Profesa Sospeter Muhongo-Waziri wa Nishati na Madini
Historia na elimu
Profesa Sospeter Muhongo ni Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Tano (SAT). Profesa Muhongo, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, ameteuliwa kwenye baraza la kwanza la mawaziri la Rais John Magufuli.
Muhongo ana umri wa miaka 61, akiwa amezaliwa Juni 25, 1954 katika Wilaya ya Musoma Mjini, mkoani Mara. Alisoma elimu ya msingi na sekondari mkoani humo.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu shahada ya jiolojia. Kwa sababu ya ufaulu wa hali ya juu, alipata ufadhili kwenda kusoma shahada ya uzamili Chuo Kikuu cha Gӧttingen nchini Ujerumani na baada ya kuhitimu aliendelea tena na shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin, ambako alijikita kwenye jiolojia.
Muhongo anaongea lugha nne, Kiswahili, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa na amemuoa Bertha Mamuya, ambaye wamezaa naye mtoto aitwaye Rukonge. Muhongo na Berta wanalea yatima watatu.
Uzoefu
Katika maisha yake ya kitaaluma amewahi kupokea na kutunukiwa tuzo nyingi, achilia mbali ushiriki wake katika mambo mengi ya kitafiti. Serikali ya Ufaransa ilimtunukia cheo cha ofisa mwenye tunu iliyotukuka ya kitaaluma - Ordre des Palmes Académiques, iliyoanzishwa na Mfalme Napoleon mwaka 1808.
Mwaka 2004 alipokea tuzo inayoheshimiwa na Jamuiya ya Wanajiolojia wa Afrika ya Prof Robert Shackleton wa Uingereza (Geological Society of Africa’s prestigious Prof Robert Shackleton Award), kwa ajili ya utafiti wa kipekee kuhusu jiolojia ya miamba yenye umri wa zaidi ya miaka 500 barani Afrika (Precambrian Geology of Africa).
Amekuwa mshiriki wa ngazi ya juu (fellow) wa Akademia ya Sayansi ya Nchi Zinazoendelea (FTWAS), Chama cha Wanajiolojia wa Afrika (FGSAf), Akademia ya Sayansi ya Afrika (FAAS) na Akademia ya Sayansi ya Tanzania (FTAAS).
Profesa Muhongo amewahi kuwa makamu wa rais wa Tume ya Ramani ya Jiolojia ya Dunia (CGMW), mhariri mkuu wa Jarida la Afrika la Sayansi za Miamba na Madini (The Journal of African Earth Sciences, Elsevier) na hadi sasa ni mjumbe wa bodi kadhaa za uhariri wa majarida na vijarida vya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amewahi kuwa rais wa Chama cha Wanajiolojia wa Afrika (1995-2001), mkurugenzi mwanzilishi wa Ofisi ya Sayansi ya Kanda ya Afrika (ICSU) yenye makao mkuu jijini Pretoria, Afrika Kusini (2005-2010), mwenyekiti wa bodi ya Unesco-IUGS-IGCP Programu ya Kimataifa ya Sayansi ya Jiolojia (2004 - 2008) na mwenyekiti wa Kamati ya Programu ya Kisayansi (SPC) ya Mwaka wa Kimataifa wa Sayari ya Dunia uliotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN-IYPE) mwaka 2007-2010.
Mwaka 2009, Profesa Muhongo aliteuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgombea wa nafasi ya mkurugenzi mkuu wa Unesco na alikuwa miongoni mwa wasomi wanne mashuhuri walioingia kwenye mchujo wa mwisho, japokuwa hakupewa wadhifa huo.
Mwaka 2014 alishinda tuzo ya Heshima ya Jumuiya ya Wanasayansi wa Jiolojia na Uchimbaji Petroli na Gesi Asilia ya Nigeria (NMGS)/AMNI ya Profesa M.O. Oyawaye.
Profesa Muhongo ametumia takribani maisha yake yote katika masuala ya taaluma na utafiti. Hakuwahi kuwa kiongozi wa kuwakilisha wananchi hadi alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge na baadaye Waziri wa Madini Mei 2012 - katika mabadiliko ya tano ya Baraza la Mawaziri. Muhongo aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri Januari 24, 2015 kutokana na shinikizo kubwa la Bunge akituhumiwa kutochukua hatua katika kashfa ya uchotwaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegtetas Escrow.
Baadaye mwaka 2015 Muhongo alikuwa kati ya wana CCM zaidi ya 40 waliochukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho. Kwa bahati mbaya ndoto yake ya kusaka tiketi hiyo ilikwama baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali na Kamati Kuu ya CCM.
Baada ya kukosa tiketi ya kugombea urais, Muhongo alijitosa kwenye kura za maoni ndani ya CCM akisaka kuliongoza jimbo la Musoma Vijijini. Muhongo aliongoza kura za maoni ndani ya chama chake kwa kupata 30,431 kati ya 37,144 zilizopigwa. Mshindani wake, Antony Mtaka ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Hai, alipata kura 3,457.
Kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika wa Oktoba 25, Profesa Muhongo alishinda kwa jumla ya kura 41,731 dhidi ya 24,984 za mpinzani wake wa karibu, Zakaria Mbura kutoka Chadema. Baada ya ushindi huo, Rais JPM alimteua kuongoza tena Wizara ya Nishati na Madini, uteuzi ambao umekosolewa sana na vyama vya upinzani na hata ndani ya CCM wakiuhusisha na dhana ya rais kudharau maazimio ya Bunge lililopita.
Nguvu
Nampima kuanzia kwenye weledi wake, kujiamini kwake na kazi aliyoifanya katika kipindi kifupi alichokaa wizarani kabla ya kujiuzulu mwaka 2015. Pamoja na yote yaliyotokea, bado utendaji wake hauwezi kudharauliwa na ni wa kuigwa japokuwa tuna wajibu wa kuyajadili mapungufu yake.
Kwanza, Muhongo ni mchapakazi na mtu mwenye kiu ya mabadiliko. Baada ya ugunduzi wa gesi asilia na mafuta katika sekta za nishati na madini nchini, aliweza kusimamia mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watu waliopata mafunzo mazuri ya kitaaluma katika eneo la mafuta na gesi asilia na leo Tanzania inajiandaa kusimamia sekta hii kwa kushirikiana na watu wenye mitaji kutoka nje, tayari tukiwa na mtaji wa wataalamu wetu.
Pili, ni msimamizi mzuri wa mambo katika rekodi zake. Amesimamia ongezeko la usambazaji umeme vijijini na mijini na amesimamia punguzo la gharama za kuunganishiwa umeme vijijini na mijini. Japokuwa miradi mingi kati ya hii ilianzishwa chini ya mtangulizi wake, William Ngeleja, Watanzania ni mashahidi kuwa utekelezaji wa hali ya juu ulisimamiwa na Profesa Muhongo.
Tatu, huyu ni mwanasiasa na mwanataaluma asiyekata tama. Alipoanguka uwaziri 2015 angeweza kuachana na siasa moja kwa moja, lakini alijifunza na kusimama tena, akapambana jimboni na leo amerudi pale alipo. Kutokata tamaa huku ndiko kunahitajika wakati atakapokuwa akitoa miongozo yenye changamoto kwenye wizara hii.
Nne, Muhongo anayejifunza kutokana na makosa yake. Alipoteuliwa na Kikwete kwa mara ya kwanza mwaka 2012 kuwa mbunge, na akapandiswa na kuwa waziri papo kwa hapo, Muhongo alikuwa ni mtu wa majivuno, kiburi, dharau na anayeongea lugha za kuudhi kila mara. Alipojiuzulu kwa shinikizo la kutosimamia vizuri sakata la Escrow, alirejea kwao na kuamua kugombea ubunge na tayari anaonekana ameanza kujifunza namna gani ya kuwasiliana na watu na kwa muda gani.
Kwa kipindi kifupi ambacho nimemuona akiwa waziri baada ya kuteuliwa na Magufuli, lugha yake ya mawasiliano imeshabadilika, anawasiliana na watu na siyo “viatu”, na anajenga hoja na si kuonyesha kuwa anajua kuliko wengine. Haya peke yake yanaweza kufanya aanze kutazamwa kama mtu anayejifunza kutokana na makosa yake.
Udhaifu
Udhaifu mkubwa wa Muhongo ambao bado sijathibitisha kama ameondokana nao au la! ni tabia ya kudandia ajenda zisizomuhusu na kutumia weledi wake kama kinga ya uozo ambao naye inawezekana haujui vizuri. Mathalani, Muhongo aliwashangaza watu wengi aliposimama hadharani ndani ya Bunge na hata nje na kudai kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow si za umma.
Wakati anatetea hoja hiyo tayari alikuwa na taarifa za kina za namna hata Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alivyokagua akaunti hiyo na namna Benki Kuu ilivyohusika katika jambo hilo. Kuna mambo huhitaji mantiki ndogo sana kuyatatua, hakuna hata siku moja katika sheria zetu CAG akaenda kukagua fedha binafsi, hakuna hata mara moja ikatokea Baraza la Mawaziri na vyombo vya Serikali vikakaa na kujadili fedha za mtu au taasisi binafsi, na haiwezekani hata siku moja ofisi za Serikali zikapitishiana vimemo huku na kule kutoa maelekezo kuhusu fedha za mtu au taasisi binafsi.
Msimamo wa Muhongo unamaanisha kwamba huenda kuna nyakati anatumia taaluma na mamlaka yake vibaya na hilo si jambo jema ikiwa anataka kufanya mabadiliko tunayoyahitaji. Kwenye sakata la Escrow, sisi tusio na mipaka na ambao tunaamini kuwa Muhongo hahusiki na wizi wa fedha zile na kwamba hakunufaika nazo na wala hakuwa na nia mbaya juu ya fedha hizo, tunaamini kuwa Muhongo alitumika vibaya aidha kwa kujua au kutojua kueleza kuwa fedha zile za Escrow Sh306 bilioni hazikuwa za umma na mimi binafsi naamini kuna siku atasimama hadharani na kukiri kuwa alichokisema hakikuwa cha kweli.
Matarajio
Muhongo anajua kwamba amekuwa msaada mkubwa katika sekta ya nishati na madini tangu alipokabidhiwa kwa mara ya kwanza hadi kujiuzulu. Anatambua kwamba anao wajibu wa moja kwa moja kutorudia makosa ya nyuma na kufanya kazi kubwa ili kujenga uaminifu kwa wananchi juu yake kwani “alishaumwa na nyoka”.
Vipaji na elimu yake ni msingi mkuu wa kuyafikia matarajio anayoyaota siku zote, lakini zaidi ya yote, aina ya Serikali iliyo madarakani hivi sasa inaweza kuwa msaada mkubwa kwake kufikia matarajio hayo.
Wakosoaji wa Muhongo wanatarajia kwamba ataachana na kugeuzwa kuwa “kondoo wa kafara” katika masuala muhimu yatakayojitokeza mbele ya safari. Siri kubwa ya kufikia matarajio hayo ni kufanya kazi kwa uwazi. Wananchi wanatarajia kuona mikataba ya madini inafumuliwa, sekta ya madini na ile ya nishati zinaendeshwa kwa uwazi mkubwa na ushirikishwaji wa wananchi unakuwa wa juu kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma.
Changamoto
Muhongo na wenzake wanatambua kwamba Nishati na Madini ni wizara muhimu mno kwa serikali ya Tanzania. Hapa ni mahali kuna miradi mingi na mikubwa na fedha nyingi. Nishati ni eneo ambalo linachangamana na vyanzo mbalimbali vya kupata nishati hata kama vyanzo hivyo si nishati. Vitu kama mafuta, gesi na upepo ni vyanzo muhimu vya nishati mbalimbali na vyote viko kwenye wizara hii.
Tanzania ni nchi mojawapo duniani ambayo inazalisha madini mengi. Mathalani, Tanzania inashikilia nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha dhahabu ikiwa nyuma ya Afrika Kusini na Ghana na mara chache sana imewahi kuwa nyuma ya Mali. Tanzania ni ya sita barani Afrika kwa kuzalisha madini ya shaba. Tanzania imo kwenye nchi kumi za Afrika zinazozalisha almasi kwa wingi. Tanzania ndiyo nchi peke yake inayozalisha madini aina ya Tanzanite. Kwa bahati mbaya, sekta ya madini imeshindwa kulisaidia taifa kwa kutoa mchango mkubwa kwenye mapato kama inavyotakiwa na ni lazima sasa Muhongo na wenzake watuletee mipango ya dhahiri ambayo itaikwamua sekta ya madini.
Vilevile, kumekuwa na suala la mikataba ya madini na hata kwenye nishati pia. Kwa kiasi kikubwa mikataba hiyo ni ya siri na isiyo na mwelekeo wa kulisaidia taifa. Viongozi wachache tu ndiyo wameendelea kunufaika na mikataba ya madini huku Serikali ikikosa mapato. Kwa sababu “Serikali ya Magufuli” imeshajinasibu kama mwarobaini wa kuhakikisha maeneo ambayo kodi zilikuwa hazilipwi kwamba zinaanza kulipwa.
Kila mmoja anasubiri kuona mipango ya Muhongo kutatua suala hili muhimu. Kuweka uwazi kwenye mikataba ya madini na kuhakikisha mapato ya madini yanaongezeka na kufahamika.
Maeneo ambako madini yanachimbwa nchini yanatia huruma na hasira. Ukienda huko unaweza kujithibitishia kuwa madini hayo ni laana kwetu na siyo tunu. Huko ndiko mahali ambako kuna umasikini uliopitiliza, shuleni watoto wanakaa chini na wananchi wamechoka. Lazima Muhongo na wenzake waje na mikakati na sera na sheria za msingi zitakazokwamua maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo madini yanachimbwa, kundoa manyanyaso dhidi yao, mauaji na ulemavu unaosababishwa na vyombo vya dola kwa kisingizio cha kulinda migodi ya madini, mikakati ya wazi ya kulinda maisha ya wafanyakazi wa migodini.
Hizi ni changamoto zinazohitaji majibu ya lazima.
Kwa upande wa nishati, tuna changamoto nyingi. Moja kubwa ni nchi kuendelea kutegemea umeme unaotokana na maji peke yake, hivi sasa tumeanza pia kuongeza umeme wa gesi, lakini bado hautoshi. Kwa ujumla kuna vyanzo vingi vya umeme lakini havijatumiwa ipasavyo, mojawapo ni upepo, na wakati huo huo hata hivyo vyanzo vya umeme wa maji havijapanuliwa kiasi cha kuzalisha umeme kwa kiasi cha kutosha.
Muhongo na wenzake wanapaswa kuja na mkakati mahsusi ili kupanua vyanzo vya umeme, ikiwezekana ndani ya miaka michache ijayo ili Tanzania iwe na umeme wa kutumia ndani na kiasi kikubwa kinachobaki kuuza kwa nchi jirani.
Kipaumbele cha kuzalisha umeme mwingi na kuhakikisha unafika vijijini kwa uhakika ni changamoto ya kudumu hadi sasa. Nchi inapokuwa na umeme wa kutosha ina maana viwanda vitakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi na kufunguliwa zaidi, ile sera ya viwanda aliyokuwa anaihubiri Magufuli itatekelezeka.
Lakini pia lazima Muhongo awe na mikakati mbadala ya kumaliza tatizo la umeme kwa kuwezesha miundombinu ya kila namna ya kusimamia miradi mikubwa ya umeme wa jua ambao ni nafuu, ya asili na isiyo na gharama kubwa baada ya kusimika.
Hitimisho
Pamoja na faida nyingi za kumrudisha Muhongo katika wizara hii, ukweli ni kuwa anapaswa azidi kujifunza diplomasia, tena sana. Yale aliyojifunza kwenye kampeni za ubunge, kuwafuata wananchi majumbani kwao, kukaa nao chini, kuwauliza matatizo yao na kuwapa uongozi wa utu ndiyo yanapaswa kufanyika sasa. Hatutegemei tena kusikia kauli za kifedhuli kama ile ya “wafanyabiashara wa Tanzania wana pesa za madafu” iliyompa anguko. Muhongo anayajua na lazima ayarekebishe.
Lazima pia ajifunze kuheshimu na kusikiliza mawazo ya wengine. Wananchi wa kawaida, watendaji wa Serikali na wafanyabiashara wanaweza kuwa na mawazo mazuri kuliko ya Profesa. Muhongo. Kusoma sana hakuna maana ya kujua kila kitu na Mungu aliwaumba binadamu hivyo. Kitakachomsaidia kwa dhati ni kusikiliza mawazo ya watu, kuwashirikisha kutafuta majibu na kuyasimamia.
Na rai ya mwisho kwake ni namna gani atafanya kazi na Bunge la sasa. Kwa sababu mikasa iliyomuondolea uwaziri ilitokea bungeni, na kwa sababu naamini yeye Muhongo hakuiba fedha za escrow na hakuhusika katika mipango hiyo. Ni wakati mwafaka sasa kufanya kazi na wabunge kwa karibu, kazi yake iwe ya mafanikio makubwa ili awathibitishie umuhimu wake na kujenga imani mpya naye. Mimi binafsi napenda sana utendaji wa Muhongo na namtakia kila la heri.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).
KUHUSU MCHAMBUZI
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).
No comments :
Post a Comment