Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, February 13, 2016

SIKU 100 ZA JPM: Kasi ya Rais Magufuli ilivyowaliza waliojenga mabondeni D’Salaam

Polisi wakisimamia kazi ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kwenye bonde la Msimbazi eneo la Mkwajuni, Wilayani Kinondoni, Dar es Salaam. Picha na Maktaba
By Jackline Masinde, Mwananchi
Leo zimetimia siku 100, tangu Rais John Magufuli alipoingia katika Ikulu kuwatumikia wananchi, lakini baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali yake zimewaachia vilio na majonzi baadhi ya wananchi, hasa wale walioathiriwa na uamuzi wa kubomoa nyumba zilizojengwa katika maeneo yasiyostahili kuishi binadamu kama vile mabondeni.
Majonzi hayo yalikuja baada ya Serikali ya Magufuli kutangaza kiama cha kubomoa nyumba zote zilizo ndani ya mita 60, kutoka kwenye kingo za mito na mabondeni, lengo likiwa ni kuondokana na majanga ya mafuriko yanayoweza kutokea.
Agizo hilo lilianza kutekelezwa Desemba mwaka jana, ikiwa ni mwezi mmoja na siku kadhaa tangu kuapishwa kwake na kuacha wakazi zaidi ya 200,000 wakiwa hawana makazi.
Operesheni ya kubomoa nyumba ilianzia maeneo ya Mwenge, Kinondoni na Temeke Jijini Dar es Salaam na baadaye iliendelea mikoa mingine, ikiwamo Arusha na Iringa huku ikisimamiwa na Baraza la Taifa la Uhifadhi Mazingira (NEMC), halmashauri na Jeshi la Polisi.
Wananchi ambao nyumba zao zilikumbana na kadhia ya ubomoaji, wanasema kuwa siku 00 za Rais Magufuli madarakani, hazijawasaidia lolote zaidi zimewaongezea hali ngumu ya maisha huku wakijutia kumchagua.
“Kiukweli siku 100 za Magufuli nimeziweka kwenye rekodi yangu, zimenifanya maisha yangu kuwa tofauti, kwani nalala nje kitu ambacho nilikuwa ninakisikia tu kwenye vyombo vya habari,” anasema Erasto Majani mkazi wa bonde la Mkwajuni.
Wanasema wamekuwa ombaomba kwa kukosa makazi, wengine wamebadilisha mtindo wa maisha yao kwa kulala juu ya vifusi, wamepoteza ndugu na jamaa zao kwa mstuko wa kubomolewa nyumba zao.
“Haya ni maisha mapya aliyotuletea Magufuli, mpaka najuta kwa nini nilimchagua, nilijua atakuwa mtetezi wa wanyonge kama alivyokuwa anatuahidi kwenye kampeni zake, lakini ametugeuka ,” anasema Isabela Philipo, mkazi wa Hananasifu.
Wananchi hao wanasema uwepo wa Magufuli kumewafanya wamkumbuke Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwani alikuwa na huruma na wananchi wake.
“Magufuli amenifanya nimkumbuke Kikwete pamoja na mapungufu aliyokuwa nayo, lakini alikuwa na roho ya utu, hakutaka kabisa tuvunjiwe nyumba zetu,” alisema Ally Gambo.
Operesheni ilivyokuwa
Operesheni ya bomoabomoa iliendeshwa kwa awamu mbili, ya kwanza ilihusisha wakazi wa Mwenge, Pugu Mnadani na Temeke na nyumba zaidi ya 700 zilibomolewa.
Awamu ya pili ilihusisha ubomoaji wa nyumba za bonde la Msimbazi maeneo ya Kigogo, bonde la Mkwajuni, kata ya Hananasifu Manispaa ya Kinondoni.
Awamu hii ilihusisha ubomoaji wa nyumba zaidi ya 8,000 huku ikiacha vilio simanzi na majonzi kwa wakazi wa maeneo hayo, watu wakipoteza maisha na wengine kupata maradhi ya kupooza.
Bomoabomoa yasitishwa
Kutokana na kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali , Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na NEMC ilisimamisha shughuli ya ubomoaji kwa muda wa siku 14 ili kuwapa nafasi ya kuhamisha mali zao wenye nyumba zilizotakiwa kubomolewa huku ikiwataka wananchi hao kubomoa wenyewe nyumba zao.
“Kama unafahamu umejenga nyumba yako eneo ambalo halitakiwi kisheria, tafadhali vunja mwenyewe kwa kuwa bomoabomoa itarudi kwa nguvu,” alisema Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Aliongeza: ”Ukibomoa mwenyewe utaondoka salama na vyombo vyako, milango, madirisha hata matofali lakini ukisubiri , vyote hivyo vitaharibiwa.’’
Januari 5 shughuli ya ubomoaji iliendelea maeneo ya Bonde la Msimbazi, Mlalakua, Mbezi Beach na Kawe.
Bomoabomoa yapingwa
Wakati NEMC ikianza tena kazi ya kubomoa nyumba zilizoko katika maeneo hatarishi kwa makazi ya binadamu baada ya kusimamishwa kwa muda wa siku 14, Mahakama Kuu ilizuia kuendelea kwa zoezi hilo baada ya wakazi 674 waliovunjiwa nyumba zao kufungua kesi kupinga ubomoaji .
Aidha, aliyekuwa Meneja Kampeni wa Magufuli, Abdallah Bulembo, alipinga ubomoaji wa nyumba hizo akidai kuwa utamjengea chuki Rais kwa wananchi .
“NEMC wasiwe kama wameshuka kutoka mbinguni..., wasituharibie imani ya wananchi kwa Rais... kwani walikuwa wapi siku zote mpaka wasubiri Rais Magufuli kuingia madarakani? Sikubaliani na bomoabomoa hiyo,” alisema.
Mabomu yarindima
Baadhi ya vijana na wananchi ambao nyumba zao zilibomolewa walifunga barabara na kuchoma mataili kupinga uwekaji alama ya X kwenye nyumba zilizoko mabondeni.
Vurugu hizo zilisababisha askari kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wamefunga barabara.
Tangu ubomoaji usitishwe na mahakama, hali imetulia kidogo, wananchi wanaendelea na maisha yao mabondeni na bado hawataki kuhama pamoja na kuwa baadhi nyumba zao tayari zimeshabomolewa, waliosalia wanasubiri hatima ya kesi yao.  

No comments :

Post a Comment