye vibali halali 492, hivyo kwa hesabu za haraka, zaidi ya Sh3.4 milioni zilipotea.
Alisema kwa ujumla wanatakiwa wakusanye kiasi cha Sh75 milioni kwa mwezi, lakini walikuwa wanakusanya Sh18 milioni huku Sh55 milioni zikiingia mifukoni mwa wajanja.
Simbachawene alimpa siku tatu mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwaondoa wale wote waliokaa muda mrefu katika eneo hilo na kujimilikisha kila kitu.
“Kigwangalla naomba usitufungie, Jumanne nitataka kupata maelezo ya waliohusika na haya mabanda. Si kweli kwamba yamegharimu Sh100 milioni. Hadi Jumatatu umeme uwe umerudishwa kwenye hayo mabanda, yatumike ili kupunguza mbanano,” aliagiza Simbachawene.
Mwigulu aliwataka wote waliokuwepo mnadani Desemba 24, kufika kwa katibu mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Jumatatu na kuanzia leo waanze kutafuta kazi ya kufanya kwa sababu ya kujumlisha ng’ombe na mbuzi imewashinda.
Mwigulu alisema hayo baada ya juzi usiku kukuta machinjio ya Vingunguti kuna vibali 300 vya mbuzi, lakini kukiwa na mbuzi zaidi 1,000 na ng’ombe zaidi ya 200 hawakuwa na vibali, kitu alichosema kinaashiria wanafanya makusudi siyo kwamba hawajui kujumlisha.
“Kuanzia sasa vibali vyote vya wanyama wanaotakiwa kuchinjwa hapa, vitolewe kwenye mnada wa Pugu, huku wakusanya ushuru wa Serikali Kuu na Halmashauri watakusanya hapa katika machinjio ya Vingunguti. Mnaolipia ushuru hakikisheni mnaondoka na risiti, lango la kuingizia ng’ombe lijengwe mara moja hata matatu, manne tena kwa fedha inayopatikana hapa hapa machinjioni,” alisema Mwigulu huku akishangiliwa.
Kigwangalla alisema anakubali ombi la Simbachawene la kutaka wasifungiwe kwa muda na watavamia wakati wowote kukagua maagizo waliyotoa kama yanafanyiwa kazi.
Alisema mambo aliyoyaona akiwa katika Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa miaka miwili iliyopita ndiyo aliyoyakuta jana , hivyo hatawavumilia wanaohusika.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment