Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya utengenezaji, usafirishaji na uagizaji wa vifaa vifavyotumia mfumo wa Kisasa wa mawasiliano ya Nchini China { CEICE } ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar. Wa pili kutoka kushoto aliyevaa suti nyeusi na miwani ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya CEICE Kutoka Nchini China Bwana Liu Yang
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya CEICE Kutoka Nchini China Bwana Liu Yang upo akimkabidhi Balozi Seif zewadi ya Nembo ya Kampuni hiyo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya utengenezaji, usafirishaji na uagizaji wa vifaa vifavyotumia mfumo wa Kisasa wa mawasiliano ya Nchini China { CEICE } baada ya kumaliza mazungumzo yao Ofisini kwake Vuga.Picha na – OMPR – ZNZ.
Kampuni ya utengenezaji, usafirishaji na uagizaji wa vifaa vifavyotumia mfumo wa Kisasa wa mawasiliano ya Nchini China { CEICE } imeonyesha nia yake ya kutaka kujenga viwanda vya utengenezaji wa vifaa hivyo Visiwani Zanzibar katika azma yake ya kutoa huduma ndani ya ukanda wa Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika.
Naibu Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Kanda ya Kusini Mashariki ya Afrika Bwana Kang Kai alisema hayo wakati Ujumbe wa Viongozi Sita wa Kampuni hiyo kutoka Nchini China na Mjini Dar es salaam ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Kang Kai alisema Kampuni ya CEICE imeamua kuwekeza miradi yao Zanzibar kwa lengo la kuunga mkono mpango Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China wa kuelekeza nguvu zake za Uchumi katika kusaidia Maendeleo ya Bara la Afrika { China – Africa }.
Alisema kutokana na ongezeko kubwa la vyuo Vikuu Bara la Afrika hivi sasa linazalisha wasomi wengi ndani ya vyuo hivyo kundi ambalo linaweza kutumia taaluma yao kupitia ushirikiano na Miradi inayotekelezwa na Kampuni ya CEICE.
Bwana Kang Kai alisema Kampuni ya CEICE imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa vifaa vya Kieletronik na kuviuza kwa Makapuni makubwa ya Kimataifa yakiwemo yale ya Sam sung na Sonny.
Alisema ujenzi wa Viwanda hivyo ndani ya Visiwa vya Zanzibar mbali ya kuwapatia ajira wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu lakini pia watapata fursa ya kutumia vipaji walivyonavyo katika uzalishaji ndani ya viwanda hivyo.
“ Mpango wetu wa kutaka kuwekeza Visiwani Zanzibar unalenga kutoa ajira pana katika miradi ya Viwanda pamoja na Umeme unaoambatana na mfumo wa kisasa wa ulinzi unaotumia umeme yaani Security System ”. Alisema Bwana Kang Kai.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Vitega Uchumi na Maendeleo kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Nd. Shariff Shariff aliueleza Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya CEICE kwamba Serikali inahitaji Viwanda katika mpango wake wa kuelekea Nchi ya Viwanda.
Nd. Shariff alisema katika kuupa nguvu mpango huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga eneo maalum ndani ya Ukanda wa Maeneo huru ya Uchumi yaliyopo Fumba kwa ajili ya Taasisi na Kampuni zinazohitaji kutaka kujenga viwanda vyao Zanzibar.
Akitoa shukrani zake kwa Ujumbe huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema zaidi ya wakaazi Milioni 600 wanaoishi ndani ya ukanda wa Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika wanahitaji huduma muhimu za mitandao ya kisasa.
Balozi Seif alisema huduma za upatikanaji wa Vifaa kama TV, Simu na hata vitu vya umeme ni sehemu ya maisha kwa sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya mfumo wa uliopo hivi sasa unaoifanya Dunia kuonekana kama kiganja badala ya Kijiji.
Ujumbe wa Kampuni hiyo ya utengenezaji, usafirishaji na uagizaji wa vifaa vifavyotumia mfumo wa Kisasa wa mawasiliano ya Nchini China { CEICE } ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wake Bwana Liu Yang upo Nchini Tanzania kuangalia maeneo ambayo inaweza kuwekeza miradi yao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Kamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/3/2017.
No comments :
Post a Comment