Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, George Simbachawene, ameagiza kuitwa ofisini kwake kwa viongozi wa Manispaa ya Dodoma, Idara ya Elimu, ili wakatoe maelezo ya kwa nini wanachangisha michango.
Simbachawene alitoa agizo hilo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi hizo na kukuta viongozi hao hawapo. Alitaka kujua kwa nini Shule ya Msingi Makulu inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wazazi.
Awali, Waziri huyo alizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake aliokuwa akiwafafanulia kuhusu fedha za elimu bure, lakini alikatisha mazungumzo hayo baada ya swali la mwandishi aliyeuliza ni kwanini shule ya Makulu inaendelea kuwachangisha michango wazazi.
Aliondoka ofisini hapo akiongozana na baadhi ya maofisa wa wizara na kuelekea katika shule hiyo kwa lengo la kwenda kuthibitisha alichoulizwa.
Alipofika, alielezwa kuwa wamepatiwa kibali na ofisi ya Elimu, Manispaa ya Dodoma.
“Hili halikubaliki hata kidogo, sisi tumetoa waraka Namba 6, 2015 kuzuia michango halafu maofisa wa manispaa wanatoa maagizo mengine, twendeni kwao,” alisema Simbachawene baada ya Mwalimu Mkuu, Janeth Justine kumuonyesha barua ya kutakiwa achangishe.Akitoa ufafanuzi kuhusu fedha zilizopelekwa katika shuleni mbalimbali nchini, alikiri kuwa ni kiasi kidogo, lakini alisisitiza kitumike kama ilivyoelekezwa.
Hata hivyo, Mwalimu wa Justine alithibitisha wazazi kuagizwa wachangie huduma za maji, umeme na mlinzi.
Kaimu Katibu Mkuu Tamisemi, Benard Makali, aliagiza uongozi wa Manispaa ya Dodoma kufika leo ofisini kwa waziri wakiwa na majibu ya kwanini wamepuuza maagizo yaliyotolewa na Serikali.
No comments :
Post a Comment