NA EDITOR
26th January 2016.
Katika mkutano huo, wananchi watapata fursa ya kuwashuhudia na kuwasikiliza wabunge wakijadili masuala mbalimbali yanayoikabili nchi wakati wa vikao hivyo.
Vikao hivi vinafanyika katika kipindi ambacho Watanzania wana njaa ya mabadiliko ya kutaka kuona taifa lao likipiga hatua kimaendeleo.
Baada ya miaka 55 ya Uhuru ni aibu kwa taifa la Tanzania lenye rasilimali nyingi likihesabiwa miongoni mwa mataifa maskini duniani.
Sio siri uchaguzi ulifanyika mwaka jana na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu vyama vya upinzani vitakuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Katika huola vyama vya upinzani vitakuwa na jumla ya wabunge 110, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiongoza kikiwa na wabunge 66. Chama cha Wananchi (CUF) kina wabunge 42 wakati vyama vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo vina wabunge mmoja kila kimoja.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina wabunge 265 katika Bunge hili, hivyo kitaendelea kuwa kinara.
Ni wazi kuwa wabunge pamoja na kwamba wanawawakilisha wananchi, lakini pia watakuwa na jukumu la kuwakilisha ma kutetea misimamo vya vyama vyao.
Hata hivyo, wabunge wanapaswa kuelewa kuwa wana dhamana ya kuwakilisha wananchi na kuzingatia maslahi ya taifa na sio kujikita tu kwenye siasa za vyama kwa kuzingatia kuwa taifa letu linakabiliwa na changamoto nyingi.
Itakumbukwa kuwa tangu nchi yetu ipate uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita, imekuwa katika vita dhidi ya maadui watatu ujinga, umaskini na maradhi. Ni maadui hao ambao wamesababisha nchi yetu kuchelewa kupata maendeleo licha ya kuwa na rasilimali lukuki.
Hata hivyo, pamoja na kupita awamu nne za uongozi, lakini bado vita hiyo haijafanikiwa kwa kiasi kinachotarajiwa na wengi. Mathalani, Tanzania ilikuwa haipishani kiuchumi na nchi za bara la Asia za Korea Kusini, Hong Kong, Taiwan na Singapore katika miaka ya 1950 na 1960.
Hata hivyo, nchi hizo zimeipita Tanzania kiuchumi kutokana na kufanya mapinduzi makubwa ya elimu, huduma za afya na kuinua maisha ya raia wake. Nchi hizo nne hizi hujulikana na jina la `Asia Tigers’ (Chui wa Asia) kutokana na kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi licha ya rasilimali ilizonazo.
Wananchi walio wengi wanaamini kuwa viongozi na watendaji wa serikali ndio chanzo cha nchi kushindwa kupiga hatua kimaendeleo kutokana na utendaji wa kiwango cha chini.
Kwa kuwa sote tunafahamu kuwa jukuku la Bunge ni kuisimamia serikali, ni matumaini yetu kuwa wabunge watazingatia jukumu lao na kuzingatia maslahi mapana ya taifa pale wanapotekeleza majukumu yao.
Wananchi wahawatarajii kuona wabunge wakiendekeza mipasho ya kisiasa ndani ya Bunge badala ya kutetea maslahi ya wananchi.
Hata hivyo, haya yote yatafanikiwa ikiwa uongozi wa Bunge nao utazingatia weledi na kutenda haki wakati utakapokuwa unasimamia shughuli za bunge. Spika na Naibu Spika wanatakiwa kutenda haki na kuwa tayari kutoa usawa kwa wabunge wote bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Viongozi hao wanapaswa kutanguliza maslahi ya taifa, kwa kudumisha demokrasia na kuzingatia kanuni za Bunge la Jamhuri ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment