Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 16, 2016

Tuwe watu makini,tuzingatie kanuni, taratibu, tusikurupuke!

Jenerali Ulimwengu.
WAKATI tukishuhudia serikali mpya inayoundwa na Rais John Magufuli ikianza kufanya kazi, inatubidi turejee mambo kadhaa ambayo tunaweza kudhani tunayaelewa vyema lakini tukajikuta uelewa wetu una walakini.

Mojawapo ya mambo hayo ni ile hoja ya kujua na kuelewa kwamba nchi hii ipo hapa na itaendelea kuwa hapa kwa muda mrefu ujao. Bila shaka, katika kuwapo kwake itapitia mabadiliko mengi, makubwa na madogo, mema na mabaya, milima na mabonde, lakini itaendelea kuwapo kwa muda mrefu ujao.

Hivyo hatuna budi kupanga mambo yetu kama nchi kwa mtazamo wa muda mrefu. Hii ina maana kwamba tunalazimika kuchukua wasaa, kuwaza, kutafakari na kupanga kwa ajili ya masafa marefu.
 
Pia hatuna budi kupangilia kazi zetu ili kazi ya leo iwe ni msingi wa kazi ya kesho, kama vile kazi ya jana ndiyo imekuwa msingi wa kazi ya leo.Hapa tunatakiwa kujifunza kuangalia mbele kwa masafa marefu, na tupange vivyo hivyo. Ingawaje baadhi ya mipango huangalia vipindi vifupi, kwa mfano bajeti inayoangalia kipindi cha mwaka mmoja baada ya mwingine, mitazamo yetu haina budi kuwa ya kimkakati.

Tunatakiwa kuachana na tabia ya kuendesha mambo yetu kama vile kila wakati tunakabiliwa na dharura. Tunatakiwa tuachane na mtindo wa kufanya kazi kwa mtindo wa “operesheni” isipokuwa pale tu inapobidi. 

Mara nyingi tunapojikuta katika kazi inayofanyika kioperesheni, maana yake ni kwamba kumekuwapo na uzembe ambao umeendelea kwa muda mrefu bila wahusika kuukomesha.

Kwa mfano, tunapojikuta tukiendesha operesheni ya kukomesha kipindupindu, maana yake ni kwamba tumekubali kuishi katika mazingira machafu kwa muda mrefu hadi uchafu tulioulea kwa muda mrefu unapojionyesha waziwazi.

Hivi majuzi tumepata taarifa za maelfu ya makontena ya mizigo yaliyopita katika Bandari yetu bila kulipiwa ushuru, na serikali yetu ikaingia katika operesheni nyingine ya kufukuza maofisa, kuwasimamisha baadhi yao na kuwataka wafanyabiashara husika kulipa ushuru ambao walikuwa hawajaulipa.

Operesheni za aina hii zinadhihirisha jinsi ambavyo mifumo ya utendaji ilivyoporomoka na jinsi ambavyo uzembe umeendekezwa kiasi kwamba inaonekana kama vile serikali ilikuwa imelala.

Serikali makini haina budi kuweka na kusimamia sheria zilizo wazi na zinazoainisha wajibu wa kila mtu na hatua zinazopasa kuchukuliwa iwapo wajibu huo umekiukwa. Serikali makini haipaswi kuruhusu ofisa mmoja, hata angekuwa ni waziri au rais, kuamua kwa utashi wake binafsi nani alipe kodi na nani asilipe kodi. Serikali inayoendeshwa kwa mtindo huo inakuwa ni sehemu ya ile dola ya jinai (criminal state) niliyoijadili hivi karibuni.

Barani Afrika zipo serikali kama hizo zinazoendeshwa na wahuni, na ni jambo la hatari kubwa kwetu sisi kujaribu kuwaiga wahuni hao ambao wamezifikisha nchi zao katika hatua ya kusambaratika. Asiyejua kufa na atazame kaburi, na katika bara hili makaburi yapo ya kutosha, na hatuna sababu yakuongeza jingine hapa kwetu.

Tukijifunza kufanya kazi zetu na kuendesha shughuli zetu kwa mpangilio unaoeleweka, tutazingatia sheria, kanuni na taratibu, na wala hatutakuwa na sababu ya kulipukalipuka kila mara tunapoona mambo hayaendi sawa. Hatutakuwa na sababu ya kuwaona mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya wakikimbizana na maofisa wao.

Wala hatutakuwa na sababu ya kutoa amri zisizotekelezeka kwa sababu tu tunataka kumfurahisha mkubwa wetu. Tumepata uzoefu mkubwa huko tulikotoka. Tumewaona wakuu mbalimbali waliozoea kuendesha shughuli za serikali kwa kutoa amri walizotaka zitekelezwe “ndani ya siku saba” na kweli wahusika wakaonyesha utii kwa kupeleka taarifa kwa mkuu, lakini taarifa hizo zikaja kuthibitika kuwa ni za uongo.

Leo hii tukiangalia hatuoni alama yoyote kwamba jambo la maana lilifanyika wakati ule kutokana na amri za mkuu. Amri hizo hatimaye zinakuwa ni mzaha, na wakati mwingine zinakuwa ni ghali kwa maana ya muda unaopotea na gharama zinazoweza kusababishwa na amri hizo.

Mfano mwafaka wa sasa hivi ni gharama za “bomoabomoa” inayoendeshwa hivi sasa. Hatuna budi tujiulize ni kiasi gani cha akili na fikra waliwekeza wahusika katika operesheni hiyo. Waliketi kweli na kupanga na kuangalia na kupima kile walichokuwa wanakikusudia, au walisema “Hapa kazi tu” kisha wakaenda “kufanya kazi” bila tafakuri.

Msemo wa “Hapa kazi tu” hauwezi kuwa na maana kwamba tufanye kazi bila kufikiri. Tukifika huko tutakuwa tunajiumiza sisi wenyewe.

Tumeshuhudia amri zikitolewa kuwafukuza kazi maofisa ambao wanazo taratibu za ajira zao, na wakati mwingine haiyumkiniki kwamba anayetoa amri ya kuwafukuza anao uwezo wa kisheria wa kufanya hivyo. Tumewaona wakuu wa mikoa au wilaya wakitoa amri za kuwakamata na kuwafunga maofisa waliomo katika maeneo yao kwa sababu hii au ile, mara nyingi ikiwa wazi kwamba hawana uwezo huo kisheria.

Maofisa wanaokamatwa na kufungwa katika mazingira hayo wanaweza kuchukua hatua za kuishitaki serikali kwa kuwanyima uhuru wao, na hata kuwadhalilisha. Nawajua mawakili ambao wangependa sana kuajiriwa kama watetezi wa maofisa hao ili watengeneze fedha nzuri. Hakuna sababu ya serikali kuwapa fursa hiyo kwa kuendekeza tabia za kizamani. Zama za wakuu kuwakamata na kuwatupa watu kizuizini zimekwisha; leo hii tunaona watu wengi wanaojua haki zao na namna ya kuzitetea.

Hatuna budi kujali taratibu katika ngazi zote, iwe ni ngazi ya serikali ya kijiji, utawala wa wilaya, utawala wa ngazi ya mkoa hadi Ikulu. Tusikubali tabia ya kudharau au kupindisha taratibu ama kwa sababu tunaziona kuwa ni ndogo au kwa sababu tuna haraka ya kufanya “kazi tu.”

Hivi majuzi Rais John Magufuli aliteua Baraza la Mawaziri, na katika kufanya hivyo akawateua wabunge kadhaa ambao akawateua tena kuwa mawaziri katika serkali yake. Lakini wakati akiwateua, Bunge lilikuwa limekwisha kuahirishwa, na kwa sababu hiyo hawakuwahi kula kiapo cha ubunge, na kwa sababu hiyo walikuwa hawajawa wabunge. Hiyo ina maana kwamba Rais aliwateua na kuwaapisha mawaziri ambao bado walikuwa hawapata hadhi ya ubunge, tendo ambalo ni kinyume cha Katiba.

Najua hili linaweza kuonekana kama jambo dogo la urasimu na ambalo halina uzito mkubwa kiasi hicho. Mwanasheria mmoja mkongwe aliniambia wakati akijibu hoja yangu kwamba Rais Magufuli hakuwa wa kwanza kufanya hivyo, lakini hoja yangu ni kwamba kama kosa lilikwisha kutendeka huko nyuma hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuliendeleza.

Kadri tunavyosonga mbele ndivyo tunavyotakiwa kuboresha kila jambo tunalolitenda. Tusipofanya hivyo, na badala yake tukajiingiza zaidi katika ushabiki kiasi kwamba hata wanasheria wanashindwa kutetea umuhimu wa kuheshimu sheria, tutajikuta katikati ya vurugu ambazo hazitaturuhusu kupiga hatua yoyote ya maendeleo.

Kuna wakati kundi moja liliingia madarakani likiwa na kauli-mbinu ya “Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya”. Hayati Profesa Seithy Chachage, kwa ucheshi, akaniambia kwamba akizipanga silabi za kwanza za kauli-mbiu hiyo moja chini ya nyenzake, anachokisoma ni ANGUKA.

Mbali na ucheshi, baadaye niliandika kutanabahisha wasomaji kwamba iwapo hujui unakokwenda, ni bure kuongeza ari, nguvu au kasi. Wakati unapohisi kwamba umepotea, ni vyema zaidi kuketi na kutafakari ili uweze kutambua hapo ulipo ni wapi, ulitaka kwenda wapi, na ni wapi ulipopotezea njia ili urejee hapo na kuanza kutafuta njia sahihi kwa uangalifu na umakini mkubwa zaidi. Ukiongeza kasi inawezekana ukawa unazidi kupotea mwituni.

Narudia ushauri wangu ambao niliwahi kuutoa kwa watawala wetu wa awamu mbili zilizopita. Ni dhahiri kwamba nchi imepotea katika mambo mengi na sasa hivi inakwenda bila dira inayoeleweka. Ni muhimu kuketi na kuamua mwelekeo na mustakabali wa nchi ili watawala watakaofuata wawe na dira ya kufuata bila kujali wanatoka chama gani.

Wote wawili, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, ama walipuuza ushauri huo au hawakuuelewa. Baada ya Kikwete kuingia Ikulu kwa ushindi wa kihistoria, mimi binafsi niliamini kwamba alikuwa na fursa ya kipekee ya kuitisha kongamano la kitaifa ambalo lingefanya kazi ya kuchora hiyo dira. 

Badala yake ndiyo tumezidi kupotea hivi kwamba hata mtaa wa mahali anapoishi na kufanya kazi mkuu wa nchi yetu tumepabandika jina la kiongozi wa Ubeberu duniani, Barack Obama. Ni kama vile hatujawahi kuwa na Julius Nyerere. Huko ndiko kupotea njia kweli kweli, kwa sababu imefika wakati siyo tu hujui uendako bali pia hujijui wewe ni nani.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tuwe-watu-makinituzingatie-kanuni-taratibu-tusikurupuke#sthash.wnkHaoIN.dpuf

No comments :

Post a Comment