Uamuzi huo ni pamoja na kusimamisha watendaji wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Hatua hiyo iliongeza mapato ya Desemba, mwaka jana hadi kufikia Sh. trilioni 1.4 kutoka wastani wa Sh. bilioni 900 kwa mwezi.
Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, kwa kile kilichoelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kwamba Rais hajaridhishwa na utendaji wa taasisi hiyo.
Pia ilimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito, ili kupisha uchunguzi kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ununuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati.Serikali ya Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika ukusanyaji wa kodi na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na ubadhilifu wa fedha za umma kuanzia ngazi ya chini hadi juu na tayari baadhi ya watu wamewajibishwa, ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Vigogo saba wa TRA wamefikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, kusimamishwa kazi na anachunguzwa, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka kuondolewa na kuvunja Bodi ya TPA ni miongoni mwa mambo mengine yaliyoleta mtikisiko katika serikali ya Magufuli ndani ya siku 100.
Katika kukabiliana na matumizi mabaya ya fedha za umma, Rais alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu, na kusimamisha kazi vigogo wengine wanne, kupisha uchunguzi wa ufisadi wa zaidi ya Sh. bilioni 179.6 katika mradi wa vitambulisho vya taifa.
Miongoni mwa mambo yaliyompa sifa Rais katika kipindi hiki alichokaa madarakani ni pamoja na kufuta shamrashamra za sherehe za Uhuru zilizokuwa zifanyike Desemba 9 ,mwaka jana, na kuamuru Sh. bilioni nne zilizokuwa zitumike kwenye sherehe hizo kupanua barabara ya Morocco-Mwenge, Dar es Salaam ambayo ujenzi wake unaendelea.
Rais magufuli pia aliagiza zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya vinjwaji na viburudisho kwenye hafla ya kuzindua Bunge, zitumike kununulia vitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Vitanda 300 vilipatikana kutokana na fedha hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment