Rais Dk Shein asisitiza mshikamano kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA)
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Jakarta, Indonesia 07.03.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuimarisha mashirikiano kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA), hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi kwa nchi hizo sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (I0RA), unaofanyika mjini Jakarta Indonesia, mkutano ambao unaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Jumuiya hiyo.
Katika hotuba yake aliyoisoma katika Mkutano huo, uliowashirikisha viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo, Dk. Shein alisema kuwa umefika wakati kwa nchi hizo wanachama wa Jumiya ya IORA kuimarisha zaidi ushirikiano pamoja kutatua changamoto zilizopo zikiwemo hali ya usalama, kupambana na uharamia baharini, vita dhidi ya madawa ya kulevya, ugaidi, athari za tabianchi na mambo mengine yanayoweza kuleta athari katika nchi wananchama.
Dk. Shein, alitoa wito kwa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya IORA kuongeza kasi katika utekelezaji wa malengo na maazimio ya Jumuiya hiyo ikiwa ni pamioja na kuitekeleza dhana ya uchumi wa bahari iliyoanzishwa mwaka 2015 na Jumuiya hiyo.
Aliongeza kuwa nchi zilizopo katika eneo la Ukanda wa Bahari ya Hindi ambazo zina idadi ya watu zaidi ya Bilioni 2 na pato la Taifa la jumla kwa Mataifa hayo lipatalo tirioni 9, iwapo zikishirikiana vizuri zinaweza kuleta maendeleo ya haraka hasa katika sekta nzima ya biashara za kimataifa na uwekezaji katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa, Jumuiya hiyo ina umuhimu mkubwa kwa nchi wanachama, kwani katika kipindi cha miaka 20 imefanya mambo mengi kwa nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya uvuvi, miradi ya kuendeleza na kudumisha utalii, Mradi wa Kudumisha Ushirikiano wa Utamaduni, kuimarisha usafiri wa bahari na Mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi na mengineyo.
Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli, Dk. Shein alisaini makubaliano yaliyofikiwa na Jumuiya hiyo katika mkutano huo na kuahidi kuwa Tanzania itachukua juhudi za makusudi katika kuyatekeleza makubaliano hayo kwa lengo la kuiimarisha Jumuiya hiyo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wajumbe kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuhudhuria mkutano utakaofanyika Zanzibar katika mwezi wa Septemba utakaohusiana na Utekelezaji wa Mikakati yenye kulenga kuimarisha uongozi wa masuala ya uvuvi, bahari pamoja na rasilimali zake.
Aidha, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Indonesia kwa mapokezi yao mazuri na ukarimu wao kwa viongozi na wageni waliohudhuria mkutano huo na kutoa pongezi kutoka kwa Rais John Pombe Magufuli aliyemuwakilisha katika mkutano huo kwa kutayarisha vyema mkutano huo ambao umepata mafanikio makubwa.
Dk. Shein alitoa pongezi zaidi kwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kwa ushirikiano mzuri na Serikali ya Indonesia kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya ya mkutano huo wenye kauli mbiu ya maadhimisho ya mika 20 ya Jumuiya hiyo isemayo “Kuimarisha ushirikiano wa bahari kwa lengo la kudumisha amani na usalama katika Bahari ya Hindi”.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Washirika wa mazungumzo ambao jumla yao ni nchi saba zikiwemo Jamhuri ya Watu wa China, Misri, Ufaransa, Japan, Uingereza, Marekani na Ujerumani kwa kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama wa Jumuiya ya IORA hatua ambayo imewezesha kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo katika nchi za ukanda wa bahari ya Hindi.
Jumuiya hiyo ambayo imetimiza miaka 20 tokea kuanzishwa kwake ina wanachama 21 wakiwemo Australia, Bangladesh, Comoro, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu, Indonesia, Malaysia, Madagascar, Msumbiji, Srilanka, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Yemen, India, Kenya, Mauritania, Oman, Singapore, Shelisheli, Afrika Kusini na Somali.
Viongozi wa nchi mbali mbali kutoka Jumuiya hiyo walipata fursa ya kutoa hotuba zao ambapo walisisitiza haja ya kuimarisha mashirikiano kwa nchi wanachama katika mipango ya kujiletea maendeleo sambamba na kuweka mikakati madhubuti katika kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuutumia vyema ukanda wa Bahari ya Hindi.
Walieleza kuwa hali ya amani na utulivu sambamba na kuweka mazingira mazuri ya kiuchumi iwapo yatafikiwa kwa pamoja maendeleo makubwa yataendelea kupatikana katika Jumuiya hiyo.
Mapema akitoa hotuba yake katika uzinduzi wa Mkutano huo wa viongozi wakuu, Rais wa Jamhuri ya Indonesia ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Joko Widodo alitoa pongezi kwa viongozi wote wa Jumuiya ya IORA na kusisitiza kuwa azma ya Jumuiya hiyo ni kuimarisha mashirikiano na urafiki kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili kuona zinaendelea kupiga hatua kimaendeleo, kiuchumi na kisiasa.
Aliongeza kuwa kuimarika kwa Jumuiya hiyo tokea ilipoasisiwa mwaka 1997, imeweza kuleta mafanikio makubwa kwa nchi wanachama na ikiwa ni pamoja na kutekeleza lengo la kukuza uchumi na kusisitiza haja ya uhifadhi wa mazingira hasa ya bahari, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kueleza kuwa ukuaji wa teknolojia nao utasaidia kuimarika kwa Jumuiya hiyo.
Mikakati mbali mbali ilielezwa na Wenyeviti wa vikao vilivyotangulia vikiwemo vikao vya Mawaziri pamoja na Wadau wengine kutoka nchi wanachama katika uzinduzi wa Mkutano huo wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi na Srrtikali wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika Mjini Jakarta Indonesia.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments :
Post a Comment