Wakati viongozi wa kamati ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi mkuu wakikutana Ikulu Zanzibar jana, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), pia imekutana na kujadili waraka wa ajenda ya kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe mjini hapa, unaonyesha kuwa vikao hivyo vimefanyika kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti na kwamba wakati kamati ya muafaka ikikutana chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu, ZEC walikutana makao makuu ya tume hiyo, mtaa wa Maisara chini Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha.
Hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa kutoka katika vikao hivyo, licha ya kwamba habari za ndani kutoka kwenye vyanzo vyetu, zinadai kuwa ZEC walikuwa na ajenda nzito ya kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Viongozi wanaoshiriki mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi mkuu ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, na marais wastaafu wa Zanzibar.
Viongozi hao wastaafu ni pamoja na Ali Hassan Mwinyi, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Salmin Amour Juma ambaye hata hivyo, inadaiwa jana hakuhudhuria kikao hicho cha tisa cha kutafuta muafaka.Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alithibitisha jana kufanyika kwa mazungumzo hayo na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif.
“Kweli mazungumzo yamefanyika na Maalim Seif amehudhuria, lakini sisi kama chama hatufahamu kilichoafikiwa katika mazungumzo hayo,” alisema Shehe.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Salum Maulidi Kibanzi, alipoulizwa alisema yeye si msemaji wa mazungumzo hayo na kutaka watafutwe wahusika.
“Mimi si msemaji wa mazungumzo hayo, kwani kila mnapoandika taarifa mnapata wapi?”alihoji Kibanzi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Hassan Khatibu, alisema tangu kuanza mazungumzo hayo, wametakiwa kuwa na subira na kwamba taarifa watapewa baada ya kukamilika kwake.
“Mambo haya tumeambiwa tuwe na subira mpaka mazungumzo yakamilike watatoa taarifa. Kwa sasa sina cha kuzungumza,” alisema Khatibu.
Mazungumzo hayo ya kwanza kufanyika tangu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kukutana na wahariri wa vyombo vya habari Jumatatu wiki hii na kulalamika juu ya kuwepo kasi ndogo ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
Katika mkutano huo, Maalim Seif aliweka bayana msimamo wa CUF kwamba hawako tayari kuona uchaguzi huo unarudiwa badala ya kukamilisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Viongozi hao waliokutana kwa zaidi ya saa tano na nusu, walianza kuingia mmoja mmoja Ikulu saa tatu asubuhi na kufanya kikao hadi alasiri.
Pamoja na kutokutolewa kwa taarifa yoyote juu ya kilichojadiliwa na kuamuliwa, ZEC kwa mara ya mwisho waliitaka Kamati Tendaji ya Tume kuandaa mpango kazi wa kurudiwa kwa uchaguzi baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi, Oktoba 28, mwaka jana.
Waraka wa kurejewa uchaguzi ndiyo ajenda kubwa iliyotawala katika kikao hicho cha ZEC pamoja na gharama zitakazotumika katika marudio.
Jecha na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Salum Kassim Ali, hawakupatikana kuzungumzia yaliyojiri katika kikao hicho lakini taarifa zilizopatikana zimedai kumekuwepo na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wajumbe juu ya mustakabali wa uchaguzi huo.
Habari hizo zilidai kwamba baadhi ya wajumbe walikubali kurudiwa kwa uchaguzi huo huku upande mwingine wakipinga.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment