Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 31, 2017

BURIANI ALHAJ SHEIKH AHMED ISLAM!

Na Ramadhani K. Dau, Malaysia
Ilikuwa siku ya Jumamosi tarehe 23 Disemba 2017, majira ya saa 5 usiku kwa saa za Malaysia nilipopata ujumbe mfupi wa sms kutoka kwa Sheikh Issa Othman, maarufu Mufti wa London, Imam wa Masjid Maamur ukiniarifu msiba wa mzee wetu Sheikh Ahmed Islam. Ujumbe wake ulikuwa mfupi sana: “Mzee wetu Ahmed Islam amefariki sasa hivi. Maiti inaletwa msikitini hivi sasa. Maziko kesho In Shaa Allah. Innallillahi Wainnaillahi Raajiuun”.
Mara tu baada ya kupata taarifa hiyo na baada ya kumtakia maghfira mzee wetu, nikajua kuwa kwa mara nyingine tena umeniangukia wajibu wa kuandika Taazia ya mtu ambaye namfahamu, namheshimu na alikuwa na ukaribu sana na mimi. Nimeshawahi kuandika huko nyuma kuwa kuandika Taazia ni jambo zito na gumu sana. Kila niandikapo hutamani sana Taazia hiyo iwe ndio ya mwisho. Lakini kwa mipango Yake Mwenyezi Mungu, najikuta nashindwa kukwepa wajibu huo. Hata hivyo, mara hii nilidhani ningeweza kuukwepa wajibu huo kwa kumuomba rafiki yangu na ndugu yangu mwanahistoria maarufu Sheikh Mohamed Said aandike Taazia hiyo nami nilikuwa tayari kumpa maelezo yoyote ambayo yangemsaidia katika uandishi wake. Pamoja ya kuwa alikubali kuifanya kazi hiyo, Mohamed alisisitiza kuwa lazima na mimi niandike. Kwa jinsi ya msisitizo aliouweka Sheikh Mohamed, nimejikuta kwa mara nyingine tena  nalazimika kuandika Taazia hii huku nikiwa na moyo wa huzuni sana kwa kuondokewa na mzee wangu ambaye alikuwa mithili ya baba yangu mzazi.
Marehemu mzee Ahmed Islam ana mambo mengi na sura nyingi. Wapo wanaomfahamu kama ni miongoni mwa wazee maarufu na viongozi katika jamii ya Waislamu, wapo wanaomfahamu kama mtaalamu wa masuala ya Rasilimali Watu (Human Resources) na wapo wanaomfahamu mzee Ahmed Islam kama mwana michezo mahiri.
Marehemu mzee Ahmed Ijhad Islam alizaliwa Zanzibar tarehe 22 Disemba 1930 akiwa ni mtoto pekee wa Sheikh Ijhad Islam na bibi yetu Bi Maryam Mussa. Kwa bahati mbaya, mzee Ijhad Islam alifariki wakati mzee Ahmed akiwa mdogo na hivyo akalelewa na mama yake. Baada ya msiba huo, bibi yetu Bi Maryam aliolewa na kupata mtoto mmoja wa kike ambaye jina lake ni Zerah.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi na Sekondari kwenye Government School (sasa Ben Bella) Zanzibar mwaka 1948, ilipofika mwaka 1957 marehemu mzee Ahmed Islam alikwenda Cornwall, Uingereza kuchukua masomo katika fani ya Mawasiliano yaani Telecommunications. Wakati huo alikuwa ameajiriwa na kampuni ya Cable and Wireless (C&W) ambako alikuwa Meneja Msaidizi (Assistant Manager). Kampuni hii ilikuwa ndiyo kampuni kubwa ya mawasiliano Afrika Mashariki. Baada ya kurudi masomoni, marehemu aliendelea na kazi yake na baada ya kampuni ya C&W kumezwa na Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki (East African Post and Telecommunication), mzee Islam akahamia Dar es Salaam mwaka 1970. 
Akiwa Dar es Salaam mzee Islam alifanyakazi katika Shirika hilo na baada ya mgawanyiko yakaundwa Mashirika mawili tofauti; Shirika la Posta (TPC) na Shirika la Simu (TTCL). Marehemu mzee Islam alihamishiwa TTCL hadi alipostaafu mwaka 1986 akiwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu yaani Director of Manpower. Baada ya kustaafu, marehemu alifanyakazi Ubalozi wa Ufaransa kwa mkataba wa miaka 3. Wakati wa uhai wake, mzee Islam amefanya mengi katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi wa dini, ujenzi wa nchi, uendelezaji wa michezo na utoaji nasaha kwa Taasisi na vijana mbalimbali katika masuala ya ndoa na kujiendeleza kwenye elimu ya juu.  
Kwa upande wa dini, marehemu ametoa mchango mkubwa sana. Miongoni mwa matunda ya kazi yake ni usimamizi wa ujenzi wa Masjid Maamur iliyopo Upanga, Dar es Salaam. Kwa wanaokumbuka vizuri jiografia ya Upanga, kabla 1987 pale palipojengwa Masjid Maamur hapakuwa na msikiti. Lakini kwa kushirikiana na wazee wenziwe marehemu mzee Islam aliweza kusimama kidete katika kusimamia ujenzi wa Masjid. Si wengi wanaofahamu kuwa ujenzi wa Masjid Maamur ulianza na msukusuko mkubwa kwa sababu kulikuwa na mwanajeshi ambaye alikuwa amepanga kwenye nyumba ya jirani ambayo ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).  Mwanajeshi yule alikuwa anatumia kiwanja cha msikiti kufugia mifugo na kulima mboga. Siku moja marehemu mzee Islam alikwenda kwenye kiwanja kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa msikiti. Yule mwanajeshi hakutaka msikiti ujengwe pale pamoja ya kuwa kiwanja hicho kilikuwa mali halali ya Msikiti. Hivyo basi, akatoka na bastola na kutaka kumshambulia mzee Islam kwa risasi.  Marehemu mzee Islam hakuogopa. Badala yake alimwambia yule mwanajeshi afyatue risasi haraka ili amfungulie njia ya kwenda peponi.  Mwanajeshi akabaki ameduwaa na hatimaye akaondoka. Baada ya hapo ujenzi ukaendelea kwa amani na yule mwanajeshi akahamishiwa Songea. Ilipofika mwaka 2013, marehemu mzee Islam pia alichangia kwa kiasi kikubwa usimamizi wa ukarabati mkubwa wa msikiti huo kwa ufadhili mkubwa wa kampuni ya Oil Com.
Mbali na Masjid Maamur, marehemu mzee Islam pia alitoa mchango mkubwa sana katika ujenzi wa Masjid Ngazija hapa Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya sana tokea ukoloni hadi leo, katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Central Business District), hakuna msikiti wowote mkubwa wala mdogo zaidi ya msikiti wa Ngazija. Lakini msikiti huo ambao ulijengwa wakati wa ukoloni ulikuwa ni mdogo sana kiasi cha kutokidhi mahitaji ya Waumini. Hivyo basi kwa kushirikiana na viongozi wengine kama vile marehemu Sheikh Aboud Maalim, marehemu Profesa Haroub Othman Miraji, Sheikh Saidi Kassim, Habibu Nuru, AbdulHamid Mhoma na wengineo, marehemu mzee Islam alishiriki kusimamia ujenzi wa msikiti mpya wa Ngazija ambao kwa sasa una ghorofa 3 na ndio msikiti pekee uliopo Dar es Salaam Central Business District. Pamoja na usimamizi wa ujenzi wa misikiti, mzee Islam ametunga vitabu mbali mbali vya dua na nyiradi na alikuwa mmoja wa wasimamizi wa uradi wa kila wiki Masjid Ngazija na Masjid Rawdha. 
Mchango wa marehemu mzee Islam katika kuwaendeleza vijana wa Kiislamu kielimu ni mkubwa bila kifani. Nina hakika si watu wengi wanaofahamu kuwa mzee Ahmed Islam ndiye ambaye aliyefanikisha kupatikana kwa kiwanja ambacho kwa sasa imejengwa shule ya Sekondari ya AlHaramain jijini Dar es Salaam. Naishauri BAKWATA ambayo ndio Wamiliki wa Shule ya AlHaramain wathamini mchango wa mzee Ahmed Islam kwa kulipa jina lake moja ya madarasa au kumbi za shule. Aidha mzee Islam alikuwa mstari wa mbele kwenye Taasisi ya Tanzania Muslim Solidarity Trust Fund katika kusimamia nafasi za masomo za vijana wa Kiislamu wanaokwenda kusoma Uturuki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kiislam (Islamic Development Bank) iliyopo Jeddah, Saudi Arabia. Chini ya ufadhili huo, kwa karibu miaka 30 sasa Benki hiyo imekuwa ikifadhili vijana wa Kiislamu 15 kwenda kusoma masomo ya Uhandisi (Engineering) na Utabibu (Medicine) kwenye Vyuo Vikuu nchini Uturuki. Miongoni mwa watu walionufaika na mpango huu ni Dr. Hussein Mwinyi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr. AsanteRabi Kighoma Malima wa Chuo Kikuu cha Northeastern Marekani, Dr. Mashavu, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, Dr. Munawwara Kaguta daktari wa hospitali ya Aga Khan na wengine wengi.  
Moja ya mafanikio makubwa ya jitahada za marehemu mzee Islam ni uvumbuzi ambao ulifanywa mwezi Agosti 2014 na Dr. AsanteRabi Kighoma Malima ambaye alivumbua kifaa cha kuweza kubaini maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na saratani (cancer) yakiwa katika hatua za awali kabisa. Kutokana na uvumbuzi wa kifaa hicho ambacho amekiita Biolom, Dr. Malima alipewa tuzo na Gavana wa jimbo la Massachusetts, Bwana Deval Patrick. Haya ni matunda ya mzee wetu Ahmed Islam ambayo yameiletea sifa kubwa sana nchi yetu katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia. Aidha mwaka 2002, mzee Islam aliishawishi Taasisi ya Muslim Aid ya London kuja kujenga maabara 3 za kisasa katika shule ya Sekondari ya Twayyibat iliyopo Temeke Dar es Salaam. Katika kipindi hicho hicho, kwa kupitia Muslim Aid, mzee Islam pia alifanikisha ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Sotele, Kisiju Mkoa wa Pwani. Harakati za marehemu mzee Islam kuwasaidia vijana katika kutafuta elimu hazikuanzia Dar es Salaam. Wakati akiwa Zanzibar, marehemu alikuwa akiwahimiza sana vijana kusoma na yeye binafsi alikuwa akijitolea kuwapa vijana mafunzo ya ziada (tuition) usiku kwa kutumia taa za kibatari/koroboi.
Marehemu mzee Islam alikuwa Mcha Mungu sana. Pamoja na kuwa na umri mkubwa wa miaka 87 na kuandamwa na maradhi ya miguu, kamwe hakuacha kuswali swala zote katika msikiti Maamur. Siku zote alikuwa wa kwanza kuingia msikitini na kuswali kwenye kiti msitari wa mbele. Hata wakati alipopata maradhi ambayo yalihitimisha safari yake hapa duniani, hakuacha kwenda kuswali msikitini. Wiki tatu kabla ya kufikwa na umauti, kwa muda wa siku mbili mfululuzo alikuwa hawezi kula vizuri na matokeo yake akawa hana nguvu. Hata hivyo ilipofika siku ya Ijumaa akataka lazima aende msikitini. Watoto wake walimsihi sana lakini hakukubali. Ikabidi abebwe apelekwe Masjid Maamur kwa ajili ya swala ya Ijumaa na hiyo ndio ikawa Ijumaa yake ya mwisho kuswali msikitini. Ijumaa iliyofuata wazee wa Masjid Maamur pamoja na watoto wake wakamsihi sana awe anaswali nyumbani. Ikabidi akubali kwa shingo upande kwani hakuwa na njia nyingine ya kwenda msikitini isipokuwa kwa kubebwa na wabebaji ndio hao waliomtaka aswali nyumbani.
Mwaka 1997, nilibahatika kusafiri kwenda Umra na marehemu mzee Islam wakati Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lilipofanya safari yake ya kwanza kwenda Jeddah, Saudi Arabia. Katika safari yetu walikuwepo marehemu mzee Ahmed Rashad Ali, marehemu Siraju Juma Kaboyonga na mkewe marehemu Jaji Madina Muro, marehemu Prof. Haroub Othman, marehemu Balozi Selemani Hemedi, Dr. Idris Rashid, Jenerali Ulimwengu, mama Fatma Maghimbi, Mhe Hamad Rashid, mwanahistoria Sheikh Mohamed Saidi na wengineo. Wengi walimshuhudia takriban kwa siku zote tulizokuwa safarini, marehemu mzee Islam alikuwa anaamka usiku kufanya ibada. 
Jambo hili la kuswali Tahajud limethibitishwa na mmoja kati ya watoto wake ambaye alizaliwa mwaka 1961. Anasema yeye amemshuhudia baba yake akiswali Tahajud kila siku tokea apate fahamu. Inasemekana alianza utaratibu huu wa kuswali usiku kuanzia mwaka 1951 na hakuacha kisimamo cha usiku mpaka maradhi yalipomzidi mwishoni mwa mwaka huu. Siri nyingine aliyokuwa nayo marehemu mzee Islam ni kudumisha Sunna ya kufunga siku za Jumatatu na Alhamisi. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanawe, amemuona baba yake akifunga Sunna hii tokea yeye alipokuwa mdogo. 
Mzee Islam alikuwa mtu wa watu na alikuwa mwepesi sana wa kusaidia watu wenye matatizo. Aidha mzee Islam alikuwa anapenda sana kusuluhisha watu. Milango ya nyumba yake ilikuwa wazi saa zote ambapo watu wa rika zote walikuwa wanaenda kila siku kutaka misaada au ushauri.  Mzee Islam alikuwa jeshi la mtu mmoja na alikuwa zaidi ya Taasisi. Hapa ntasimulia matukio matatu kati ya matukio mengi sana ambayo yanaonesha ukarimu na utayari wa marehemu katika kusaidia watu. Siku moja mama mmoja kutoka mkoa wa Kilimanjaro alikwenda nyumbani kwa mzee Islam akiwa na watoto wa kike watatu ambao wote walikuwa yatima. Baada ya kueleza matatizo yake na ugumu wa maisha ya kulea wale mayatima, marehemu mzee Islam akamshauri wale watoto wabaki kwake na yeye atachukua jukumu la kuwalea na kuwasomesha. Yule mama akakubali rai ile. Hivi niandikavyo Taazia hii, mtoto mmoja amemaliza masomo ya Shahada ya kwanza katika Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa sasa anafanyakazi Tanga. Mwingine amemaliza Shahada ya Uzamili katika fani ya Uthamini vifaa vya ujenzi (Masters Degree in Quantity Survey) kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam. Na wa mwisho hivi sasa anachukua Stashahada (Diploma) ya Uhasibu. 
Tukio la pili lilitokea mwaka 1991 wakati kijana mmoja alipokwenda nyumbani kwa mzee Ahmed Islam kumuomba msaada wa kwenda masomoni Ujerumani. Kama ilivyo kawaida yake, mzee Islam hakusita na alisimamia uchangishaji wa fedha kwa ajili ya safari masomo ya kijana huyo. Leo hii, kijana huyo ni daktari bingwa nchini Ujerumani. Mifano kama hii ipo mingi na nafasi haitoshi kuisimulia yote.
Tukio la tatu lilitokea mwaka 2008 na linamhusu kijana ambaye alikuwa na tatizo la ada ya kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kijana yule alihitaji nusu ya ada (shs. 400,000) ili asajiliwe na Chuo. Baada ya kuhangaika sana alipata shs. 100,000. Hatimaye kuna mtu alimwelekeza kwa mzee Ahmed Islam. Alipofika nyumbani kwake na kueleza shida yake, mzee Islam akamwomba arudi siku ya pili. Naam, aliporudi siku ya pili alimpa shs. 300,000 na yule kijana akarudi chuoni kuendelea na masomo. Kana kwamba haitoshi, wakati yule kijana yupo masomoni, kuna mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mzumbe ambaye ni yatima alikuwa na tatizo sugu la nyonga. Kwa kuona hali yake ilivyo, yule kijana wa Chuo Kikuu akamchukua mgonjwa hadi nyumbani kwa mzee Ahmed Islam. Kwa kuwa uso umeumbwa na aibu, yule kijana akabaki barabarani na akamuelekeza mgonjwa nyumba anayokaa mzee Islam. Marehemu alimtafuta daktari bingwa wa kumshughulikia yule yatima hadi akapona. Hivi sasa yule yatima ni Mhandisi baada ya kuhitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa upande wa michezo, mzee Islam hakuwa nyuma. Wakati wa uhai wake, alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu kiasi cha kuitwa mchawi wa mchezo huo. Alipokuwa Zanzibar alicheza timu ya Vikokotoni na timu ya Taifa ya Zanzibar. Akiwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar, mzee Islam alishiriki katika mashindano kadhaa ikiwemo mashindano maarufu ya kombe la Gossage akicheza namba 10. Mwaka 1952 timu ya Taifa ya Zanzibar ilifika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika Nairobi Kenya na kushika nafasi ya pili baada ya kuzifunga timu za Tanganyika na Uganda. Pamoja wachezaji wengine, timu ya Zanzibar iliwakilishwa na marehemu mzee Ahmed Islam, marehemu mzee Abdul Majham Omar, Mzee Mwinyi (Mpiringo), Seif Rashid na Maulid Mohamed (Machaprala). Pamoja na umahiri wake wa kucheza mpira wa miguu, mzee Islam alikuwa mchezaji hodari wa Kriket na mpira wa magongo (hockey). Kama ilivyo kwenye mpira wa miguu, marehemu mzee Islam alichezea timu za Taifa za Zanzibar kwenye Kriket na Hockey.  
Wakati wa uhai wake, mzee Islam alikuwa mzungumzaji wangu sana sio tu kwenye masuala ya jamii lakini pia masuala ya michezo. Mimi na marehemu tulikuwa tunakubaliana kwenye mambo mengi sana isipokuwa mambo mawili ambayo tulikubaliana kutokubaliana. Kwanza kwenye upenzi wa mpira kwa timu za hapa nyumbani  marehemu mzee Islam alikuwa mpenzi mkubwa wa Yanga wakati mimi ni mpenzi wa Taifa Stars. Kwa upande wa timu za nje ya nchi, mzee Islam alikuwa anaipenda sana Manchester United. Bahati mbaya sikuwahi kumuuliza sababu ya yeye kuipenda Manchester United. Kama sababu ni kutembelea jiji la Manchester wakati alipokuwa masomoni Uingereza, basi nilitarajia angeipenda Manchester City kwa sababu klabu hiyo ndio ipo katika jiji la Manchester wakati timu ya Manchester United ipo shamba kabisa kwenye kitongoji kidogo kinachoitwa Old Trafford. Kwa hapa nyumani, kitongoji cha Old Trafford mfano wake ni kama vile Dar es Salaam na Ruvu Darajani pale panapouzwa samaki wakavu au mbele kidogo kwenye kijiji cha Vigwaza. Wenyewe Waingereza wanasema there is only one team in Manchester (Manchester kuna timu moja tu) ambayo ni Manchester City. Pia wanao msemo wao unaosema there is only one football team in London; the Gunners! (London kuna timu moja tu ya mpira wa miguu; washika Bunduki). Najua Balozi Saleh Tambwe na Balozi Juma Mwapachu watalipinga hili. Lakini haya si maneno yangu. 
Niliwahi kuandika mapema mwaka huu kuwa kutokana na vifo vilivyoongozana vya wazee wa Dar es Salaam, jiji letu limebaki kuwa na ukiwa. Mwaka huu tumeshuhudia kuondokewa kwa Kamanda Dr. Mohamed Chiko, mzee Iddi Sungura, mzee Issa Ausi (smart boy), Ali Bob, mzee Kitwana Selemani Kondo, Balozi AbdulKarim Omar Mtiro (Cisco), Kleist AbdulWahid Sykes na sasa mzee Ahmed Islam. Jiji la Dar es Salaam limegubikwa na huzuni kubwa. Lakini kwa sababu kifo ni faradhi hatuna budi tuikubali hali hiyo.
Mzee Islam ametangulia lakini ameacha simulizi ambazo zitazungumzwa kwa miaka mingi sana baada ya yeye kuondoka. Wakati wa uhai wake, marehemu mzee Islam na mama yetu Bi Rukia Ahmed Iddi ambaye alifariki 1989 walijaaliwa kupata watoto sita ambao ni Islam, Biubwa, Mohamed (maarufu Eddy), AbdulRahman, Abubakar na Mussa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Amrithishe mzee wetu Ahmed Islam Jannat Firdous kama Alivyosema Mwenyewe kwenye Quran Sura 23 Aya 1-11 pale Alipozitaja sifa za watu wema kisha Akamalizia kwa kusema Atawarithisha Firdous na wataishi humo milele. Pia tunamwomba Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema na Atukutanishe na mzee wetu Ahmed Islam kwenye Firdous. Aaamiin.

No comments :

Post a Comment