Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 11, 2016

MADIWANI ‘WAMTOSA’ LIPUMBA!

Uamuzi uliotolewa na Ukawa wa kutoshirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba hautaathiri umoja huo wa vyama vya upinzani katika uchaguzi wa umeya wa manispaa za Dar es Salaam, baada ya madiwani wa CUF kumsusa.

Profesa Lipumba anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwamba ndiye mwenyekiti halali wa CUF, hata pale mkutano mkuu uliporidhia kujiuzulu kwake na kufuatiwa na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi kumfukuza uanachama.
Mgogoro huo wa CUF uliokigawa chama hicho makundi mawili, uliwasukuma viongozi wa Ukawa wakiongozwa na Freeman Mbowe kutoa tamko la kumtenga Profesa Lipumba kwa madai kwamba analazimisha uenyekiti wa chama.

Licha ya Profesa Lipumba kudai anaungwa mkono na wanachama wengi wa CUF, madiwani wote wa chama hicho katika manispaa za Dar es Salaam wametangaza kuiunga mkono Ukawa kwenye uchaguzi wa meya katika manispaa zote.

Uchaguzi wa meya unafanyika baada ya kuanzishwa kwa wilaya mpya za Ubungo na Kigamboni. Ubungo imemegwa kutoka Wilaya ya Kinondoni na Kigamboni imemegwa kutoka Wilaya ya Temeke.

Tayari manispaa za Ubungo na Kinondoni zimegawana kata na kila moja itakuwa na meya na uchaguzi unatarajiwa kufanyika wiki ijayo. Manispaa za Temeke na Kigamboni bado hazijafikia mchakato wa kugawana kata na madiwani.

Madiwani kadhaa wa CUF waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa nyakati tofauti walisema hawamuungi mkono Profesa Lipumba anayepinga Ukawa.

Maulid Mtulia ambaye ni Mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF, ameonyesha wasiwasi kwamba kuna njama ya kumpunguza Salima Mwasa ambaye ni Mbunge Viti Maalumu wa CUF katika orodha ya wapigakura wa halmashauri hiyo.

Amesema endapo Mwasa ataondolewa halmashauri ya Kinondoni, idadi ya kura za Ukawa itabaki 17 dhidi ya CCM 17.

Tayari Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilishagawanya rasmi madiwani wake kwenda Manispaa mpya ya Ubungo na wengine kubakia Kinondoni kulingana na jiografia ilivyo. Kinondoni itabaki na kata 20 wakati Ubungo itakuwa na kata 14.

Kwa upande wa CCM, katika Manispaa ya Kinondoni ina madiwani tisa, viti maalumu vitatu na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais, wenye sifa ya kupiga kura, ambao ni Profesa Makame Mbarawa, Angela Kairuki, Dk Tulia Ackson, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi Augustine Mahiga. Hatua hii inafanya idadi ya kura za CCM kuwa 17 dhidi ya 18 za Ukawa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM, Kinondoni, Salum Madenge alikataa kutaja idadi ya kura halisi za CCM katika halmashauri hiyo ya Ubungo huku akisema chama hicho kitashinda kwa hesabu na jinsi kilivyojiandaa. Madenge alisema suala la uchaguzi ni hesabu na CCM imejipanga kupata ushindi katika uchaguzi huo.

“Kama wao wana kura hizo 14, basi sisi ni zaidi yao, subiri utaziona siku ya kupiga kura. Unajua uchaguzi ni hesabu kwa hivyo tumeshajipanga wala usijali…, ” alisema Madenge huku akitoa kicheko.

Halmashauri ya Ubungo
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole alinukuliwa Julai mwaka huu akizitambua Kata 14 za halmashauri hiyo za Makurumla, Mburahati, Manzese, Mabibo, Sinza, Ubungo, Makuburi, Kimara, Mbezi, Msigani, Saranga, Goba, Kibamba na Kwembe.

Hesabu ya kata hizo inaonyesha kuwa CUF ina kura (2), Chadema (10) na CCM (2). Kwa tofauti ya idadi hiyo ya madiwani, inaifanya CCM kukosa nafasi yoyote ya ushindi hata bila kutegemea mgogoro wa Lipumba ndani ya CUF.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, John Kayombo alisema uchaguzi huo utafanyika siku yoyote kuanzia wiki hii.

Kuhusu mchanganuo wa idadi ya kura za vyama, Kayombo alitaka kusubiri waraka kutoka mamlaka husika.

“Kata ziko 14 na CCM ina Kata(2), CUF (2) lakini naomba tusubiri waraka utakaokuwa na taarifa zote za uchaguzi, wala usijali tutaweka mbele ya vyombo vya habari, nadhani itakuwa wiki hii,” alisema Kayombo.

Temeke na Kigamboni
Kwa Halmashauri mbili za Temeke na Kigamboni, CCM itakuwa na nafasi ya kuchukua ushindi kwa hesabu ya kura zozote zitakazogawanywa katika pande hizo mbili kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ikilinganishwa na Ukawa.

No comments :

Post a Comment