Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhandisi ya Naif { Naif Engineering Company } Bibi Khadija Naif Alyafei hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Bibi Khadija Naif Alyafei amejitolea kuwa Balozi wa kuitangaza Tanzania kwenye fursa za Kibiashara na masuala ya Utalii katika Mataifa ya Ghuba akilenga zaidi Nchi ya Saudi Arabia.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, Ompr
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziar Balozi Seif Ali Iddi alisema Kamisheni ya Utalii Zanzibar italazimika kutafsiri vitabu vya Utalii kwa lugha mbali mbali za Kimataifa ili kuvitangaza vizuri Kiutalii Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuimarisha miundombinu katika Sekta ya Utalii.
Alisema wakati umefika kwa Kamisheni hiyo kufungua njia zaidi za kuutangaza Utalii wa Zanzibar katika kuhamasisha Watalii kutoka Mataifa mbali mbali Duniani zikiwemo hasa Nchi za Ghuba badala ya nguvu zao kuzielekeza upande mmoja tu wa Mataifa ya Ulaya na Amerika.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhandisi ya Naif Bibi Khadija Naif Alyafei aliyejitolea kuwa Balozi wa kuitangaza Tanzania kwenye fursa za Biashara na masuala ya Utalii katika Mataifa ya Ghuba akilenga zaidi Nchi ya Saudi Arabia, mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Balozi Seif alisema Mataifa mengi ya Ghuba yanaonyesha kwamba Wananchi wake wanapendelea Utamaduni wa Tanzania lakini wanashindwa kuuelewa kwa kina kutokana na vitabu vingi vya Kamisheni ya Utalii Zanzibar kuandikwa Lugha chache kama za Kingereza na Kifaransa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwa vile Jamii ya Dunia imetawaliwa na Lugha tofauti, Kamisheni hiyo ijikite kutekeleza jukumu hilo muhimu na Wizara inayohusika na Utalii ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo itawajibika kugharamia kazi hiyo.
Amempongeza Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Uhandisi ya Naif Bibi Khadija Naif Alyafei kwa juhudi kubwa anazochukuwa katika kujitolea kuwa Balozi wa kuitangaza Tanzania na hasa Visiwa vya Zanzibar kwenye fursa za Kibiashara na masuala ya Utalii ndani ya Mataifa ya Ghuba.
Balozi Seif alimuomba Bibi Khadija Naif kutumia maarifa zake ya Kitaalamu kuwahamasisha Wawekezaji wa Mataifa hayo washawishike kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi na Biashara Nchini Tanzania.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuhamasisha Wawekezaji wa ndani na nje kuitumia fursa hiyo kwa kigezo kikubwa kilichopo cha mazingira mazuri yaliyozunguukwa na rasilmali sambamba na hali ya amani na utulivu iliyoshamiri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Zanzibar imejipanga kufanya Mapinduzi ya Viwanda kwa kuwatumia wajasiri amali wake wadogo wadogo ili ikabiliane na tatizo la usindikaji wa biadhaa wanazozalisha wajasiri amali hao pamoja na Wakulima.
Mapema Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhandisi ya Naif Bibi Khadija Naif Alyafei alisema Taasisi yake imejikita zaidi katika kuwahamasisha wajasiri amali wadogo wadogo ili wapate nafasi ya kuzitangaza biadhaa wanazozalisha katika fursa za Kibiashara zilizopo katika Mataifa ya Ghuba.
Bibi Naif alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uwepo wake Visiwani Zanzibar umemuwezesha kukutana na Wajasiri amali mbali mbali Mijini na Vijijini Unguja na Pemba na amehamasika kulazimika kuchukuwa baadhi ya sampuli za bidhaa wanazozizalisha na akazitangaze kwenye masoko ya Nchi hizo.
“Nimepata vitu vingi kutoka kwa wajasiri amali pamoja na Vitabu vya Utalii nilivyopewa na Kamisheni ya Utalii Zanzibar nitakavyovitumia vyema katika kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wakati nitakaporejea Nchini Saudi Arabia kati kati ya Mwezi ujao wa Disemba “. Alisisitiza Bibi Naif.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Uhandisi ya Naif {Naif Engineering Company} aliishukuru Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa msaada mkubwa iliyompa wa Vitabu ambao utamuwezesha kazi yake ya kujitolea kuwa rahisi zaidi kwenye utekelezaji wake.
No comments :
Post a Comment