MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MINDI KASIGA.
TANZANIA na Malawi zinatarajia kufanya mkutano wa kuimarisha uhusiano baina ya nchi mbili hizo.
Mkutano huo utafanyika Aprili 3 hadi 5, mwaka huu nchini Malawi ikiwa ni mwendelezo wa majadiliano ya kumaliza mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa unaozikabili nchi hizo kwa muda mrefu sasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mindi Kasiga, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Kasiga alisema atakayeiwakilisha Tanzania katika mkutano huo Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk. Augustine Mahiga.
“Tutakwenda Malawi kufanya mkutano wa siku saba lengo ni kutatua migogoro ya mipaka baina ya nchi hiyo na yetu," alifafanua.Alisema kupitia mkutano huo, wataongeza umoja na mshikamano na kutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara kwa pande mbili hizo na hivyo kufungua fursa nyingi zaidi zitakazonufaisha wananchi wa nchi hizo.
Kasiga alisema mkutano kama huo kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2003 hapa nchini na kwamba ukimya wa muda mrefu uliokuwapo ulitokana na mwingiliano wa ratiba uliochelewesha kufanyika kwa mkutano mwingine.
No comments :
Post a Comment