Wakati Uchaguzi Mkuu wa Kenya ukikaribia, kampeni zikipamba moto na wanasiasa nchini kuonekana kuwa sehemu ya mchakato huo, muungano wa Nasa unadaiwa kuwa na mpango wa kuanzisha kituo cha kujumlisha matokeo nchini.
Hata hivyo, Serikali imekanusha madai hayo ikisisitiza kwamba haiwezi kuruhusu chama chochote kutoka Kenya kuja kuanzisha kituo cha kujumlisha matokeo kwa sababu kufanya hivyo ni kuingilia mambo ya nchi hiyo jirani.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 8 na wagombea wanaochuana vikali ni Rais Uhuru Kenyatta anayetetea nafasi hiyo kupitia chama cha Jubilee na Raila Odinga anayewakilisha muungano wa Nasa.
Gazeti la Daily Nation la Kenya liliripoti jana kwamba, Juni mwaka huu, Nasa ilitangaza kwamba itaanzisha vituo vitatu maalumu kwa ajili ya kujumlisha kura zake katika nchi za Kenya, Ujerumani na Tanzania.
Gazeti hilo lilibainisha kwamba Serikali ya Tanzania iliridhia mpango huo wa Nasa na kwamba kituo hicho kitawekwa huko Kigamboni. Pia, limeeleza kwamba Odinga alikuja Tanzania Mei kwa ajili ya maandalizi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga alisema amesikia maneno hayo lakini hakuna chama cha siasa cha Kenya kilichoomba kuanzisha kituo cha kujumlishia matokeo yake na kwamba Serikali haiwezi kukubali.
Dk Mahiga alisema wameihakikishia Serikali ya Kenya kwamba maneno hayo ni ya uongo, hakuna kitu kama hicho na Serikali haiwezi kuruhusu kwa sababu itakuwa ni kuingilia mambo ya ndani ya Kenya.
Rais John Magufuli na Edward Lowassa waliogombea urais nchini katika uchaguzi wa mwaka 2015 nchini, kupitia CCM na Chadema, mtawalia, wanatajwa kuongeza nguvu ya ushawishi kwa wapigakura wa Kenya.
Lowassa na chama chake wametangaza kumuunga mkono Rais Kenyatta kwa imani kwamba ndiye mgombea bora kwenye uchaguzi huo.
Lakini pia vyama vikubwa vya siasa vimekuwa vikijinadi kwamba vikipewa dhamana, vitaiga mfano wa Rais Magufuli katika kupambana na ufisadi nchini humo na kuzingatia masilahi ya watu wa chini.
Odinga amekuwa rafiki mkubwa wa Rais Magufuli na alimuunga mkono katika wa uchaguzi wa 2015.
Desemba 6, 2012 kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Kenya, Dk Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, alikwenda Kenya na kumpigia debe Odinga na chama chake cha ODM.
Urafiki huo uliendelea hata baada ya Dk Magufuli kushinda urais kwani Aprili mwaka jana, Odinga alikuja nchini kumtembelea na wawili hao walikutana Chato, Geita wakati Rais akiwa mapumziko.
Juzi, Lowassa aliyekuwa Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo, Joseph Nkaisery katika mahojiano na gazeti la Daily Nation, alisisitiza kwamba anamuunga mkono Kenyatta kwa sababu analinda uhuru wa demokrasia.
Hata hivyo, tofauti na Chadema, chama kingine cha upinzani nchini cha ACT-Wazalendo jana kilitangaza kuunga mkono muungano wa Nasa katika uchaguzi huo kikilekeza kuwa ni baada ya kupitia ilani za vyama vyote na kujiridhisha kwamba ndiyo upande pekee ambao wananchi wataupigia kura.
Katika barua iliyosainiwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, ACT-Wazalendo imebainisha kwamba imekuwa ikifuatilia siasa za Kenya na inaamini kwamba Nasa inaweza kuwaletea Wakenya mabadiliko ya kweli.
“Tumefuatilia ahadi na ilani zote za uchaguzi. Tumefikia uamuzi kwamba Nasa ndiyo chama ambacho Wakenya watafikiria kukipigia kura ili kiwaletee mabadiliko ya kijamii na kiuchumi na Afrika Mashariki kwa ujumla,” alisema Zitto katika barua hiyo, “Tunajua kwamba uchaguzi wa Kenya ni kwa ajili ya Wakenya kuamua lakini tunatambua pia kwamba Kenya imara ni EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki) imara. Tunaamini Nasa italeta uongozi imara chini ya kiongozi wake, Raila Odinga.”
/ Mwananchi
No comments :
Post a Comment