Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Jaji mstaafu Joseph Warioba akizungumza wakati wa kongamano la saba la jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo
Dar es Salaam. Wasomi wameitaka Serikali kuanza mchakato wa Katiba mpya ili kuunda Tume Huru ya Uchaguzi.
Wakizungumza katika mdahalo uliotayarishwa na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutathmini hali ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wasomi hao walisema tangu mfumo wa vyama vingi uanze nchini mwaka 1992 kumekuwa na malalamiko kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokuwa huru na haki kutokana na namna wajumbe wake wanavyopatikana.
Mdahalo huo uliongozwa na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba na Profesa Issa Shivji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jesse James alisema wajumbe wa NEC kuchaguliwa na Rais ndicho chanzo cha tume kuonekana kuwa si huru na kuwa na mfumo usio shirikishi.
“Mfumo mzima wa usimamiaji wa chaguzi kuwa chini ya wakurugenzi ambao ni waajiriwa wa Serikali kwa vyovyote hawawezi kufanya uamuzi tofauti na matakwa ya Serikali,” alisema.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Lupa Ramadhani alisema uchaguzi huo uligubikwa na viashiria vya upendeleo katika vyama pamoja na kutawaliwa na matumizi makubwa ya fedha.
“Hii inaonyesha kuwa chama chenye fedha nyingi kina uhakika wa kushinda kutokana na kujimudu kifedha,” alisema.
Alifafanua kuwa katika uchaguzi uliopita, rushwa ilionekana wazi kutokana na ubutu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambayo haijafafanua utendaji wake na mwingiliano kati ya dini na siasa.
Dk Ayoub Rioba wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ya UDSM, alisema ni vyema ikawepo taasisi maalumu ya kushughulikia demokrasia ya vyombo vya habari na mikutano ya mara kwa mara ya majukwaa ya wahariri ili kuhamasishana jinsi ya kuripoti habari kwa usahihi.
No comments :
Post a Comment