Chama cha wananchi CUF chasema hakitarudi kwenye meza ya mazungumzo kutafuta suluhu ya kisiasa Zanzibar mpaka pale mchakato wa uchaguzi wa marudio utakapositishwa.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na aliyekuwa mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, wamekutana jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kulaani vurugu wanazofanyiwa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Viongozi hao walikutana jana kwa mazungumzo mafupi katika ofisi za Lowassa zilizoko Mikocheni, na kisha kutoa tamko hilo.
Tamko hilo lilielekeza lawama kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa anawafumbia macho watu ambao wamekuwa wakipita kwenye nyumba za wafuasi wa (CUF) na kuwafanyia hujuma mbalimbali.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa jana, Maalim Seif alisema kwa kuwa CUF ilijitoa kwenye uchaguzi wa marudio, walitarajia CCM iendelee na taratibu za maandalizi ya uchaguzi huo ambao wana uhakika wa kushinda kwa asilimia 100, kwa kuwa hawana mpinzani.
Lakini hali imeanza kuwa tofauti visiwani Zanzibar.
Alisema katika hali ya kushangaza, serikali ya Zanzibar imeanza kutoa vitisho kwa wananchi hasa kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF, ambapo wamekuwa wakipigwa, kujeruhiwa na wakati mwingine kuporwa mali zao lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na vyombo vya dola.
Alisema katika hali ya kushangaza, serikali ya Zanzibar imeanza kutoa vitisho kwa wananchi hasa kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF, ambapo wamekuwa wakipigwa, kujeruhiwa na wakati mwingine kuporwa mali zao lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na vyombo vya dola.
“Yanayoendelea Zanzibar ni kama hakuna serikali, watu wanaoficha sura zao wamekuwa wakipita kwenye ngome za CUF na kuwafanya wananchi wanavyotaka, nimemweleza Makamu wa Pili wa Rais, amesema hajui, nimemweleza Rais Dk. Shein naye ati anasema hajui suala hilo," alisema Hamad.
"Sasa niliwaambia kama hamjui mimi ndiyo nimewaambia, lakini vile vile hawajachukua hatua zozote.”
KADI ZA KUPIGIA KURA
Katika hatua nyingine, Maalim Seif alisema wafanyakazi wa Serikali wameamriwa wamepeleke vitambulisho na shahada zao za kupigia kura kwa waajiri wao ambavyo huwekewa kumbukumbu ili iwe rahisi kwa serikali kuwatambua wafanyakazi ambao hawakwenda kupiga kura.
“Hii si mara ya kwanza kutokea Zanzibar, wakati fulani tuliposusia uchaguzi ilishawahi kutokea wafanyakazi kutakiwa kupeleka vitambulisho na kisha kufanyiwa upembuzi kujulikana nani alikwenda kupiga kura na nani hakwenda na mwisho wa siku wale waliobainika kwamba hawakwenda kupiga kura wote walifukuzwa kazi,” alisema Maalif Seif
Alisema katika tukio la juzi, watu waliofunika nyuso zao walifika maeneo ya Michenzani na katika ofisi za CUF sehemu inayoitwa Msumbiji, eneo lenye wafuasi wengi wa chama chake ambako walipiga watu ovyo ovyo na kuvunja maduka na kupora bidhaa mbalimbali.
Maalim Seif alisema katika maeneo ya Jang’ombe pia watu hao waliwavamia wananchi kuwapiga na kuwajeruhi lakini hakuna hatua zozote walizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na badala yake vyombo hivyo navyo vimekuwa vikijidai kushangaa kuhusu watu wanaofanya vurugu hizo.
CHANZO: THE GUARDIAN
No comments :
Post a Comment