Viongozi wa madhehebu ya dini walikutana jijini Dar es Salaam jana pamoja na wanasiasa kujadili "hofu iliyotawala" miongoni mwa wananchi inayosababishwa na kutokea kwa matukio ya mauaji na watu kutekwa nchini.
Viongozi hao pia walijadili uimara wa taasisi za madhehebu ya dini, uimara wa mfumo wa serikali, pamoja na uimara wa taasisi za vyama vya siasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Katika siku za karibuni, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22) alifariki kwa kupigwa risasi na polisi akiwa kwenye daladala jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.
Rais John Magufuli alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter Jumapili "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."
Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa sana na kifo cha Akwilina, na kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.
Aidha, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ambaye pia alikuwa katibu wa Chadema kata ya Hananasif, Daniel John, alikutwa ameuawa na mwili wake kutupwa katika ufukwe wa Coco jijini Dar es Salama pia wiki iliyopita baada ya kutekwa mwanzoni mwa mwezi na watu wasiojulikana.
Akizungumza katika kikao hicho, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza alisema hofu nchini bado ipo baada ya kuwapo kwa matukio ya watu kupigwa risasi na kutekwa.
"Sijawahi kuona risasi za moto zikirushwa kwa raia, watu wanapigwa risasi mchana kweupe, sasa inatakiwa tufike mahali tuseme basi," alisema Askofu Bagonza.
Alisema viongozi wa dini wataendelea kuonya matukio kama hayo pindi yatakapotokea bila ya kujali nani yupo madarakani.
Naye Amiri Mkuu wa Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Yusuph Kundecha alisema ni kweli hofu miongoni mwa wananchi ipo baada ya kuwapo kwa matukio ambayo hawajawahi kuyaona miaka ya nyuma.
Alisema hofu hiyo inatokana na baadhi ya matamshi ya viongozi wanayoyatoa kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa.
Akizufungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia alisema:"Tanzania bado kuna hofu, vipo viashiria ambavyo siyo vizuri.
"Kuna Watanzania wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi, akiwamo binti Akwilina. Wengine wamepotea, wengine wametekwa na kuuwawa.
"Bado kuna manung'uniko, malalamiko miongoni mwa wananchi, mauaji yanatokea, Watanzania wana hofu juu ya matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu."
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, alisema lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kujadili lengo la 16 katika 17 ya malengo ya millennia, ambalo linahusu amani, haki na taasisi imara.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema Watanzania siyo kwamba wana hofu tu, bali hata hali ya kuishi haipo.
Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alisema kongamano hilo limejikita katika kuwa na mazungumzo ya kujenga amani.
Alisema Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani na kwamba watu wanapoandamana, kuuawa, kukaidi amri ya polisi maana yake hakuna amani nchini.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), Kilumbe Ng'enda alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye amani kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Nchi za Maziwa makuu.
"Kwenye nchi hamuwezi kukaa kama mpo peponi, lazima mtatofautiana," alisema Ng'enda, "(lakini) Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye amani."
Viongozi wengine wa dini waliohudhuria ni Askofu Dk. Alinikisa Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristu nchini, Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk. Fredrick Shoo, Askofu Moses Matonya, Askofu Stephen Munga na Askofu Ebem Mshiu.
Pia Sheikh Hassan Kebeke ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya viongozi wa amani Mwanza alikuwepo.
No comments :
Post a Comment