Nondo ,aliyedaiwa kujiteka
Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania (TSNP) umesema usingeweza kupuuza taarifa za hatari ya usalama iliyokuwa ikimkabili mwenyekiti wao Abdul Nondo.
Taarifa za kupotea kwa Bwana Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka tarehe 6 Machi baada ya Nondo kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa usalama wake uko hatarini.
Hali hiyo ilipeleka taharuki miongoni mwa wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla huku wengi wakidhani kuwa bwana Nondo alikuwa ametekwa.
Akizungumza na BBC mapema hii leo, msemaji wa TSNP Helllen Sisya amesema taarifa za nini hasa kilichomsibu bwana Nondo zinakinzana
"Sisi bado hatuamini Uchunguzi uliofanywa na polisi kwa kuwa hatujamsikia Nondo akiongea na kile tulichoelezwa na polisi mkoani Iringa na hiki tulichokisikia leo kwa polisi Dar es Salaam haviendani", alisema Sisya.Mtandao wa wanafunzi(TSNP)
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania ambao ulitoa taarifa kwa Umma kuhusu kupotea kwa Abdul Nondo,hawakubaliani na taarifa hiyo ya polisi kwa kudai kuwa inakanganya,Polisi wanadai kuwa alipatikana akiendelea na shughuli zake za kawaida alipoenda kumtembelea mpenzi wake na wakati wao walipata taarifa kutoka kwa jeshi la polisi wa Iringa kuwa Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui.
Mapema leo Jeshi la polisi nchini Tanzania lilizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam,Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa ulikuwa uzushi.
Kamanda wa Polisi,Lazaro Mambosasa amedai kuwa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua taharuki mnamo tarehe 6,Machi kwa madai kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana si za kweli kwa kuwa uchunguzi wa jeshi la polisi umebaini kwamba mwanafunzi huyo alikutwa akiendelea na shughuli zake za kawaida na wala hakutekwa au kutoa taarifa kuwa ametekwa. Afande Lazaro Mambosasa
Upelelezi umebaini kuwa alikuwa anafanya mawasiliano na mpenzi wake wakati yuko safarini kutoka Dar es salaam kuelekea Iringa hata baada ya muda aliodaiwa kutuma ujumbe kuwa yuko hatarini.
Lakini jeshi hilo la polisi halikuishia kwenye mawasiliano ya simu tu bali lilienda kumpima afya yake na kubaini kuwa ni mzima wa afya na hana tatizo la akili.
Aidha jeshi la polisi limedai kuwa litaendelea kumshikilia mpaka atakapopelekwa mahakamani kusikiliza kesi yake kuhusu uzushi na imetoa onyo kwamba haitamhurumia mtu yeyote atakayesambaza taarifa za namna hiyo.
Viongozi wa mtandao wa wanafunzi wametakiwa kufika kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo hivi karibuni nchini Tanzania kumekuwepo na visa vya mauaji na kutoweka kwa watu bila kujua kiini cha kutoweka kwao.
/ BBC
No comments :
Post a Comment