Ufugaji vipepeo ni biashara yenye faida kubwa na kwa kiasi kikubwa, imeweza kuwanufaisha wanakijiji wa Pete na maeneo jirani ya kijiji hicho, kilichpo mkoa wa Kusini unguja.
Ufugaji huo ni njia bora ya kujikwamua kiuchumi, lakini kiafya kwa wananchi wa kijiji cha Pete, wameweza kuhifadhi mazingira kutokana na ufugaji huo wa vipepeo.
Asha Mohammed, ni mfugaji vipepeo wa kijiji cha Pete, ambaye awali shughuli zake zilikuwa kukata kuni kwa ajili ya biashara, bila ya kujua athari za ukataji wa miti.
“Kabla ya biashara hii, nilikuwa nakata kuni na huwa nalazimika kuingia katika Msitu wa Hifadhi ya Jozani kwa ajili ya kukata miti ili niweze kupata kuni, lakini kwa sasa shughuli hiyo nimeiacha,” anasema Asha.
Kijiji cha Pete kimezungukwa na Msitu wa Hifadhi wa Jozani, ambao ni msitu mkubwa kwa Zanzibar, ukifuatiwa na msitu wa Ngezi uliopo kisiwani Pemba.
Asha ambaye ni mfugaji vipepeo, anasema baada ya kuonekana kuwa wanakijiji wamejikita zaidi katika kuushambulia msitu wa Jozani, kwa kufanya shughuli za kijamii, ikiwemo kukata miti kwa ajili ya kuni za biashara na utengenezaji mkaa.
Anasema kuwa, kupitia Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira wa Msitu wa Jozani, walipatiwa mafunzo ya ufugaji vipepeo, ili kuachana na shughuli za uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti.
Anasema kuwa, kupitia Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira wa Msitu wa Jozani, walipatiwa mafunzo ya ufugaji vipepeo, ili kuachana na shughuli za uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti.
“Biashara ya ufugaji wa vipepeo ni nzuri na kwa kweli imetukomboa kiuchumi, wananchi wengi wa kijiji hiki cha Pete na kwa upande wetu sisi wanawake, tumeacha utegemezi kutoka kwa waume zetu,” anasema Asha.
Anasema imetimu miaka mitano sasa, tangu waanze biashara hiyo ya vipepeo, ambayo imempatia faida kubwa, ikiwemo kuwezesha kusaidia kuhudumia familia yake ya watoto watano na mahitaji mbalimbali, ikiweme ya shule.
Asha anasema kuwa, jinsi shughuli za ufugaji vipepeo ulivyo, wanalazimika kwenda kwenye misitu kuwinda vipepeo na kisha wanawafuga kwa utaratibu maalum, ili wawawezeshe kutaga na vipepeo wadogo ndio wanaouzwa.
Kwa mujibu wa Asha, vipepeo hao wadogo huuzwa katika kituo kikuu cha ununuzi wa vipepeo kinachojulikana kwa jina la Zanzibar Butterfly Centre (ZBC)) kilichopo kijijini hapo.
“Namshukuru Mungu, biashara nzuri si haba. Tunapata pesa na zinatusaidia katika harakati zetu mbalimbali,” anasema mfugaji huyo wa vipepeo.
Asha anasema kuwa, biashara ikiwa nzuri kwa mwezi wanaingiza wastani wa Sh. 400,000 na ndio chanzo cha fedha anachokitegemea.
Anafafanua kuwa, katika kipindi cha mvua za Vuli, vipepeo wanapatikana kwa wingi msituni, kutokana na mimea na miti inakuwa imenawiri na kutoa maua.
Juma Khamis, ni mfugaji mwingine wa vipepeo wa kijiji hicho, anayesema kuwa na ushindani mkubwa katika ufugaji vipepeo kijijini, kila mmoja anajitahidi kumshinda mweziwe katika uzalishaji vipepeo na hatima ya yote ni kunufaika na fedha za kutosha.
Anasema, baada ya kuwinda vipepeo, huwa wanawahifadhi katika sehemu maalum ambayo hawawezi kushambuliwa na wadudu wengine, ili waweze kutaga na hawawezi kukimbia.
Khamis anasema kuwa, wakiwa katika hifadhi nzuri, huwa wanawapa chakula kila siku ili wawe na afya na lishe wanazopenda ni matunda kama machungwa na malimau.
Anasema mwanzoni waliidharau biashara hiyo, lakini walipoianza waligundua ina tija na faida kubwa, kinyume na walivyofikiria awali.
“Hatuna tatizo na soko maana tunauza hapa hapa kijijini petu na huwa wanahitajika kwa wingi, maana inafika kipindi vipepeo wanatakiwa,” anasema mfugaji huyo.
Anasema ili vipepeo wapatikane kwa wingi ni lazima kuwepo miti mingi, hivyo anawashauri wanakijiji wenziwe kuacha kukata miti ovyo, pia kuwa na utamaduni wa kupanda miti.
Khamis anatamka:”Kweli miti au mimea ina faida nyingi, maana bila ya miti vipepeo haviwezi kupatikana kwa wingi. maana sasa vipepeo vimekuwa ni wakombozi wetu.”
MNUNUZI WA VIPEPEO
Meneja Msaidizi wa mradi wa Zanzibar Butterfly Centre, Alfred George, anasema kuwa idadi kubwa ya wanakijiji hicho, hasa wanawake wamepata ajira ambayo imekuwa ikiwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Anasema licha ya mradi huo kuwapatia ajira wananchi, pia umewaongezea wanakijiji uelewa wa kuhifadhi mazingira.
George anasema kuwa, kabla ya mradi wa vipepeo, wanakijiji walijishughulisha na uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji miti ya kuni na kutengeneza mkaa.
Anasema mradi wa ufugaji wa vipepeo ulianza mwaka 2007, kwa kutolewa elimu ya bure ya ufugaji vipepeo kwa wana kijiji cha Pete wanaofanya biashara hiyo wako zaidi ya 50.
“Wafugaji hao hutafuta vipepeo misituni na kuwafuga kama kuku wa mayai kisha baada ya kutaga mayai vifaranga vya vipepeo huja hapa kuuza kama ni kituo kikuu cha ununuaji wa vipepeo,” anasema George.
Anaongeza kwa kutamka:“Sisi hapa ni kama ‘centre’(kituo), Kazi yetu ni kununua vipepeo kutoka kwa wafugaji na biashara hii ina soko kubwa, maana kifaranga cha kipepeo tunanunua kutoka kwa wafugaji Sh. 1000 na sisi tunauza nje ya nchi ikiwemo Ufaransa, Uholanzi na Uingereza.”
George anasema licha ya kununua vipepeo, pia imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaofika katika eneo hilo kuangalia shughuli ya ufugaji, ambako kuna shamba maalum la ufugaji vipepeo.
Anasema katika msimu wa utalii, wengi wao wanafika kijijini Pete kuangalia shughuli hiyo ya ufugaji na kuna tozo wanalolipia.
Kwa mujibu wa George, vipepeo wanahitajikka sana katika nchi za Ulaya wakiwatumia kwa shughuli mbalimbali kama vile harusi.
Anaeleza changamoto za mradi huo, kuwa katika kipindi cha ukame wenye jua kali au mvua zinapokuwa nyingi, uzalishaji vipepeo unakuwa mgumu, kwani wanakuwa adimu.
“Vipepeo vinategemea sana maua ya miti mbalimbali, hivyo ikiwa kuna jua kali, maua hamna na msimu wa vipepeo vingi baada ya kumalizika kwa mvua,” anasema George.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira wa Msitu wa Jozani(JECA), Awesu Shaaban Ramadhani, anasema licha ya kuongeza uelewa wa hifadhi ya viumbe hai na mazingira, pia mradi wa ufugaji vipepeo umesaidia suala la kipato kwa wanakijiji waliojiunga na mradi huo.
Anasema kabla ya kuanza kwa mradi huo, Msitu wa Hifadhi ya Jozani, ulikuwa hatarini kutoweka kutokana na wana kijiji wa Pete na maeneo jirani kuushambulia kwa kukata miti.
"Msitu wa Jozani ambao ndio msitu mkubwa kwa Zanzibar na kivutio kwa watalii, ulikuwa karibu kuangamia. Lakini sasa ni furaha tele kwamba wanakijiji wengi wao wamejiunga mradi wa ufugaji wa vipepeo kwa lengo la kuzalisha kipato na kuhifadhi mazingira,” anasema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment