Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akisalimiana na Uongozi wa Skauti Tanzania alipokutana nao kwa mazungumzo kumtaarifu maandalizi ya maadhimisho ya kutimia Miaka 100 ya Skauti Tanzania yanayotarajiwa kufanyika Makao Makuu Mjini Dodoma.
Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Skauti Tanzania hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mkuu wa Skauti Tanzania Bibi Mwatum Bakari Mahiza akitoa Taarifa za maadhimisho ya kutimia miaka 100 tokea kuanzishwa kwa Chama cha Skauti Nchini Tanzania.Wa kwanza kulia ni Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania Ndugu Abdulkarim Shah.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na kuagana na Skauti Mkuu Tanzania Bibi Mwatum Makari Mahisa Nje ya Ofisi yake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akiagana na Kamishna wa Skauti Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Maalim Ali Rajab.
Aliyesimama kati kati yao ni Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania Nd. Abdulkarim Shah.
Balozi Seif kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Skauti Tanzaania mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Na. Othman Khamis OMPR.
Chama cha Skauti Tanzania kinatarajia kuadhimisha miaka Mia Moja ifikapo Tarehe 21 hadi 28 Julai Mwaka huu katika Kampasi ya Chuo Kikuu Makao Makuu Mjini Dodoma kwa kushirikisha Vijana wapatao 5,000 kutoka Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na zaidi ya wageni 1,000 kutoka Nje ya Tanzania.
Mkuu wa Skauti Tanzania Bibi Mwatum Mahisa alieleza hayo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Tisa wa Chama hicho Bara na Zanzibar alipokuwa akitoa Taarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bibi Mwatum alisema vugu vugu la maadhimisho hayo limekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mh. Mizengo Piter Pinda alipofanya ziara ya kuhudhuria maadhimisho ya Skauti Nchini Uganda Mwaka 2016 na kushawishika na Maadhimisho hayo.
Alisema kutokana na uzito wa maadhimisho hayo Kitaifa yatakayoambatana na maonyesho na mambo mbali mbali Tuzo maalum zitatolewa kwa Marais waliopita pamoja na watu waliofanya ushujaa zaidi katika utekelezaji wa ujenzi wa Taifa kiuzalendo.
Mkuu huyo wa Skauti Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mipango imeanza kuchukuliwa katika hatua za awali za maadhimisho hayo ambapo Vijana Kumi wa Skuli za Msingi na Kumi Sekondari wataandaliwa kila Halmashauri za Wilaya Nchini washiriki kwenye tukio hilo muhimu.
Alieleza kwamba Wizara za Elimu, Afya, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje, Tamisemi pamoja na ile inayosimamia Utamaduni kwa upande wa Tanzania Bara zimeshateuliwa na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa kusimamia jambo hilo la Kihistoria.
Bibi Mwatum alifahamisha kwamba Mataifa Manne ya Kigeni ambayo ni Korea, Poland, Uganda, na Malawi yameshathibitisha kuhudhuria Maadhimisho hayo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina pingamizi kwa Vijana wake katika kushiriki Maadhimisho hayo ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania.
Balozi Seif alisema Skauti ni sehemu muhimu na adhimu kwa kuwaandaa Vijana katika muekeo wa kuwa na Utii, Heshima na Maadili mema, lakini kubwa zaidi ni kujengeka katika mazingira ya kuwa Wazalendo kwa Taifa lao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Viongozi wa Skauti Tanzania kwamba anaiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kutekeleza wajibu wa kulishughulikia suala hilo katika kuwaanda Vijana wa Zanzibar wawe sehemu ya maadhimisho hayo Kitaifa.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi huo wa Skauti Tanzania kwa utayari wao wa kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwa Chombo hicho muhimu Nchini Tanzania linafanikiwa.
Chama cha Skauti ndani ya Ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kimeasisiwa Visiwani Zanzibar mnamo Mwaka 1912.
No comments :
Post a Comment