dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 17, 2016

NANI NI NANI SERIKALI YA JPM? Profesa Jumanne Maghembe – Waziri wa Maliasili na Utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Abdallah Maghembe      

By Julius Mtatiro
HISTORIA NA ELIMU
Profesa Jumanne Abdallah Maghembe ni Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la Rais John Magufuli. Ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Kilimanjaro tangu mwaka 2000. Profesa Maghembe ana miaka 64 hivi sasa na ifikapo Agosti, atafikisha miaka 65 kwani alizaliwa Agosti 24, 1951 huko Usangi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1959 katika Shule ya Msingi Kiwaleni, Usangi na baadaye akahamia katika Shule ya Msingi Lomwe hukohuko Usangi ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1965. Alipata masomo ya sekondari katika Shule ya Dodoma mwaka 1966 hadi 1969 kisha akajiunga katika Shule ya Sekondari Tosamaganga na kusoma kidato cha tano na sita mwaka 1970 na 1971. Baada ya kufaulu vizuri kidato cha sita, alichagulikuwa kusomea masuala ya misitu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alijiunga chuoni hapo mwaka 1972 na mwaka 1975 akahitimu Shahada ya Sayansi ya Misitu (BSc. Forestry).
Mwaka 1975, alikwenda Norway na kujiendeleza zaidi katika elimu na ubobezi wa masuala ya misitu na mwaka 1977, alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Misitu (MSc Forestry).
Kati ya mwaka 1977 na 1978 Maghembe aliendeleza ubobezi wake kwenye sekta ya misitu, alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Duke, New York – Marekani.
Alirejea UDSM mwaka 1979 na kuanza masomo ya juu zaidi na akatunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Sayansi ya Misitu (PhD in Foresty Science) mwaka 1982.
Kati ya mwaka 1983 hadi 1985 alikuwa katika Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Kilimo na Misitu (ICRAF), Nairobi, Kenya ambako aliendeleza mafunzo ya kiutafiti baada ya shahada ya uzamivu (Post Doctoral Research). Mwaka 1986 hadi 1987 alitunukiwa cheti maalumu cha masuala ya misitu baada ya kushiriki kozi muhimu iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Oregon cha Uingereza. Ameoa na ana watoto.
UZOEFU
Ajira yake ya kwanza ilikuwa UDSM kuanzia mwaka 1975, akiwa mfundishaji msaidizi na mhadhiri msaidizi, mwaka 1980 alipanda na kuwa mhadhiri na mwaka 1982 akapandishwa na kuwa mhadhiri mwandamizi na kudumu hapo hadi mwaka 1985.
Mwaka 1985 alipandishwa kuwa Profesa Mshiriki lakini mara hii akiwa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua).
Tangu 1988 hadi alipoingia kwenye siasa, alikuwa Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Idalo, Marekani na wakati huohuo kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 2000 alikuwa Mwanasayansi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti katika Kilimo na Misitu (International Centre for Research in Agroforesty) yenye makao makuu yake jijini Nairobi.
Katika muda wote wa kushiriki kwenye masuala ya taaluma kwa vitendo, msomi huyu amewahi kuchapisha maandiko zaidi ya 65 yanayotokana na tafiti mbalimbali za kisayansi alizofanya kwenye maeneo aliyobobea.
Aliamua kuachana na kazi za utafiti na taaluma jijini Nairobi mwaka 2000 na kurejea nyumbani kuanza siasa. Akaweka nia katika Jimbo la Mwanga na kuridhiwa na CCM. Kwenye uchaguzi wa jumla akawabana wapinzani wake wakiongozwa na TLP, NCCR na CUF akawa mbunge.
Mwaka 2005 alirejea ulingoni jimboni Mwanga kwa mara ya pili, akavuka kizingiti cha kura ya maoni na kuwa mgombea wa CCM. Kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huo akapambana na Juma Kilaghai kutoka CUF na kushinda kwa kura 25,218 sawa na asilimia 78.1 akifuatiwa kwa mbali na Juma Kilaghai wa CUF aliyepata kura 5,317 sawa na asilimia 16.5.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ulikuwa mgumu kwa CCM katika majimbo mengi nchini, lakini haikuwa kwa Jimbo la Mwanga. Profesa Maghembe alisimama tena kwa mara ya tatu na kupata ushindi wa asilimia 78.9 uliotokana na kura 20,638, alifuatiwa na Msuya Yatery wa Chadema aliyepata kura 4,476 sawa na asilimia 17.02.
Wakati wengi wakitegemea kwamba huenda miaka 15 katika siasa imemtosha, uamuzi wake ukajibu maswali ya wengi baada ya kutangaza kuwa hatastaafu ubunge mwaka 2015. Akashiriki kura za maoni ndani ya CCM na kuwashinda Joseph Thadayo na Karia Magaro kwa kupigiwa kura 10,743 dhidi ya Thadayo aliyepewa kura 6,889 na Magaro kura 252.
Kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 alipambana vilivyo na kada wa Chadema, Henry Kilewo. Matokeo ya mwisho yalimpa ushindi kwa kura 21,982 dhidi ya 17,366 za Kilewo.
Katika nyakati tofauti, Profesa Maghembe ameshikilia nyadhifa za uwaziri (hakuanzia kwenye unaibu waziri) kwenye uongozi wa JK. Alianza kwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Januari hadi Oktoba, 2006 akahamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii alilokaa kwa takribani miaka miwili (Oktoba 2006 hadi Februari 2008). Februari 2008 akahamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi alikokaa kwa miaka takribani miwili tena (Februari 2008 hadi mwishoni mwa 2010).
Katika kipindi cha pili cha JK, alikabidhiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko kuanzia Novemba 2010 hadi Mei 2012. Kisha akahamishiwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuanzia Mei 2012 hadi Novemba 2015.
Rais Magufuli alipoingia amemkabidhi Wizara ya Maliasili na Utalii. Ndani ya CCM Maghembe amekuwa na nyadhifa kadhaa za kawaida tangu mwaka 2000. Amewahi Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mkoa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM taifa.
NGUVU
Nguvu yake ya kwanza ni ubobezi. Kiongozi huyu ni mmoja wa wasomi “nguli” hapa Tanzania akiwa na shahada nne za chuo kikuu zikiwamo mbili za uzamili na zote zikimuweka karibu na masuala ya kilimo na misitu. Ubobezi huu ni tunu kwake kwa sekta aliyokabidhiwa hivi sasa ambayo inaendana kabisa na fani yake.
Pili, ni kiongozi mzoefu bungeni. Amekaa bungeni kwa miaka 15 mfululizo na amekuwa mmoja kati ya wabunge wenye mchango mkubwa katika masuala ya kitaaluma yanayohusu kilimo na misitu. Ameshiriki kwa kiasi kubwa pia kutoa ushauri mwingi uliochangia kutungwa kwa sheria mbalimbali za mazingira na misitu.
Ni kiongozi mzoefu ndani ya Serikali ya Tanzania. Amefanya kazi serikalini kwa miaka 35, miaka 20 akifanya kazi za kitaaluma kitaifa na kimataifa na 10 akiwa waziri kwenye wizara tano, huo siyo uzoefu mdogo. Bahati aliyonayo hivi sasa ni kwamba JPM amempa wizara ambayo aliwahi kuiongoza kwa miaka miwili huko nyuma.
UDHAIFU
Rekodi ya Maghembe katika baadhi ya wizara alizowahi kupitia siyo nzuri sana kulingana na uwezo wake kitaaluma. Mathalan, alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Oktoba 2006 hadi Februari 2008, ni wakati ambao vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa vilizidi kuripoti matukio makubwa ya ujangili uliochukua mamia ya wanyama muhimu. Hadi anaondoka kwenye wizara hiyo, hakuna mitandao mikubwa iliyochukuliwa hatua.
Wakati alipokuwa Waziri wa Elimu kati ya mwaka 2008 hadi 2010 ndiyo wakati ambao migogoro kati ya taasisi za elimu na Serikali ilipamba moto huku mkakati wake wa kutatua mizozo hiyo ukiwa nguvu badala ya diplomasia na kuzungumza na makundi husika na hata Mwaka 2013 wakati akiwa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, alitajwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mikoani kwamba ni mmoja kati ya mawaziri ambao wanaiangusha Serikali ya chama hicho kwa utendaji mbovu.
Jeuri, kiburi, dharau na kutosikiliza watu wengine ni jambo jingine linalomuangusha waziri huyu. Watendaji na baadhi ya wataalamu wa wizara alizopitia wameniambia kwamba ni mtu wa kuzungumza zaidi na kutoa maelekezo zaidi kuliko kusikiliza, hata anapokuwa mbele ya wataalamu wa fani asizozijua. Tatizo la namna hii kwa wabobezi husababishwa na ngazi ya elimu waliyofikia na kule kudhani kuwa wao wanajua kila kitu. Kama hajajifunza huko nyuma sijui kama atajifunza sasa lakini wananchi wanategemea abadilike na kutenda kazi kwa kuwashirikisha watu waliomzunguka, kuwaamini na kuamini taaluma zao.
MATARAJIO
Matarajio ya Profesa Maghembe katika wizara ya sasa ni kujifunza kutokana na makosa na kutumia wasaa huu vizuri ili kuziba mapengo ambayo hakuyafanyia kazi kwa miaka saba iliyopita. Anaweza kuazima mbinu alizitumia alipokuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na kuifanya wizara yake iongoze katika tathmini za mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaojumuisha wizara sita. Hii siyo wizara ngeni kwake na anayo kila sababu ya kuanza kazi mara moja.
Kilio cha wadau wa utalii na maliasili ni kilekile; ushirikishwaji wa mipango na hatua za wizara. Wanasema hata masuala ya ujangili yanaweza kutokomezwa ikiwa watahusishwa kubuni mbinu muhimu za kupambana na hali hiyo. Vinginevyo wanasema Profesa Maghembe akiamini zaidi vyombo vya dola na kuwapuuza, anaweza kumaliza miaka yake mitano bila rekodi ya kujivunia.
CHANGAMOTO
Tanzania ni kati ya nchi tajiri duniani katika eneo la vivutio vya utalii na masuala ya maliasili kwa hiyo inastahili kukusanya fedha nyingi kutokana na maliasili na utalii, huenda mara 20 ya fedha zinazokusanywa sasa, lakini kwa sababu ya mipango mibovu, ujanja mwingi, kukosa uaminifu na usimamizi mbovu, sekta hii imedorora. Leo nchi kama Kenya ambayo ina vivutio vichache vya utalii kuliko Tanzania, inapokea mabilioni ya dola kila mwaka kutokana na utalii, sisi bado tunapiga “mark time”.
Taifa letu linahitaji mkakati madhubuti wa kujitangaza kiutalii ili tufuatiliwe na nchi nyingi duniani. Mathalani, ikiwa televisheni yetu ya Taifa na nyingine za ndani zinaonekana kwenye “virusha matangazo” vya kimataifa, wizara inapaswa ibuni vipindi maalumu vya matukio muhimu yanayoendelea kwenye mbuga zetu za wanyama kila wiki na kuyarusha kila baada ya muda fulani. Matangazo ya namna hiyo na yale ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake, yafanywe kwenye vyombo vya habari vya kimataifa na chaneli mbalimbali zinazoonekana kwenye nchi zinazoongoza kuleta watalii ukanda wa Afrika Mashariki ili wengi wajue nini kinapatikana Tanzania.
Tumejionea majuzi baada ya Mbwana Samatta kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, kwa wachezaji wa ligi za ndani ya Afrika, baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti kuwa Samatta ni raia wa Tunisia, vingine vikamtaja kama raia wa Gabon. Hali hiyo pia inavikumba vivutio vya kitalii, mtalii anapofuatilia viunganishi vya utalii vya Kenya kwenye mitandao ya kijamii anakuta vinautaja Mlima Kilimanjaro hivyo kujua uko Kenya! Huo wote ni udhaifu Unaothibitisha kuwa sekta ya utalii inahitaji nguvu ya ziada, mipango ya kisasa na mbinu endelevu ya kuikwamua.
Lakini pia sekta hizi mbili (maliasili na utalii) ni kati ya zile ambazo zinanuka rushwa kubwa. Profesa Maghembe anapaswa kuwa mzalendo kuongoza sekta hizi kwani kuna makundi makubwa ya matajiri yameshageuza maliasili za Tanzania kuwa sehemu ya wao kukwaa utrilionea na ubilionea.
Mathalani, kwenye maliasili kuna matajiri na wamiliki wengi wa vitalu vya kuwindia wanyama hai kinyemela na kwa mikataba mibovu, kati yao wapo wanaojihusisha moja kwa moja na uwindaji haramu ambao unateketeza maelfu kwa makumi elfu ya wanyama muhimu na adimu kila mwaka. Watu hawa wanafanya hivi kwa sababu wanalindwa na maofisa wa juu wa wizara hii na watu wenye nyadhifa kubwa ndani ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama. Mbinu za wawindaji haramu ziko dhahiri na zinafanywa kwa kushirikiana na maofisa na watu nyeti serikalini, Serikali yoyote yenye intelijensia inayofanya kazi kwa uhakika lazima inatambua mitandao ya kijangili inasaidiwa na nani na yuko wapi. Mifumo yetu inapaswa kuimarishwa na Profesa Maghembe achukue hatua kali na za haki kwa wote ambao wanahusika na mitandao hii bila chembe ya huruma.
Askari wa wanyamapori mathalani, wanazo changamoto nyingi kwenye utendaji kazi wao, wanasema majangili wanatumia vifaa vya kisasa na mbinu za hali ya juu kufanya uwindaji, wao (askari wa wanyama pori) kwenye mapori mengi hata vikingia risasi wanavyo vichache mno, mara nyingine wanakuwa na oparesheni endelevu lakini menejimenti hazina mafuta ya kutosha ya magari. Askari hawa ni lazima watatuliwe masuala muhimu yanayowakabili kwa wakati. Mapori na misitu yetu muhimu visilindwe kwa kubahatisha, nchi zilizoendelea zimekuwa na ufanisi kwenye ulinzi wa mbuga na mapori yao kwa sababu ya teknolojia.
Unapotumia (mathalani) teknolojia ya “drones” ambazo zinajengewa kituo kwenye mbuga husika. Vifaa hivyo vinao uwezo wa kupaa angani vikiongozwa na kompyuta na vikapiga picha na kuchukua video za matukio mbalimbali yanayoendelea kwenye mbuga. Kazi ya askari inakuwa ni kufanya doria na kusubiri maelekezo kutoka chumba cha udhibiti kuwajulisha ni wapi “drones” hizi zimepatilia shaka.
Faida ya kuwa na vifaa vya namna hii kwenye mbuga zetu ni kutufanya tuajiri askari wachache, wenye vifaa vya kutosha na ambao wanafanya doria zao kwa saa chache wakielekezwa na chumba cha udhibiti wa vifaa vilivyoko angani. Gharama tunayopata hivi sasa na siku za usoni kuwapoteza twiga, tembo na wanyama wengine adimu ni kubwa kuliko kuamua kufunga mitambo ya kisasa kulinda maliasili zetu. Profesa Maghembe anayo changamoto kubwa kwenye eneo hili.
HITIMISHO
Profesa Maghembe siyo waziri wa kutumainiwa na kutegemewa sana katika Baraza la JPM. Siyo tu kwa sababu wadau wengi walishangazwa na uteuzi wake, la hasha! Ni kwa sababu amekuwamo serikalini kwa miaka 10 mfululizo akizunguka kwenye wizara na ni moja tu ndiyo tathmini za ndani ya Serikali zinaonyesha kwamba ilipiga hatua.
Nadhani JPM amempa wizara hii kwa sababu ya ukongwe na kutambua kuwa atampa msaada mkubwa ili waziri huyu afanye majukumu yake. Mtu wa haiba ya Profesa Maghembe kwa maana ya sifa zake, elimu, ubobezi, weledi na uzoefu akiamua kufanya kazi na kufanyia kazi hoja za wanaomkosoa, anaweza kupata mafanikio yatakayowafanya wachambuzi wengi waanze kufanya utafiti kujiuliza ikiwa mawaziri waliofanya kazi kwenye Serikali iliyopita walikuwa wanafeli kwa sababu ya kuwa na rais asiyefanya maamuzi magumu.
Hata hivyo, wakati haufichi kitu, miaka michache kutoka sasa sote tutaelewa kama Profesa Maghembe alikuwa ni “mzigo” au “pipi” iliyokuwa imefichwa ndani ya ganda. Namtakia kila la heri
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi *
KUHUSU MCHAMBUZI
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).  

No comments :

Post a Comment