Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema bajeti ya uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar imeshakamilika na kinachosubiriwa ni Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Tamko hilo la serikali lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Alisema serikali imetenga bajeti ya uchaguzi huo ya karibu Sh. bilioni saba ili kufanikisha gharama za uchaguzi huo, baada ya ule wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa rasmi na ZEC na kutangazwa kwenye gazeti la serikali baada ya kubainika udanganyifu hivyo kutokuwa huru na haki.
“Uchaguzi mkuu utarejewa na bajeti yake tayari imekamilika, kinachosubiliwa ni tarehe ya kufanyika kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema.
Aidha, Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, hakuna muda wa kikomo wa kufanyika kwa uchaguzi wa marudo na jambo hilo litategemea ZEC itakavyoamua lini ufanyike.
Aidha, Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, hakuna muda wa kikomo wa kufanyika kwa uchaguzi wa marudo na jambo hilo litategemea ZEC itakavyoamua lini ufanyike.
“Katiba ya Zanzibar haikuweka kikomo cha muda wa kurudia uchaguzi baada ya kufutwa, muda wa siku 90 uliowekwa unatakiwa kutumika kama matokeo ya kura yamefungamana na uchaguzi kulazimika kurudiwa,” alisema na kuongeza:
“Hakuna mbadala wa kumaliza mkwamo wa uchaguzi wa Zanzibar zaidi ya kurudiwa uchaguzi, wananchi waendelea kudumisha amani na mshikamano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwani ni lazima kufanyika kwa sababu kinachofutwa kinakua hakipo hadi kitafutwe kipya.”
Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, amewaimiza viongozi wa Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad kutoka Chama cha Wananchi (CUF) tatizo la uchaguzi wa Zanzibar limalizike kwa wakati muafaka.
“Kuna watu wamekuwa wakipeana taarifa za stori za vijiweni maarufu Zanzibar ‘Drip’ tangu kukwama kwa uchaguzi. Acha wapeani ‘Drip’…uchaguzi wa marudio upo Zanzibar kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Alisema mazungumzo yanayoendelea kufanyika Ikulu ya Zanzibar baada ya mkwamo wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, lengo lake kuu ni kujadili amani na mshikamano baada ya kujitokeza matatizo yaliyovuruga uchaguzi huo.
“Katika mazungunmzo yetu tunazungumza namna ya kuimalisha amani na mshikamano katika nchi yetu na tukimaliza taarifa maalum itatolewa kwa wananchi,” aliongeza kusema.
CUF KUSUSIA SHEREHE ZA MAPINDUZI
Kuhusu viongozi wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kutoka CUF kususia sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa madai Rais Dk. Shein amefikisha ukomo wa kubakia madarakani, Balozi Seif alisema hiyo ni hoja ya kutaka kupotosh wananchi.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 28(1)(a) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Rais ataendelea kuwa Rais mpaka Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar jambo ambalo halijafanyika.
“Kwa msingi huo ndiyo maana SMZ imendelea kuwalipa mawaziri wote wakiwamo saba wa CUF na manaibu waziri watatu kutoka chama hicho stahiki zao kama kawaida,” alisema na kuongeza:
“Mawaziri wanaosema wamejivua uwaziri wanasema kwa utashi wa kisiasa, kwa mujibu wa Katiba na sheria bado serikali inawatambua kuwa ni mawaziri na hadi sasa hakuna aliyerejesha fedha za mshahara wanaolipwa kila mwezi.”
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment