Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 16, 2016

CUF yamtega Lipumba

Ibrahim_Lipumba
NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM, MTANZANIA.
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kipo katika maandalizi ya kuanza mchakato wa kuziba nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mbali na maandalizi hayo, pia kimesisitiza kuwa Lipumba ana haki ya kugombea kama atakuwa tayari licha ya Agosti, mwaka jana kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho ikiwemo ya uenyekiti kwa kile alichokidai kuwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilikiuka  makubaliano yao kwa kumteua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya, alisema uchaguzi wa kuziba pengo la Lipumba unatarajiwa kufanyika kati ya Agosti na Septemba, mwaka huu hivyo kila mwanachama aliye hai anastahili kuchukua fomu na kugombea nafasi hiyo.
“Uchaguzi utafanyika kwa sababu hatuwezi kukaa bila kupata kiongozi, Profesa Lipumba pia bado ni mwanachama hai hadi 2020 hivyo hata yeye kama atakuwa amesharudisha moyo wake ndani ya chama na kutaka kurudi katika nafasi yake anaruhusiwa. Lakini hakuna mtu anayefanya njama wala mikakati ya kuhakikisha Profesa Lipumba anashika nafasi hiyo na hakuna anayemlazimisha kugombea,” alisema Sakaya.
Pia alisema Lipumba ni nembo ya CUF Bara hivyo endapo atafanya uamuzi wa kurudi katika nafasi hiyo na kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo hawawezi kumzuia.
Sakaya alisema CUF itafanya uchaguzi wa kidemokrasia na kama ikitokea Lipumba akagombea na wanachama wakamchagua kushika tena nafasi hiyo atakuwa kiongozi halali.
Alisema uchaguzi huo utafanyika ili kukidhi matakwa ya kikatiba kwa kuwa katiba ya CUF hairuhusu nafasi ya kiongozi kukaa wazi ama kukaimiwa kwa zaidi ya miezi sita.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa za malalamiko yaliyoelekezwa kwa viongozi kutotoa nafasi ya kujadili barua ya kujiuzulu kwa Lipumba katika mkutano wao wa Baraza Kuu la CUF, alisema hakuna malalamiko.
Alisema barua ya Lipumba ilipokelewa mwaka jana na kuelekezwa kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CUF na kutokana na kuwapo kwa harakati za uchaguzi mkuu na ufinyu wa bajeti walishindwa kuitisha mkutano.
“Barua ilipokelewa mwaka jana na  ilielekezwa kamati kuu, lakini kutokana na muda na tulikuwa hatuna fedha kuitisha wajumbe kipindi kile cha uchaguzi hatukupata muda wa kujadili,” alisema.
Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua, alisema kutokana na hali hiyo, Aprili 2, mwaka huu wajumbe wa Baraza Kuu walikutana na katika kikao hicho pia walisomewa barua hiyo lakini hakuna mtu aliyechangia.
“Katika kikao cha juzi, barua ya Profesa Lipumba ilisomwa na hakuna mjumbe yeyote aliyechangia kama kuna mtu anasema hawajapewa nafasi, sio kosa la viongozi ni kosa la wanachama walioshindwa kutumia nafasi iliyokuwepo ya kuhoji ama kuuliza maswali,” alisema Sakaya.
Pia alisema hana taarifa ya kuwapo kwa makongamano ya nchi nzima yaliyoandaliwa na baadhi ya wanachama wa CUF ili kushinikiza kujadiliwa suala hilo.
Kitendo cha Lipumba kujiuzulu nafasi hiyo kulizua sintofahamu hapa nchini wakati Taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu na tangu wakati huo mara kadhaa alikuwa akijitokeza na kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali ya kitaifa yanayojitokeza na alisisitiza kuwa maoni yake alikuwa akiyatoa kama mwanachama wa kawaida wa CUF.
Mbali na Lipumba, kiongozi mwingine wa Ukawa aliyejiuzulu nafasi yake kabla ya Uchaguzi Mkuu haujafanyika ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa.

No comments :

Post a Comment