Rais John Magufuli amewaagiza watendaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusitisha mara moja kuwaondoa wamachinga katika miji mpaka hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa kwa kuwashirikisha na kwamba asiyekubaliana na maagizo yake hayo aachie ngazi.
Uamuzi huo ulitokana na hatua iliyochukuliwa na Serikali jijini Mwanza kuwaondoa mitaani wamachinga na kuwahamishia nje ya maji wanakosema hakuna wateja.
Agizo hilo limetolewa kwa uzito wa aina yake kwani Rais Magufuli jana alimwita Makamu wake, Samia Suluhu Hassan pamoja na watendaji wa Tamisemi na kutoa maagizo hayo baada ya kuwapo kwa malalamiko ya wamachinga kuharibiwa kwa mali zao na kupelekwa maeneo ya pembezoni.
Mbali na Samia, wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo na Katibu Mkuu, Mhandisi Mussa Iyombe.
“Unajua Mheshimiwa Makamu wa Rais, nimeona niwaite wewe na wenzetu wa Tamisemi kwa ishu moja. Kumekuwa na maagizo mengi. Na haya maagizo mengi yanakuwa na mwelekeo wa kuchonganisha Serikali na wananchi,” alisema Rais Magufuli. “Kumeibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwafukuza wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, hili jambo siyo sawa hata kidogo.
“Unajua Mheshimiwa Makamu wa Rais, nimeona niwaite wewe na wenzetu wa Tamisemi kwa ishu moja. Kumekuwa na maagizo mengi. Na haya maagizo mengi yanakuwa na mwelekeo wa kuchonganisha Serikali na wananchi,” alisema Rais Magufuli. “Kumeibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwafukuza wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, hili jambo siyo sawa hata kidogo.
“Sipendi wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara, lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji. Tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo, maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi,” alisema.
Rais alisema huo si mwelekeo wao na wala wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo yeye na Makamu wa Rais walipita kuinadi.
Alielekeza kuwa wamachinga walioondolewa katika maeneo yao Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa.
“Narudia na hii ni mara ya mwisho, kuwaambieni hata wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundombinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri na waliwashirikisha viongozi wa wamachinga.Lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Wachimbaji wadogo wafaidika
Mbali ya machinga, pia Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo, mkoani Shinyanga na badala yake waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake iondolewe.
“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mheshimiwa Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi ovyoovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu.
“Na hizi ndizo ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? Haiwezekani na wala haingii akilini,” alisema.
Awapongeza wamachinga
“(Kuhusu) Ishu iliyojitokeza Mwanza, niwapongeze wamachinga, hawakufanya fujo. Walitulia. Nilizungumza kwenye mkutano wa Biafra hadharani kuwa hawa wamachinga msiwatoe mjini, kama mnatengeneza mazingira yawe mazuri kwa ajili ya kufanya biashara zao ili wasizagae,” alisema.
“Na nilitoa mfano mnaweza hata kufunga barabara katikati ya mjini mkasema hili ndilo litakuwa eneo la machinga kufanya biashara. Lakini utaratibu siku hizi umekuwa ondokeni mjini na huko wanakopelekwa hawajatengenezewa mazingira ya biashara.
“Ndiyo maana nimewaita naibu waziri na katibu mkuu Tamisemi wawaeleze wote wanaowaongoza wasiwabughudhi wamachinga na wala wao hawakupenda kuwa wamachinga ni kama ambavyo wao (mawaziri) hawakupenda kwa sababu hawakuniuliza nilipokuwa nawateua kwenye nafasi zao.
Alisema viongozi waongee na wamachinga kabla ya kuwahamisha ili wajue kama eneo wanalohamia linawafaa.
“Kama kuna mkuu wa mkoa, DC au mkurugenzi anayeona hakubaliani na maagizo yangu aache kazi. Sisi ndiyo tunajua shida za wananchi si wao. Mkawaeleze wawaache wamachinga wafanye biashara, wawatengenezee mazingira mazuri,” alisema.
Lakini akawataka wamachinga wasichukulie amri hiyo kufanya biashara na kujenga mabanda kila mahali kwa kuwa yanachafuamandhari.
“Nilitegemea uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa vile nilizungumza hadharani, wangekuja kuniambia tuna utaratibu huu lakini nashangaa watu wanaswagwa tu wanatumia polisi, hii haiwezi kuwa sawa,” alisema.
“Natolea mfano Mwanza kama wanaona mjini hapafai wawape Furahisha au Nyamagana kwani uwanja huo umetengenezwa na Serikali. Nimewaita, nafikiri maamuzi mengine natakiwa kuhusishwa.”
Mwekezaji amekopea hekta 35,000
Rais pia alidokeza kuwa kuna mwekezaji amepewa zaidi ya hekta 35,000 ambazo ametumia kukopa nchini Uholanzi na hilo eneo halijaendelezwa hadi sasa.
“Na mtu huyohuyo alikuwa anatafuta eneo jingine la hekta 65,000. Ndiyo maana Watanzania wanakosa hata sehemu za kulima na kuchungia mifugo yao halafu tunabaki kutoa amri tu,” alisema.
Simbachawene atoa maagizo
Mara baada ya kikao hicho, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alikutana na waandishi wa habari na kufafanua maelekezo ya Rais Magufuli kuwa hao wanyonge na maskini wanaohangaika kwa shida ya ajira lazima kazi yao itambulike na iheshimiwe.
Simbachawene alisema kwa kuanzia, yatengwe maeneo ya katikati ya miji yenye wateja wa bidhaa zinazouzwa kwa kuangalia uwezekano wa kufunga japo mtaa mmoja ili utumike kwa kazi za kimachinga.
Alisema utaratibu huo hautamaanisha watu wapange bidhaa barabarani, bali mtaa mmoja au miwili itakayobainishwa kwa mpango shirikishi wa wajasiriamali na kuzuia kujenga vibanda ambavyo vitafanya maeneo hayo yaonekana machafu.
“Mamlaka zinatakiwa ziandae maeneo rafiki yenye mahitaji muhimu ili yaweze kufikika kirahisi na kuruhusu biashara kufanyika bila shida yoyote kabla ya kuwahamisha wafanyabiashara hao kwa njia shirikishi zaidi,” alisema Simbachawene.
Simbachawene pia alisema wataziangalia na kuzitolea majibu tozo wanazotozwa na kuangalia namna ya kuzifuta kabisa.
Agizo latekelezwa
Baada ya kauli ya Rais kusambaa kwenye vyombo vya habari, viongozi wa Serikali mkoa, walianza kutekeleza agizo hilo kwa kuwaruhusu wamachinga kurejea maeneo ya katikati ya jiji walikoondolewa mwishoni mwa wiki.
“Kiutaratibu na kwa mujibu wa sheria, amri ya Rais haijadiliwi, bali inatekelezwa mara moja. Tayari tumeanza utekelezaji wa suala la wamachinga,” alisema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Mongella alisema viongozi wa halmashauri za Manispaa za Ilemela na Nyamagana wataanzisha majadiliano ya pamoja kati yao na wamachinga pamoja na wadau wengine kuhusu maeneo, miundombinu na njia bora ya kila upande kutekeleza agizo la Rais.
Kauli ya Mongella inafanana na ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Merry Tesha aliyesimamia kuwaondoa wamachinga usiku wa kuamkia Desemba 3, aliyejibu kwa kifupi kuwa tayari ametekeleza maagizo hayo.
“Tunaanza utekelezaji wa amri ya Rais mara moja,” alijibu kwa ufupi Tesha.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Leonard Masale alisema wilaya yake tayari inatekeleza agizo la Rais Magufuli kwa kuwaandalia maeneo ya kuhamia wafanyabiashara hao.
“Sisi Ilemela hatujamwondoa hata mmachinnga mmoja, bali tunaendelea na kazi ya kuwaandalia maeneo na mazingira bora ya biashara,” alisema Masale.
Chereko ya wamachinga
Agizo la Rais Magufuli lilipokewa kwa furaha na wamachinga ambao walirejea katikati ya jiji dakika chache baada ya taarifa hiyo kutangazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wamachinga waliokutwa eneo la Makoroboi wakipanga bidhaa zao chini baada ya meza na vibanda vyao kubomolewa wakati wa operesheni, walikuwa wakiimba nyimbo za kumshangilia na kumtukuza Rais Magufuli huku wakisema wako tayari kumchagua aongoze hata miaka 100 ijayo.
“Tumerudi… tumerudi… Magufuli, hata miaka 100,” huo ulikuwa wimbo wa wafanyabiashara hao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jimmy Ezekiel aliutupia lawama uongozi wa Serikali Mwanza kwa kutumia zaidi ya Sh150 milioni kutekeleza operesheni hiyo bila kuwashirikisha.
Wakati wamachinga wakifurahia agizo hilo, Wafanyabiashara wanaomiliki maduka katikati ya jiji walilalamikia kuwa halijazingatia ukweli kwa kuwa baadhi ya wamachinga wanatumika fursa kukwepa kodi.
“Hawa wamachinga hawalipi kodi ndiyo maana bidhaa zao zinauzwa bei nafuu kulinganisha na madukani,” alilalamika Agape Lema, mmiliki wa duka la vitenge eneo la Soko Kuu.
Akizungumzia hatua hiyo ya Rais, Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema inaweza kuwa ya kisiasa na kiutendaji.
‘Katika siasa, watawala wetu hawataki kuwapoteza wapigakura wao. Kila chama kinalinda wapigakura wake, kuna wamachinga, bobaboda na wengineo. Anahakikisha hawapotezi kwa sababu ndiyo watakaompigia tena kura mwaka 2020,” alisema Profesa Bana.
Kuhusu hatua hiyo, Profesa Aldo Lupala wa Chuo Kikuu Ardhi alisema tamko la Rais si la kutengua sheria lakini linazingatia haki.
Alisema Rais anaweza kutoa agizo la kutengua mabadiliko ya ardhi kupitia kwa waziri husika baada ya taratibu kadhaa kufuatwa ambazo hata hivyo, alisema hajui kama zilifuatwa.
Lakini alisema Rais ametumia uzalendo zaidi kwa kuhakikisha kwamba wananchi walio wengi wananufaika zaidi kuliko kulinda mwekezaji mmoja.
Imeandikwa na Jesse Mikofu, Sada Amir na Ngollo John na Kalunde Jamal
No comments :
Post a Comment