airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 16, 2016

Magufuli, Kikwete wapashana

 
RAIS Dk. John Magufuli na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete, wameanza kutofautiana hadharani.

Kwa kasi, kutokupepesa macho na kutokumung’unya maneno kwa Rais Dk. Magufuli, wengi walitarajia kwamba siku moja, isiyo na jina, angemwambia Mwenyekiti wake kwamba hapana.

Raia Mwema limeambiwa kwamba siku hiyo ilikwishakutimia, bila shaka ikiwa ni mapema mno, pale kwa mara ya kwanza, hali hiyo ilipojiri kwenye kikao cha Kamati Kuu ya chama chao kilichofanyika kabla ya Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, mwezi uliopita.

Katika kikao hicho cha Kamati Kuu kilichofanyika Dar es Salaam, Kikwete alieleza kutofurahishwa kwake na baadhi ya viongozi wa serikali waliokuwa wakiunga mkono kufanyika kwa uchaguzi huo wa Meya wa Dar es Salaam uliomwibua Isaya Mwita, kutoka katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kwamba Kikwete alikuwa amepewa taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM na wa jumuiya za chama hicho kuwa baadhi ya viongozi wa serikali hawakisaidii chama jijini Dar es Salaam.

“ Hivi watu wa serikali au mawaziri ni watu wa namna gani hata wasitii maagizo ya chama chao? Hivi bila CCM nani angekuwa waziri au kiongozi wa serikali. Hii ni tabia ya ajabu sana,” chanzo chetu kilimnukuu Kikwete akisema maneno karibu na hayo.

Chanzo hicho ambacho ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu waliohudhuria mkutano huo, aliliambia gazeti hili kuwa Kikwete alionyesha kukerwa na jambo hilo na alizungumza kwa ukali.

Gazeti hili limeambiwa kuwa mmoja wa wanasiasa waliotoa lawama nyingi kwa mawaziri wa Magufuli na serikali kwa ujumla ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sofia Simba.

Sofia mwenyewe anadaiwa kupokea taarifa nyingi kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wana CCM waliokuwa mstari wa mbele kutaka uchaguzi huo wa Meya usifanyike.

Inaelezwa ya kuwa wakati wajumbe wakiwa kimya baada ya kauli hiyo ya Mwenyekiti Kikwete, Dk. Magufuli aliomba nafasi ya kuzungumza na Mwenyekiti alimruhusu.

Katika maelezo yake, Magufuli ambaye anahudhuria vikao hivyo kwa sababu ya wadhifa wake wa urais, aliwatetea mawaziri wake kwa kufuata sheria na si kuyumbishwa na wanasiasa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia maelezo yako kwa makini. Naomba kusema kwamba haya matatizo yaliyopo sasa yalitengenezwa na sisi wenyewe na wengine waliosababisha haya matatizo wako humuhumu.

“Wakati wa Uchaguzi Mkuu, kuna wenzetu walitusaliti wakiwa ndani ya chama. Sasa baada ya chama kushindwa kwenye uchaguzi kwa sababu ya usaliti wao, leo wanataka mawaziri wavunje sheria kulinda usaliti wao.

“Hili kwa kweli Mwenyekiti hatuwezi kulitetea. Kama usaliti ulisababisha Ukawa wakashinda Dar es Salaam, basi tuache nasisi tuonje machungu ya usaliti. Kwa kufanya hivi tutajifunza kuwa usaliti si mzuri.

“Kama mawaziri au watumishi wa serikali watakuwa wanafuata sheria kwenye shughuli zao, mimi nitawatetea. Lakini hatuwezi kuwasema kwa kufuata sheria na kuwaacha wasaliti ambao ndio wametufikisha hapa,” chanzo chetu kilimnukuu Magufuli.

Raia Mwema limeambiwa kuwa baada ya maneno hayo ya Magufuli, Kikwete aliahirisha mkutano huo ili wajumbe wakapate mapumziko ya chai.

Kwa kawaida, kwenye vikao vigumu vya chama, Kikwete amekuwa na tabia ya kuahirisha vikao kwa muda wakati anapoona joto la mkutano limepanda na ni tabia hii ndiyo iliyofanya Uenyekiti wake uvuke baadhi ya vihunzi vigumu.

Wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM mwaka jana, Kikwete alikuwa akitumia mbinu hiyo ya kuahirisha mkutano kwa muda mfupi na wakati mwingine kuchelewesha kuanza mikutano; akisubiri “joto la wajumbe lishuke”.


Sofia Simba na Madabida
Katika duru za CCM, baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaamini kuwa Mwenyekiti huyu wa UWT bado yuko karibu na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa,Edward Lowassa. Kwamba wakati wa uchaguzi wa mwaka jana, hakupambana sana kuhakikisha Dk. Magufuli anashinda.

Mwaka 2009, wakati Lowassa akiwa anasakamwa na kashfa ya Richmond, Sofia Simba alijitokeza hadharani na kutamka kwamba katika CCM hakuna “mwanamume kama Lowassa”.

Julai 11 mwaka jana, majira ya saa saba usiku, yeye, Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa, wote wakiwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, walitamka kwa waandishi wa habari kutokukubaliana na maamuzi ya CC kukata jina la Lowassa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Nchimbi alisema kwamba wao watatu hawakukubaliana na maamuzi ya hayo ya CC iliyoketi chini ya Kikwete na “kumkata mgombea maarufu kwa manufaa ya mgombea asiye maarufu”.

“Katika kikao cha leo Kamati Kuu haikupokea majina yote yaliyojadiliwa na Kamati ya Maadili, suala ambalo ni kinyume na kanuni. Pili, Katiba ya CCM inataka mtu anayekubalika ndiye apewe nafasi ya kwanza, lakini kikao cha leo kimeonyesha kuminya wanaokubalika kwa manufaa ya wachache wasiokubalika,” alisema Nchimbi wakati huo kwa niaba ya wenzake hao wawili.

Kwa sababu hiyo, Nchimbi alitamka kwamba yeye na wenzake hao wawili wamewataarifu wenzao kwamba wamejitenga na uamuzi wa kikao hicho na kutangaza kutokuuunga mkono.

Madabida naye amekuwa akifahamika kama mfuasi wa Lowassa kwa muda mrefu; akiwa mmoja wa viongozi waliohudhuria mkutano wa waziri mkuu wa zamani huyo wa kutangaza nia uliofanyika mjini Arusha.

Lakini, Madabida alionyesha sura yake halisi Juni 26, 2015 wakati alipotangaza kwamba Lowassa ndiye chaguo la Mungu wakati alipokuwa akizungumza kwenye mojawapo ya sherehe za kidini ambazo mgombea huyo wa Ukawa alihudhuria jijini Dar es Salaam.

Mjumbe huyo wa CC alilieleza Raia Mwema kwamba wapo wana CCM wanaoamini kwamba Madabida na Sofia ni mojawapo ya sababu za kushindwa kwa CCM jijini Dar es Salaam kwa sababu hawakupambana kama ambavyo wangepambana endapo Lowassa ndiye angekuwa mgombea.

Uchaguzi Mkuu 2015

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, CCM kilifanya vibaya Dar es Salaam kuliko katika wakati mwingine wowote katika historia yake; kiasi kwamba sasa jiji hilo muhimu zaidi nchini, linaongozwa na Upinzani.

Katika Wilaya ya Ilala, CCM ilipata madiwani 22 kulinganisha na 30 wa vyama vilivyo kwenye Ukawa huku kikipata madiwani 15 katika Wilaya ya Kinondoni kulinganisha na 36 wa Ukawa. Ni Temeke pekee ambako CCM ilipata madiwani 29 kulinganisha na 17 wa Ukawa.

Kutokana na hali hiyo hiyo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, anatoka katika chama cha Chadema, pamoja na mameya wa Manispaa za Kinondoni na Ilala. Ni Temeke pekee ambako CCM ina Meya.

Magufuli na wasaliti
Wakati wa kampeni za kusaka urais, Dk. Magufuli alikuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu wasaliti walio ndani ya CCM; akisema kwamba mchana wanakuwa nao lakini usiku wanafanya kazi za Upinzani.

Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais, Dk. Magufuli akizungumza katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam alitangaza hadharani kwamba yeye hatavumilia wasaliti kama alivyokuwa Kikwete.
 


No comments :

Post a Comment