Na.Khadija Khamis –Maelezo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amewataka Mahakimu, makadhi na wasuluhishaji wa migogoro ya kazi kutekeleza majukumnu yao kwa uwadilifu wakizingatia kutoa haki kwa wanaostahiki kupata haki hizo.
Jaji Makungu aliyasema hayo katika hafla ya kuwaapisha Makadhi wa Wilaya, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo na wasuluhishi na waamuzi wa migogoro ya kazi chini ya kamisheni ya kazi katika mahakama kuu Vuga.
Aliwaeleza wasimamizi hao wapya wa sheria kuwa majukumu waliyokabidhiwa na Taifa sio mepesi na kuwataka kuzingatia maadili ya kazi ili haki na sheria iweze kuchukua nafasi yake.
Aidha alisema usuluhishi na utoaji maamuzi panapotokea migogoro katika sehemu za kazi inasaidia katika kujenga umoja na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi.
Waliapishwa kuwa Makadhi wa Mahakama ya Wilaya ni Idi Said Khamis na Sleiman Khamis Machano, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni Hakimu Amina Mohd Makame na Hamad Ali Sleiman, wasuluhishaji na waamuzi wa migogoro ya kazi ni Fatma Abdalla Hamad, Jokha Lali Ramadhani , Juma Ali Makame na Raya Said Ali .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya sheria duniani ambayo kilele chake ni tarehe tisa ya kila mwaka, Jaji Mkuu Omar Othman Makungu alisema shamra shamra za sherehe hiyo zitaanza tarehe nne mwezi ujao kwa matembezi ya hiari.
Aliongeza kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya sheria, utoaji wa vyeti kwa mawakili wapya na uzinduzi wa mahakama ya watoto katika kijiji cha Mahonda Wilaya ya Kaskazi B.
Alifahamisha kuwa kutakuwa na mikakati ya mipango kazi ambayo itasaidia kufanya kazi kwa wakati muafaka na kuwepo na utaratibu maalumu wa kuamua kesi ili kuepuka msongamano wa kesi katika mahakama ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Zanzibar alisema kaulimbiu ya siku ya sheria duniani mwaka huu ni kusimamia sheria na maadili katika kutenda haki.
No comments :
Post a Comment