Rais wa tano wa Zanzibar, Dk Salmin Amour
Handeni. Mmoja wa wanafamilia ya Rais wa tano wa Zanzibar, Dk Salmin Amour ametapeliwa kwa kuuziwa ekari 150 za ardhi wilayani hapa Mkoa wa Tanga.
Baada ya kuuziwa eneo hilo kwa ajili ya shughuli za kilimo ilibainika baadaye lilitengwa kama hifadhi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Magamba, Kata ya Kwaluguru, mwanafamilia huyo, Munil Amour alisema Februari mwaka jana alifika kijijini hapo kuomba eneo la ardhi kwa ajili ya kilimo.
Alisema alipatiwa ekari hizo na uongozi, lakini baadaye ilibainika ni hifadhi ya kijiji na mpaka sasa hajajua suluhisho la suala hilo.
Awali, mkazi wa kijiji hicho, Yusuph Sonyo alihoji jinsi wageni walivyopewa ardhi hadi maeneo ya hifadhi bila uongozi wa kijiji kuwashirikisha wananchi.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Erick Semsela alikiri mbele ya mkutano huo kupokea Sh2 milioni kwa ajili ya ekari 50 na kuwa, si eneo lote ni la hifadhi, bali ekari 15 ndizo zilizoko kwenye msitu wa hifadhi, hivyo wanafanya utaratibu wa kumfidia mtu huyo kwa kumpa sehemu nyingine.
Maelezo ya ofisa huyo yaliibua utata kuhusu ekari 100 zilizosalia na fedha zake, kwa kuwa stakabadhi hazionekani, huku mnunuzi akidai alilipa fedha zote na hadaiwi.
Kutokana na hali hiyo, wanakijiji walimtaka Ofisa Tarafa wa Magamba, Boniface Deusdedit kuwachukulia hatua viongozi wa kijiji.
No comments :
Post a Comment