NA EDITOR
21st January 2016.
Ni jambo la kusikitisha kuwa pamoja na Tanzania kusifiwa duniani kote kwa kuwa nchi ya amani na utulivu, lakini bado suala la Zanzibar limekuwa kitendawili.
Tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, siku tatu baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo, kumekuwa na jitihada kubwa za kusaka suluhu ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mzozo wa Zanzibar ulizuka kutokana na kitendo cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi huko.ZEC ilidai kuwa ilichukua hatua hiyo baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa kanuni za uchaguzi kwenye baadhi ya vituo na hasa katika kisiwa cha Pemba. Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya Maalim Seif kutangaza kuwa alikuwa ameshinda uchaguzi huo.
Hatua hiyo ilizua sintofahamu katika visiwa vya Zanzibar na ndipo hatua ya mazungumzo ilipoanza.
Mazungumzo hayo yalimhusisha Maalim Seif, mgombea wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein, na viongozi wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hata hivyo, dalili za kusuasua kwa mazungumzo hayo zilianza kuonekana kutokana na kauli za wanasiasa wa pande zote mbili zilizosikika katika siku za karibuni.
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale wa CCM, wamekuwa wakisisitiza juu ya kurudiwa kwa uchaguzi huo, jambo ambalo lilikuwa linapingwa vikali na viongozi wa CUF, ambao wanaamini uchaguzi uliopita uliendeshwa kihalali.
Kitendo cha Maalim Seif kujitoa kwenye mazungumzo haya ni pigo kubwa kwani kitaendelea kusababisha tofauti za kisiasa visiwani Zanzibar. Pia inashangaza kuona kuwa muafaka unashindwa kupatikana wakati Tanzania inasifika kwa kudumisha amani na utulivu.
Tanzania imejizolea sifa kwenye medani ya kimataifa kutokana na kusuluhisha migogoro mingi ya kisiasa katika nchi mbalimbali.
Pia inasikitisha kuona kuwa kila inapotokea suala la uchaguzi huko Zanzibar basi joto la kisiasa hupanda kiasi cha kutishia amani.
Mvutano huhusisha vyama viwili vya CCM na CUF, ambavyo viongozi wake wamekuwa wakivutana kiasi cha kusababisha sintofahamu miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Ni jambo la kushangaza kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia historia ya kisiasa kujaribu kupandikiza chuki na mgawanyiko miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Ni ukosefu wa uungwana kuona baadhi ya wanasiasa wanakumbushia siasa za vyama vya zamani vya ASP, ZNP na ZPPP, ambavyo vilikuwa na mvutano mkubwa katika miaka ya 1950 na 1960 na kuleta mambo hayo katika kipindi hiki.
Hivi kweli ni busara kweli kwa kizazi hiki kuleta siasa za miaka ya 1950 katika uchaguzi unaofanyika mwaka 2015? Suala hili la kuendekeza siasa za zamani limekuwa kikwazo kwa ustawi wa demokrasia na uchumi wa Zanzibar.
Watanzania wamechoshwa na suala hili kwani chanzo chake ni ubinafsi wa baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar wanaondekeza itikadi za vyama vyao badala ya kuzingatia maslahi mapana ya taifa.
Dhana ya kuendelea kuendekeza siasa za vyama katika Zanzibar inadidimiza kimaendeleo visiwa hivyo. Mathalani, tangu mwaka jana, hakuna Baraza la Wawakilishi huko Zanzibar kutokana na mvutano huu wa uchaguzi, hivyo kuna hatari ya mvutano huu kuongezeka zaidi ikiwa CUF itajitoa kwenye uchaguzi wa marudio.
Tunapenda kuwaeleza wanasiasa wa Zanzibar kuwa wanapaswa kukaa mezani na kuzungumza ili kupata muafaka wa tatizo hili kwa manufaa ya watu wa Zanzibar na si kuendekeza siasa za vyama na maeneo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment