Umoja huo umesema wao hawaoni suala la Tegeta Escrow kama bado ni ajenda mpya inayopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa.
Umesema kuendelea kulijadili suala hilo bungeni ni sawa na kutaka kufifisha na kupunguza kasi ya utendaji wa Rais Dk. John Magufuli ambaye ameonekana kuwa mtetezi wa wanyonge.
Hayo yalisemwa na Katibu wa umoja huo, Renatus Muabi, wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
"Tunaamini kwamba serikali iliyopita ya awamu ya nne ilipokea mapendekezo ya Bunge lililopita na kuyafanyia kazi, tuliona baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali wakiachia ngazi na wengine kuhojiwa kwenye vyombo mbalimbali vyenye mamlaka husika,” alisema.Muabi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), alivitaja vyama vinavyounda umoja huo kuwa ni NRA, AFP, Sau, CCK, Chausta, Demokrasia Makini, ADC, UPDP, AFP, TLP, UDP,
Tadea, Jahazi Asilia na Chauma.
"Sisi tunaona escrow ni jambo jepesi ambalo halistahili kutuchukulia muda mrefu au hata Bunge kuliwekea umuhimu na kulipa kipaumbele, tunaamini kwamba serikali hii ya Rais Magufuli imejipambanua kuwa inataka kufanya kazi ambazo zitakuwa na tija kwa taifa," aliongeza kusema.
Alisema ni kwa msingi huo makatibu wakuu hao hawaoni suala hilo ni muhimu kwa sasa kuliko hali ya kisiasa Zanzibar na mchakato wa kupata Katiba mpya.
UCHAGUZI KURUDIWA Z’BAR
Vyama hivyo vimesema kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kama ilivyotangazwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) si haki ya kidemokrasia.
Muabi alisema mwendelezo wa mazungumzo kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamekuwa ni ya siri takriban vikao 10 ambavyo wananchi pamoja na viongozi wengine wa kisiasa wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo visiwani Zanzibar hawajui kilichokuwa kinajadiliwa na vyama hivyo viwili, huku ikieleweka kwamba Zanzibar si ya CCM wala CUF pekee.
"Sisi makatibu wakuu wa vyama visivyo na uwakilishi bungeni kama wadau muhimu wa siasa tunatoa msimamo wetu kwamba tumesikitishwa na kushangazwa na vyama vya CUF na CCM kuliteka suala la mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kuufanya ni mgogoro wa vyama viwili pekee ambavyo vimekuwa na mazungumuzo ya muda mrefu kuhusu kutafuta muafaka wa mgogoro huo pasipo kushirikisha vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi huo vipatavyo 12 katika nafasi mbalimbali zikiwamo na za urais," alisema Muabi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment