Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha
Jana, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza kuwa uchaguzi Mkuu wa visiwani humo utafanyika Machi 20.
Kutangazwa kwa tarehe hiyo kumekuja ikiwa imekaribia miezi mitatu tangu Tume hiyo ilipofuta matokeo ya uchaguzi uliotangulia wa Oktoba 25 ikitaja sababu mbalimbali.
Hata hivyo, hatua hii haiungwi mkono na wadau wote wa uchaguzi visiwani. Inafahamika wazi kwamba chama kikuu cha upinzani CUF kilishatangaza msimamo wake wa kupinga marudio ya uchaguzi huo kikisema ni jambo ambalo halikubaliki. CUF kupitia kwa mgombea wake wa urais ambaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad kinataka matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 yahakikiwe na mshindi atangazwe.
Msimamo huo ni tofauti kabisa na ule wa chama tawala, CCM, ambacho kama ilivyotangazwa na ZEC jana, kinataka uchaguzi huo urudiwe upya.
Tofauti hizo ziliwafanya viongozi waandamizi wa vyama hivyo vikuu Zanzibar na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kukutana kwa miezi kadhaa kutafuta suluhu ambayo hata hivyo, haikuzaa matunda baada ya Maalim Seif na Rais Ali Mohamed Shein kila mmoja kujitokeza hadharani na kutoa misimamo kinzani hadi jana Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha alipojitokeza na kutangaza tarehe hiyo ya kuwachagua Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani.
Kutokana na hatua iliyokuwa imefikiwa ya mazungumzo hadi kutangazwa kwa tarehe hiyo ya uchaguzi, ni dhahiri kwamba kuna kundi kubwa la Wazanzibari hususan wanachama na wafuasi wa CUF ambao hawakubaliani na hatua hiyo.
Hiyo inadhihirishwa na jinsi hali ya usalama ilivyokuwa imeimarishwa jana visiwani humo kuanzia asubuhi kabla ya kutangazwa kwa tarehe hiyo ya marejeo, ambako idadi kubwa ya askari ilionekana mitaani kulinda usalama. Tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi huo Oktoba 28 mwaka jana hadi kuanza kwa mazungumzo ya kutafuta mkwamo wa kisiasa, tumekuwa tukisisitiza kutanguliza masilahi ya Zanzibar na Wazanzibari kwanza. Hata leo baada ya kufikiwa kwa hatua hiyo, bado msimamo wetu unabaki palepale.
Hata hivyo, safari hii tunashauri kasi na umakini viongezwe katika kufikia muafaka wa suala hili ili kuepusha aina yoyote ya mtafuruku. Wakati wengine wakisisitiza kuepusha umwagaji damu katika migogoro ya kisiasa, sisi tunataka kusiwepo hata umwagaji wa machozi.
Kwa kuwa tumekubali kuwa Taifa linaloheshimu utawala wa kidemokrasia, tunaamini pia kwamba sheria, kanuni na busara vitachanganywa katika kapu moja ili kuja na mwarobaini wa mkwamo huu kabla ya tarehe hiyo. Ndoto yetu ni kuona kila Mzanzibari, kama siyo wote kwa idadi kubwa, anashiriki katika kila mchakato wa kidemokrasia visiwani humo kama ilivyokuwa katika chaguzi nyingi zilizopita. Tunawasihi viongozi waandamizi wa CCM na wale wa CUF kurejea katika meza ya mazungumzo na kupata njia bora ya kumaliza mkwamo huo wa kisiasa. Ikiwa uamuzi ni kurejea uchaguzi, vyama hivyo na wadau washirikiane kutafuta njia za kufikia Machi 20 wakiwa wamoja.
No comments :
Post a Comment