Toleo la 444
10 Feb 2016
Kuna misimamo ya aina mbili katika suala la mgogoro wa Zanzibar. Wapo wanaoamini kuwakufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar lilikuwa ni jambo sahihi kwa sababu ni hujuma na wizi wa kura ulivyofanywa kukinufaisha Chama cha Wananchi (CUF).
Kundi la pili ni wale wanaoamini kuwa kufutwa kwa matokeo sio tu ilikuwa ni ukiukwaji wa katiba na sheria ya Zanzibar, lakini pia ulifanyika kwa lengo la kukiokoa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa kikielekea kushindwa na wapinzani wao wakuu, CUF.
Katika maandiko yangu yaliyopita, nimekuwa nikiweka wazi kuhusu msimamo wangu kuhusu Zanzibar. Kwamba, kama Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa kidemokrasia ya vyama vingi, Zanzibar haifikii kabisa kipimo hicho na kwamba CCM naamini wamekuwa wakicheza rafu sio tu katika uchaguzi huu bali tangu 1995.
Lipo tabaka moja la watu, wale waliounga mkono kufutwa kwa matokeo na pia wanaootaka marudio, wanaoamini kuwa wenzao hawastahili kutawala kwa sababu sio wanamapinduzi. Hili ni tabaka la watu wanaoiishi historia na kuiruhusu iamue maisha ya kisiasa ya Zanzibar ya sasa.
Ushahidi upo wazi. Wanasiasa wa upande mmoja wamekuwa wakisema serikali waliyoipata kwa kupindua haitotolewi kwa vipande vya karatasi.
Mtazamo huu unaenda sambamba na vitendo na maneno ya kubaguana kati ya jamii ya Wazanzibar, ubaguzi ambao wakati fulani huchukua sura ya rangi (kama tulivyoona juzi kwenye bango katika sherehe za Mapinduzi), na wakati fulani huchukua sura ya mahali asili ya watu watokeapo.
Wafadhili na misaada
Imekuwa ni kawaida kwa wazungumzaji wengi wa vyama vya upinzani kuitishia Serikali ya Awamu ya Tano kuwa itakosa misaada kwa kushindwa kutenda haki katika suala la Zanzibar na hivyo kushindwa kufikia malengo yake. Ni kweli, wafadhili wakigoma kusaidia, serikali inaweza kuathirika. Lakini inaweza pia isiathirike.
Lakini je, shinikizo hilo la kuinyima Tanzania misaada ni njia sahihi ya kuwafanya watawala wa kiafrika kutenda haki? Vipi kama wafadhili wasingekuwepo? Vipi kama sisi ndio tungekuwa nchi wafadhili ambao hatuhitaji sana misaada.
Kudai kuwa nchi itaenda mrama kwa sababu ya kukosa fedha za wafadhili ina maana kwamba kama Tanzania itaweza kujiendesha bila misaada basi suala la Zanzibar linaweza kufunikwa na maisha ya dhuluma yakaendelea kama kawaida.
Maalim Seif Sharrif Hamad na timu yake ya CUF wamekuwa wakipenda kufanya ushawishi kimataifa kupata uungwaji mkono nje ya nchi kwa mafanikio makubwa. Safari hii tunasikia wameandika barua hadi kwa Papa Francis huko Vatican. Lakini ukweli ni kwamba hata wafadhili wakiweza kushinikiza, tatizo la msingi la Zanzibar halitaondoka.
CCM hawataacha kuamini kuwa wao pekee ndio wanaostahili kutoa rais kwa sababu tu ya shinikizo la wafadhili. CCM wanaweza kufanya michezo ya kanyaboya ili tu wafadhili waridhike lakini wakaendeleza mipango yao ya siku zote.
Katika upana wake suala la kukimbilia kwa wafadhili kupata suluhisho kupitia mbinyo kwa watawala ni muendelezo vitendo vya Waafrika vya kujidhalilisha na kuwaruhusu wafadhili waendelee kuingilia mambo yetu ya ndani. Leo wanaingilia suala zuri, la haki lakini kesho watasema hatutoi fedha mpaka mhalalishe ushoga!
Pia, CUF wasione kuwa vita hii ya kutumia wafadhili ni rahisi sana. Ni ngumu na CCM pia wanaweza kuicheza.
Tunakumbuka makala iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakati wa kampeni katika jarida moja maarufu huko nje akinasibisha muungano wa upinzani na masheikh wa Uamsho, ambao vyama vya Ukawa, kupitia mgombea wao wa urais, viliahidi kuwaachia huru, ingawa baadaye wakaikana ahadi hiyo.
Katika makala ile yenye kichwa cha habari, ‘Tanzania cannot be allowed to be the new front for terrorists,’ Kinana anasema ni kundi la Uamsho ndilo limekuwa likifanya vitendo vya ugaidi visiwani humo ikiwemo kumwagia tindikali watu, wakiwemo, mapadri, watalii na wageni wengine. Aidha, Kinana alidai Uamsho wana uhusiano na makundi ya kigaidi, ikiwemo Boko Haram la Nigeria.
Pia kumekuwa na tetesi zinazoenezwa kuwa lengo la CUF ambao wanataka serikali tatu ni kuua Muungano na kisha kurudisha Waarabu na kutangaza taifa la Kiislamu. Ushahidi mzuri wa fikra hizi ni kauli ya Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliyoitoa kanisani akifafanua kwa nini Tanganyika inaihitaji Zanzibar.
Ukisoma maneno yake utagundua kuwa kudhibiti visiwa vile ni muhimu kwa Tanganyika kinachoitwa undugu wa watu wa pande hizo mbili.
Tutegemee CCM kutumia propaganda hizi kutafuta uungwaji mkono wa wafadhili ambao pamoja na kudai kuipenda sana demokrasia penye tishio la ugaidi wataunga mkono hata dikteta muuaji kuliko kuruhusu demokrasia ifanye kazi.
Tishio la machafuko
Kuna tabia nyingine iliyozuka ya kutishia kuzuka machafuko kama njia ya kuibinya serikali ikubali kutenda haki Zanzibar. Vitisho hivi sio vizuri kwani fujo zikitokea watakaoumia ni wananchi hao hao ambao wanasiasa wanadai inataka kuwakomboa kutokana na umaskini, maradhi na ujinga.
Tatizo kubwa ninaloliona ni pale wanasiasa wa upinzani wanapolizungumzia suala la machafuko ya amani kimzahamzahakuitishia CCM. Ijulikane kuwa iwapo wafuaisi wa CUF wataingia mitaani na kupinga vitendo vya dhuluma, CCM hawatawageuzia shavu la kushoto bali vitatumiwa vyombo vya dola kuwamaliza kabisa.
Matumizi ya vyombo vya dola kuua na kuukandamiza upinzani ni moja tu kati ya machaguo ambayo CCM wanayo. CCM wanaweza pia wakatumia nafasi hiyo kufanya mapinduzi mapya kama ya 1964, kukoleza wino na kutengeneza mashujaa wapya.
CUF wanapaswa wajifunze kwa uzoefu wa walioyapitia kama chama. Januari 26, 2001 idadi inayobishaniwa ya wafuasi wa CUF waliuawa kwa risasi baada ya kufanya maandamano wakilalamikia uchaguzi wa mwaka 2000. Tukio kama lile haliapaswi kurudiwa tena. Pia ikumbukwe CUF ina wafuasi zaidi wengi Pemba, huku Unguja ambako ndio makao ya serikali, CCM wakiwazidi, ingawa inaaminika Wapemba wengi wana maslahi makubwa ya kiuchumi Unguja.
Binafsi, naelewa na naamini kuwa kuandamana ili kufikisha ujumbe ni haki ya raia lakini haki hii haijawahi kuheshimiwaTanzania sio Zanzibar tu bali hata Bara. Huku bara tumeona mara kadhaa polisi wakizuia maandamanio bila sababu yoyote ya maana na wale waliojaribu kukiuka walikiona cha mtema kuni.
Inauma sana kuona chama kinanyan’ganywa ushindi. Lakini, uhai na usalama wa watu ni jambo la msingi sana. Matamko yanayotolewa na viongozi wa serikali ya CCM kuwa wamejidhatiti kupambana na wafanya fujo katika uchaguzi wa marudio hayapaswi kudhauliwa.
Magufuli ana nguvu Zanzibar?
Swali langu hilo linaweza kuwa na utata. John Magufuli ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania. Kwa hiyo, ni kweli kuwa yeye ana nguvu kubwa. Hata hivyo, kumtegemea kuwa ataweza kumaliza mgogoro kutokana na nguvu zake hizo nio ndoto.
Magufuli anahitaji nguvu za aina mbili ili aweze kuleta suluhu Zanzibar. Kwanza, Magufuli anahitaji nguvu ya kikatiba ya kuingilia mgogoro wa Zanzibar kwa maana ya kuamua suluhu iweje. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC), Jaji Damian Lubuva, Rais hana nguvu hizo.
Nguvu nyingine ambayo Magufuli anahitaji ni ile ya ushawishi wa kisiasa. Je anayo? Nguvu zinazotawala siasa za Zanzibar ni kubwa na zenye mashiko ya kihistoria.
Ni kubwa kiasi kwamba inaaminika kuwa moja ya sababu ya Salim Ahmed Salim kushindwa katika kinyang’anyiro cha nafasi ya urais mara zote jina lake lilipojitokeza ni upinzani kutoka Zanzibar. Kwa nini? Kwa sababu yeye anatajwa kuwa ni Hizbu.
Suluhu ni nini?
Suluhu ya Zanzibar itapatikana kwa mazungumzo ya pande mbili. Na mazungumzo hayo yasilenge tu kutatua mgogoro wa sasa bali pia kutibu majeraha ya muda mrefu kati ya matabaka mawili ambayo najua kuwa hayaishii tu katika siasa bali hata katika ngazi ya jamii.
Maswali muhimu ya kujiuliza ni vipi Wazanzibar wanaweza kuondoa tofauti zao na kushirikiana katika kuongoza visiwa vyao. Katika mijadala hiyo Wazanzibar lazima wakubali kufikiria nje ya boksi la demokrasia waliyoveshwa wakati haifanyi kazi.
Katika umri huu nilioshi nimejifunza mkitaka kuelewana na ndugu yako mliokosana, ongeeni wenyewe msitafute mtu wa tatu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tunapokosea-katika-kuliangalia-suala-la-zanzibar#sthash.ynHTy2ez.dpuf
No comments :
Post a Comment