Mwakyembe asema kuwa tukio la kuvamiwa clouds hawezi kulifumbia macho
Nipashe ilitaka kujua kinachoendelea kuhusu uchunguzi dhidi ya Makonda ambaye kamati ya watu watano iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ilitoa ripoti ikidai Mkuu wa Mkoa huyo alivamia kituo cha TV cha Clouds akiwa na askari wenye bunduki na kutoa vitisho kwa wafanyakazi wa kituo hicho.
Kamati hiyo ilidai kubaini Makonda alifanya hivyo ili kulazimisha video ya mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, irushwe hewani.
Katika majibu yake, Dk. Mwakyembe alisema suala hilo ni “zito” na haliwezi kuachwa lipite bila kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Huku akiendelea kuikosoa ripoti ya kamati ya Nape ambayo amekuwa akisisitiza haijakidhi matakwa ya kikatiba na kisheria kwa kushindwa kumhoji Makonda, Dk. Mwakyembe alisema Mkuu wa Mkoa huyo atahojiwa kwa mambo tisa yanayohusiana na tukio hilo.
“Hili ni suala zito maana linahusisha uvamizi ambao ni kesi ya jinai,” alisema Mwakyembe ambaye ni daktari wa sheria na Waziri wa Katiba na Sheria mpaka wiki mbili zilizopita.
“Kuna vitu tisa ambavyo upande wa pili (Makonda) utaulizwa.”
Dk. Mwakyembe hata hivyo, alikataa kuvitaja vitu hivyo tisa huku akisita pia kutaja tarehe ambayo Makonda atahojiwa.
“Upande wa kwanza (Clouds TV) tayari umeshahojiwa na ripoti tunayo. Upande wa pili nao tutauhoji na wenyewe pengine una hoja,” alisema Dk. Mwakyembe.
“Ili kukidhi matakwa ya kikatiba na kisheria, ni lazima tuuhoji upande wa pili. Hili suala kama nilivyotangulia kusema ni la jinai. Lazima mtuhumiwa apate haki ya kujitetea.
“Ukifika mahakamani, hata yule mwenye kesi ya mauaji lazima tumpatie wakili, hata kama tunao uthibitisho kwamba ameua.”
Machi 29, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari alipokaribishwa ofisi kwake mjini Dodoma, Dk. Mwakyembe alisema hawezi kuikabidhi kwa wakubwa wake ripoti hiyo ya kamati ya Nape bila kuwapo na maelezo ya Makonda.
“Taaluma yangu ni sheria, hivyo siwezi kufanya jambo hilo la kupeleka malalamiko ya upande mmoja kwa mabosi zangu bila kusikiliza ule mwingine,” alisema Mwakyembe siku hiyo.
Alisema hatateua kamati nyingine ya kufuatilia jambo hilo, bali yeye na viongozi wenzake watakuwa kamati hiyo ili kuuhoji upande wa pili kisha kupeleka taarifa kwa wakuu wake ambao ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais mwenyewe.
JELA MIEZI SITA
Kamati ya watu watano iliyoundwa na Nape kuchunguza tukio la uvamizi wa televisheni ya Clouds ilibaini kuwa kiongozi huyo aliwatishia kuwafunga jela miezi sita wafanyakazi wake endapo wasingerusha kipindi alichokitaka.
Pia Kamati hiyo ilibaini Makonda aliwatisha kuwa angewaingiza wafanyakazi hao kwenye tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya kama wasingerusha kipindi chake.
Aidha, kamati ilibaini kuwa Makonda aliwatisha wafanyakazi wa kituo hicho ili wasitoe taarifa za uvamizi wake, kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Katibu wa Kamati hiyo, Deodatus Balile.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Dk. Hassan Abass, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO, ni Mhariri Mkuu wa Magazeti ya The Guardian, Jesse Kwayu, Nengida Johannes wa Upendo Media na Mabel Masasi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ilidaiwa Makonda akiwa na askari kadhaa wenye bunduki, alivamia kituo hicho na kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha ‘Da Wikend Show’ kurusha taarifa ya mama anayedai kuzaa na askofu Gwajima, bila ya kiongozi huyo wa kidini kupewa nafasi ya kusikilizwa.
Ingawa taarifa ni ya upande mmoja, kwa mujibu wa Balile mtuhumiwa alikubali kuwaona, lakini wakati wakipanda ngazi kwenda ghorofani iliko ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ilala jijini, Makonda aliteremka kwa kutokea mlango wa nyuma.
No comments :
Post a Comment