Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu amefunguka na kumtaka Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Mtungi kujitafakari, kwani amedai kuwa Jaji huyo amekuwa ni mpofu kwa mambo mabaya wanayofanyiwa watu wa upinzani nchini.
Lissu amesema hayo kufuatia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuwaandikia barua CHADEMA ambayo anadai inatuhuma mbalimbali pamoja na vitisho mbalimbali
"Nimesoma barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, yenye tuhuma na vitisho vingi dhidi ya CHADEMA, bila kutoa ushahidi wowote na kwa kutegemea taarifa za upande mmoja tu.
"Msajili Mutungi ameituhumu CHADEMA kwa kufanya siasa za kibabe na vurugu na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa. Msajili Mutungi anastahili kujibiwa hadharani na kukumbushwa mambo kadhaa. Inaelekea amejisahau sana au anafikiria Watanzania ni wajinga wasioelewa mambo yake.
"Msajili wa Vyama vya Siasa amekosa sifa na uadilifu (moral authority) ya kunyooshea kidole CHADEMA au chama kingine chochote cha upinzani kuhusiana na jambo lolote linahusu Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.
"Tangu 2015 nchi yetu imeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Vyama vya Siasa ukifanywa. Mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ambavyo ni haki ya vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria hiyo, imepigwa marufuku bila uhalali wowote. Msajili Mutungi hajawahi kukemea ukiukwaji huo wa sheria wala kutetea haki ya vyama vya siasa
"Viongozi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, wameuawa, wametekwa nyara na kupotezwa, wamepigwa risasi katika majaribio ya kuuawa, wameteswa, wamekamatwa na kushtakiwa kwa kesi za uongo.
"Msajili Mutungi amekuwa bubu na kiziwi asiyesikia wala kukemea uonevu na ukandamizaji huu dhidi ya vyama anavyovisimamia. CCM na serikali yake zimetoa hongo kurubuni madiwani, wabunge na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao.
"Yote ni makosa ya maadili kwa mujibu wa sheria. Msajili Mutungi hajawahi kuliona hilo."Ameandika Tundu Lissu
No comments :
Post a Comment