Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad: Picha kutoka maktaba ya mzalendo.net
Na Pendo Omary – Mwanahalisi online
Jumamosi, Oktoba 8, 2016
MAALIM Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amewataka Wazanzibari kusimama imara katika kulinda visiwa vyao, anaandika Pendo Omary.
Amesema, mikakati inayofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuhakikisha maoni katika katiba pendekezwa yanapita jambo ambalo litasababisha Zanzibar kupokwa mamlaka na kuzima ndoto za Wazanzibari.
Ameonesha hofu yake kutokana na Serikali ya CCM kutokuwa na dhamira ya kweli ya kuifanya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili jambo ambalo Wazanzibari wamekuwa wakilipigania kwa muda mrefu.Akizungumza baada ya Sala ya Ijumaa, jana kwenye Msikiti wa Mbuyuni, mjini Unguja, Maalim Seif amesema kwamba, Katiba Inayopendekezwa inakwenda kumaliza kabisa ndoto ya Zanzibar ya kuwa na mamlaka kamili na kwamba, wananchi wanapaswa kuungana na kupinga kwa nguvu zote.
Ametoleo mfano suala la ardhi ambalo ndani ya Katiba Pendekezwa limewekwa kuwa la Jamhuri ya Muungano na kwamba, licha ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kupitisha sheria ya utafiti na uchimbaji madini na gesi, haitawezekana kwa kuwa ardhi ni suala la Muungano.
Maalim Seif amesema, kwa kuwa Serikali ya CCM inajua kuwa itakumbana na upinzani mkali wakati wa kura ya maoni, hivyo imeanza kusomba watu kutoka Bara kwenda visiwani ili kuongeza nguvu ya kuungwa mkono.
“Kwa kuwa Katiba hii inakuja kumaliza kabisa mamlaka ya Zanzibar, umeanza kufanyika mpango ili wapitishe kwa udanganyifu.”
“Kuna watu wanatoka bara na kuletwa Zanzibar ili wapate sababu ya kupitisha na ionekane Wanzibari wameridhia,” amesema Maalim Seif.
Pamoja na kuwepo kwa mikakati hiyo kiongozi huyo wa CUF amesema kuwa, mbinu hizo hazitafanikiwa ila kwa sharti la Wanzanibari kusimama imara katika kuitetea Zanzibar.
Ameeleza kuwa, msingi wa mikakati inayofanywa na serikali kwa sasa ni kutokana na maoni ya wananchi kuchezewa katika Bunge la Katiba.
Amesema, Jaji Mstaafu, Joseph Warioba aliwasilisha maoni ya wananchi kama alivyokusanya kutoka kwa wananchi ambao walipendekeza Serikali Tatu lakini Serikali ya CCM wamefanya hila za kurejesha Serikali Mbili kwenye Katiba Pendekezwa.
Kwa mujibu wa sheria Katiba Pendekezwa inahitaji kupigiwa kura ama kuungwa mkono kwa zaidi ya asilimia 50 ya Wazanzibari na hivyo hivyo kwa Tanganyika, ili kupata uhalali wa kuwa Katiba.
No comments :
Post a Comment