SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) Zanzibar limesema linahitaji jumla ya Sh bilioni 5 ili kukarabari na kuzifanyia matengenezo nyumba 26 zilizopo katika hali mbaya kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi humo.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Mohd Hafidh alisema hayo wakati alipokutana na uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na wataalamu wengine kutathmini hali ya majengo mbalimbali yaliyopo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Alisema baadhi ya majengo ya nyumba hizo ni zile zinazomilikiwa na Shirika la Nyumba la Serikali zilizokuwa nyumba za maendeleo.
“Tumefanya tathmini ya nyumba zilizopo katika hali mbaya ambapo tumebaini zipo nyumba 26 zinahitaji ukarabati mkubwa ambapo tumeomba Serikali kutoa jumla ya Sh bilioni tano kuzirudisha katika hali halisi ya ubora wake,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali imeweka malengo na mikakati ya kuufanya mji wa Zanzibar ikiwemo sehemu ya Mji Mkongwe kuwa kivutio cha watalii.
Alisema juhudi hizo ni pamoja na kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo yaliyopo Mji Mkongwe ambayo baadhi yake yapo katika hali mbaya ya uchakavu kiasi ya kutishia maisha ya wananchi.
“Tumeweka mikakati ya kufanyia ukarabati mkubwa majengo yaliyopo katika Mji Mkongwe na sehemu nyingine ili yawe kivutio kwa wageni,” alisema.
No comments :
Post a Comment