Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa nyumba hizo nyingi zinamilikiwa na watu binafsi na nyikngine zipo chini ya umiliki wa Kamisheni ya wakfu na mali za amani ambayo yamewekewa urithi baada ya wamiliki wake kufariki dunia.
Ofisa anayeshughulikia ukarabati wa majengo kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe, Awesu Mussa alisema ucheleweshaji wa kupatikana kwa vibali vya kukarabati majengo kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ni moja ya tatizo kubwa linalotishia uhai wa nyumba hizo na kuhatarisha usalama wa wananchi na wakazi wake.Alisema kwa mujibu wa masharti ya miji iliyopo katika orodha wa urithi wa hifadhi ya kimataifa kabla ya kufanyiwa matengenezo kwanza kunahitajika kibali ambacho kitaelekeza ukarabati huo ufanyike kwa kulingana na usanifu wa majengo ya asili.
Akielezea jengo lililoporomoka huko Hurumzi na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Khamis Kombo, alisema tayari Mamlaka ya Mji Mkongwe ilitoa kibali cha kufanyika kwa ukarabati wake na kilichotokea ni ajali.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mikakati ya kulibadilisha eneo la Darajani pamoja na Mji Mkongwe kwa kuyafanyia ukarabati mkubwa baadhi ya majengo kwa ajili ya kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa kwa ajili ya shughuli za kibiashara zaidi.
Alisema hata hivyo, kazi za kulifanyia ukarabati jengo refu la treni liliopo Darajani zimekwama kwa sasa kutokana na kushindwa kupatikana kwa kibali cha ujenzi wa jengo hilo kutoka Unesco.
/HABARI LEO
No comments :
Post a Comment