Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, January 26, 2016

Ukawa wambebesha JPM mgogoro wa Zanzibar

Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa (kushoto), akisalimiana na Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kabla ya kuanza kwa kikao chao na wabunge wa kambi ya upinzani wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mkoani Dodoma, juzi. Katikati ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Vyama vinavyounda Ukawa vimemshukia Rais John Magufuli, kuwa ndiye anayekwamisha kutangazwa kwa rais aliyechaguliwa Zanzibar Oktoba 25, mwaka jana.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya kikao cha Ukawa kilichofanyika juzi.
“Dk Magufuli akiamua wakati wowote matokeo ya Zanzibar
yatangazwe yatatangazwa. Serikali ya CCM imekuwa ikiwapangia Wazanzibari nani awe rais wao tangu kifo cha Karume (Abeid Aman) mwaka 1972,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Rais Magufuli ndiye anayepaswa kulaumiwa kama amani itakosekana Zanzibar. “Ukawa tumeamua kusubiri uamuzi wa Baraza Kuu la CUF ambalo linakutana kesho (leo) Dar es Salaam na baada ya kutoa tamko lao, wabunge wa upinzani wataunga mkono.”
“Magufuli anayevaa magwanda amesahau kuwa yeye ndiye mkuu wa majeshi ambayo yanazunguka mitaa ya Zanzibar. Majeshi yanayowatishia Wazanzibari yako chini yake,” alisema Mbowe huku akisisitiza kuwa Dk Magufuli hawezi kukwepa kupatikana kwa haki Zanzibar.
“Msimamo wetu utapatikana baada ya Baraza Kuu la CUF, ndiyo maana tunawataka wakutane wao na si Chadema kwani kumbukeni aliyepokonywa ushindi alikuwa ni mgombea wa CUF, sisi wabunge tuko pamoja nao,” alisema Mbowe.
Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alisema, “Wakisema tunakwenda kurudia uchaguzi ni nini tutakwenda kufanya? Ni kama refa aliyekataa magoli katika mechi ya kwanza kisha refa huyo huyo akachezesha mechi ya marudiano.”
Taarifa zaidi za ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa African Dream na kuhudhuriwa na Maalim Seif Sharif Hamad, wabunge na viongozi wa Ukawa na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa zinaeleza kuwa, imepangwa mikakati kuhakikisha uchaguzi wa marudio Zanzibar haufanyiki, huku msimamo rasmi ukisubiri kumalizika kwa vikao vya Baraza Kuu la CUF.
Mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar uliibuka Oktoba 28, mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi. Uchaguzi wa marudio Zanzibar umetangazwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
Juhudi za kutafuta suluhisho la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo zilizowashirikisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF ambao wote waligombea urais, zilishindikana. Tayari Maalim Seif ameshajitoa kwenye mazungumzo hayo baada ya vikao tisa.
Lissu aliwaeleza waandishi wa habari jana bungeni mjini Dodoma kuwa Wanzanzibari wamekuwa wakipangiwa rais kwa muda mrefu, kwamba aliyetakiwa kumrithi Karume alikuwa Kanali Seif Bakari, lakini Mwalimu Julius Nyerere alikataa na kuamua Abdul Jumbe awe rais.
Alisema Mwalimu Nyerere aliwaaminisha Wazanzibari kuwa kama wangempitisha Bakar badala ya Jumbe aliyempendekeza, ingeaminika kuwa Karume aliuawa kwa lengo la kimapinduzi.
Alisema hawawezi kwenda mahakamani kupinga matokeo ya urais kwa sababu wanabanwa na Katiba.
Licha ya kutotaka kueleza taarifa za ndani za kikao cha juzi, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaleza kuwa Maalim Seif aliwaeleza wabunge hao hatua zote zilizopitiwa tangu kufutwa kwa uchaguzi huo.
Maalim Seif alinukuliwa akisema viongozi wa CCM waliokuwa wakishiriki mazungumzo ya kutafuta mwafaka, walikiri kuwapo makosa kwenye kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
“Alitueleza kuwa muda wote wa mazungumzo alikuwa akisisitiza kutokubali kurudiwa kwa uchaguzi huo,” zilieleza habari hizo.
Habari zilisema katika kikao hicho, wabunge wa Ukawa walikubaliana kulizungumzia suala la Zanzibar bungeni na jinsi ambavyo kufutwa na kufanyika kwa uchaguzi huo kunavyokiuka sheria na Katiba ya nchi.
“Pia walikubaliana kulipeleka suala hilo katika jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, “ kilisema chanzo chetu.     

/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment