Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, January 21, 2016

SUZA yatia saini mkataba wa mashirikiano na Chuo Kikuu cha Comoro

                                                          



CHUO KIKUU CHA TAIFA (SUZA)
Sanduku la Posta 146, Zanzibar - Tanzania
Simu: + 255 24 2230724/2233337/2234063    Nukushi: + 255 24 2233337
Barua pepe: vc@suza.ac.tz                        Tovuti:http://www.suza.ac.tz

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimetiliana saini mkataba wa makubaliano juu ya mashirikiano na Chuo Kikuu cha Komoro mjini Moroni katika hafla maalum iliyofanyika tarehe 19 Januari, 2016  na kuhudhuriwa na uongozi wote wa Chuo Kikuu cha Komoro, Balozi wa Komoro nchini Tanzania Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Komoro, Bw Mudrik Ramadhan Soragha.

Makubaliano kati ya vyuo hivi ni moja ya matokeo ya ziara ya nchini Komoro ya Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoifanya hivi karibuni.


Profesa Idris Rai, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Dkt Said Bourhani, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Komoro wakisaini Mkataba wa makubaliano ya mashirikiano baina ya vyuo vyao.

Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo, Profesa Idris Rai, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar aliwaeleza wahudhuriaji kwamba ametembea nchi nyingi duniani lakini Komoro ni nchi ya kwanza ambayo amekuwa akijisikia kama kwamba yuko nyumbani tokea alipoingia nchini humo. Alisema kwamba kuna uwiano mkubwa sana baina ya watu wa Zanzibar na watu wa visiwa vya Komoro katika kila nyanja za maisha.

Makamu Mkuu huyo wa SUZA aliwaeleza wana Chuo hao kwamba makubaliano baina ya vyuo hivyo viwili ni tofauti kabisa na mashirikiano ambayo SUZA imekuwa ikiweka saini na vyuo vingine mbali mbali kwani hayo yanahusisha vyuo vya nchi ndugu ambazo zinashabihiana kihistoria, kimazingira, kidini na kiutamaduni.
Aliwahakikishia wanachuo waliohudhuria hafla hiyo kwamba SUZA kwa upande wake itahakikisha mashirikiano ya makubaliano yaliyofikiwa yanapewa kipaumbele na yanatekelezwa kama yatakavyopangwa.


Mkataba huo wa mashirikiano umeainisha mambo ya mashirikiano kama ifuatavyo:
-         kusaidiana kuendesha mafunzo ya lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa upande wa Komoro na lugha ya Kifaransa katika ngazi ya Shahada kwa upande wa SUZA.
-         Kufanya tafiti za pamoja kwenye maeneo ya sayansi jamii na historia, tamaduni, lugha, dini kwa upande mmoja na masuala ya mazingira, rasilimali asilia na bahari kwa upande mwingine.
-         Kubadilishana walimu na wanafunzi baina ya SUZA na Chuo Kikuu cha Komoro.
-         Kusaidiana kujenga uwezo wa wanataaluma wa vyuo viwili hivi kwa maeneo ambayo Chuo kimoja kina uwezo zaidi.
-         Kuandaa mapendekezo ya kuazisha taasisi ya pamoja inayohusu masomo ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Komoro.

Ilibainika kwamba moja ya kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa mashirikiano haya kitakuwa ni lugha ambapo lugha kuu ya taaluma inayotumika katika Chuo Kikuu cha Komoro ni Kifaransa wakati lugha inayotumika SUZA ni Kiingereza na Kiswahili. Mafunzo ya lugha katika makubaliano haya yataweza kuondosha kikwazo hicho hivyo kuwawezesha wanafunzi na wafanyakazi wa vyuo hivi kutembeleana kwa masomo na kushirikiana katika kufanya tafiti za pamoja.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Komoro, Dkt Said Bourhani aliwaambia wanachuo wa Chuo Kikuu cha Komoro kwamba utekelezaji wa mashirikiano haya ni tofauti na mashirikiano na vyuo vingi kwani safari ya Tanzania, Zanzibar kutoka Moroni ni fupi na rahisi. Pia aliwashukuru marais wa Zanzibar na Komoro kwa kufikiria na kutaka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Komoro kuanzisha mashirikiano haya.

Chuo Kikuu cha Komoro na SUZA ni vyuo vichanga lakini vimekuwa kwa kasi kubwa katika miaka ya karibuni. Wakati Chuo Kikuu cha Komoro kilianzishwa mwaka 2003 na kikiwa ni Chuo Kikuu pekee nchini Komoro kikiwa na wanafunzi karibu 9,500 katika masomo ya fani mbali mbali, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kilianzishwa mwaka 2001 na sasa kina wanafunzi karibu 4,000 waliojiunga na masomo kwenye karibu fani 40 katika ngazi za cheti hadi shahada ya uzamivu.

Mara tu baada ya ziara yake nchini Komoro, imekuwa ni hamu kubwa ya Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuona Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kinashirikiana kwa karibu sana na Chuo Kikuu cha Komoro.

No comments :

Post a Comment