Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira Zanzibar, Ali Khalil Mirza alisema kwamba kazi ya utafiti imekwenda vizuri na watafiti hao walijiegemeza zaidi katika kitalu cha Pemba- Unguja ambapo waliweza kuruka kila siku kwa muda wa saa sita.
“Huu ni utafiti wa awali, nachukua fursa hii kuwajulisha kwamba wataalam wetu wamekamilisha kazi na wamefanikiwa kukusanya taarifa za kutosha kuhusiana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar” Alisema Katibu Mkuu Mirza.
Katibu Mkuu huyo alisema kwamba awali, kazi hiyo ilipangwa kufanyika kwa muda wa miezi miwili, mwezi mmoja ndio utafiti wenyewe,lakini wakaweka na mwezi mwengine ikiwa kutatokezea dharura yoyote ambapo haikuweza kutokezea na hivyo kukamilisha ndani ya wiki tatu.
Kiongozi wa timu ya Watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna alisema wamelamilisha kazi yao na kilichobakia ni taarifa zilizokusanywa kuwasilisha Uingereza kwa ajili ya uchambuzi wa kitaalamu.
Stefan alisema kuwa wametumia muda wa wiki tatu kufanya kazi hiyo tofauti na makisio ya awali ya miezi miwili kutokana na kuanza kwa kipindi cha mvua za masika.
“Ndege yetu ina vifaa ambavyo havihitaji vishindo, kama tutaruka wakati wa mvua na ngurumo za radi basi inaweza kuingia katika kurekodiwa kitu ambacho sisi hatukihitaji katika utafiti wetu na kwa sababu hiyo ilitulazimu kufanyakazi muda mwingi zaidi” Alisema Mtaalamu huyo.
Kiongozi huyo wa timu ya wataalamu alisema kazi yao ilikuwa kukagua miamba ilioko chini ya ardhi ambapo kwa kitaalamu kazi hii inajulikana “Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey” (FTG).
Stefan alisema kwamba katika kitalu cha Pemba -Zanzibar wameona chembechembe ya mafuta,lakini taarifa zaidi ya kuwepo kwa rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia itapatikana baada ya kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa taarifa yao watakayoiwasilisha Makao Makuu ya Kampuni ya Bell Geospace ya Uingereza.
Alisema kwamba kazi ya uchambuzi wa taarifa za kitafiti walizokusanya itakamilika ndani ya mwezi mmoja na wataikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.
Nae Mtaalamu wa masuala ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta kutoka Kampuni ya ya RAKGAS ya Ras Khaimah,Graham Cunningham ambaye pia ni Meneja wa Mkaazi wa RAKGAS Zanzibar, alisema kimsingi kazi iliyoko mbele ni kubwa zaidi kwani huu ni utafiti wa awali tu.
“Kuna kazi kubwa mbele yetu, utafiti huu uliofanywa tunauita FTG (Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey), utatusaidia kujuwa Object ilipo, lakini kazi bado inaendelea” Alisema Mtaalam huyo.
Alisema kwamba katika kipindi cha miezi mitatu au minne wanatarajia kuanza awamu ya pili ya utafiti kwa kutumia meli maalum ambayo itakuwa na kazi ya utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia katika mwambao wa pwani ya Zanzibar katika kitalu cha Pemba-Zanzibar.
Mtaalamu huyo alisema pia utafiti huo utahusisha gari maalum litakalokuwa likitafiti katika maeneo ya ardhini katika sehemu ambazo taarifa zake zimetolewa katika utafiti wa awali uliofanywa na ndege ya Kampuni ya Bell Geospace.
Kazi ya Utafiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar ilianza rasmi Machi 18 baada ya uzinduzi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd Machi 14 kwa Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza kufanya utafiti huo kwa niaba ya Kampuni ya RAK GAS ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.
/ Maelezo
No comments :
Post a Comment