MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad ameshauri upangaji wa bajeti upangwe kutokana na mapato yaliyopo.
Profesa Assad alitoa ushauri huo juzi alipotoa mada katika semina ya wabunge wa Kamati nne za Bunge iliyofanyika Dar es Salaam.
Alisema changamoto iliyopo sasa ni kwamba bajeti hupangwa kwa kuangalia matumizi au matakwa yaliyopo kabla ya kuangalia mapato.
“Kwa kuwa hatuangalii kwanza tulichonacho kabla ya kupanga bajeti matokeo yake bajeti inakuwa haitekelezeki,”alisema.
Alisema changamoto nyingine za bajeti ni pamoja na kupandisha bei wakati wa ununuzi wa bidhaa za umma, kushuka thamani ya shilingi na ubadilishaji wa matumzi ya fedha tofauti na bajeti ilivyoelekeza.
Mbali na kutoa elimu kwa wabunge ya jinsi ya kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, CAG pia aliwataka wabunge kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua kama kuna jambo lolote limetokea.
“Kama kuna kitu kimetokea tujenge utaratibu wa kuhoji kwanza kitu gani kimetokea, kwa nini kimetokea, athari zake na hatua zipi za kuchukua,”alisema.
Alisema kufanya hivyo kutaepusha migogoro kutokea na kwamba kwa uzoefu hatua hizo huwa hazifuatwi.
Akichangia katika semina hiyo, Mbunge wa Babati Vijijini,Jitu Son alisema kama semina hizo zingekuwa zinatolewa tangu zamani ni dhahiri wabunge wangekuwa wanafanya kazi zao kwa umahiri.
“Vilevile semina kama hizi zingekuwa zinafanyika kuanzia ngazi za halmashauri ili na wao wajifunze jinsi ya kuandaa bajeti hali itakayofanya mfumo mzima wa kuandaa bajeti kuanzia ngazi ya chini kuwa mzuri,”alisema.
Mbunge wa Viti Maalum, Felista Bura alitaka apatiwe ufafanuzi iwapo Ofisa Masuuli atabainika kuokoa fedha lakini kwa kutofuata utaratibu hatua zipi zichukuliwe.
Semina hiyo ilihusisha Kamati ya Bajeti, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) , Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC).
No comments :
Post a Comment