dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, September 20, 2018

Serikali yasitisha matangazo ya uzazi wa mpango!

SERIKALI imesitisha matangazo yanayohamasisha uzazi wa mpango yanayorushwa kwenye runinga na redio mbalimbali nchini mpaka itakapotangazwa tena.

Sitisho hilo limetolewa katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya kwenda kwa Shirika la Msaada la Marekani (USAID).

Shirika hilo ndilo linalofadhili mradi wa Tulonge Afya unaotoa matangazo hayo ya kuhamasisha uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari.Nipashe ilipomtafuta Dk. Ulisubisya ili kuthibitisha kama barua hiyo ni ya wizara, alikiri kutoka wizarani na kwamba wameamua kufanya hivyo ili kujipanga kwa ajili ya kuandaa ujumbe mpya.

“Ni kweli tumetoa taarifa hiyo, tunataka kuboresha ujumbe kuhusu mpango wa uzazi salama kwa Tanzania,” alisema kwa kifupi.

Barua hiyo iliyosambaa mitandaoni juzi, ilieleza kuwa serikali inatambua mchango na juhudi za shirika hilo katika kuboresha uzazi wa mpango.

Ilieleza kuwa wizara inakusudia kufanya marejeo ya maudhui yote ya matangazo kwenye runinga na redio kwa ajili ya uzazi wa mpango.

“Hivyo unaombwa kusimamisha mara moja kutangaza na kuchapisha maudhui yoyote yale ya uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari mpaka itakavyoamuliwa vinginevyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Akiwahutubia mamia ya watu Septemba 9, mjini Meatu Mkoani Simiyu, wiki mbili zilizopita, Rais John Magufuli alisema Watanzania waendelee kuzaa, lakini wachape kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wanaowazaa.

Alisema anafahamu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango, lakini mengine yeye (Magufuli) hakubaliani nayo.

“Najua Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango hapa, lakini mimi mengine huwa sikubaliani nayo sana, utapangiwaje kuzaa...kwa hiyo katika kushauriwa mengine tukubali na mengine tukatae tutumie msemo wa mzee Jakaya Kikwete ‘Ukiambiwa changanya na za kwako’ kuzaa ni muhimu,” alisema.

Katika mkutano huo Rais Magufuli aliwaeleza wananchi kuwa katika mataifa ya kigeni aliyowahi kuishi hakuwahi kusikia wimbo wa uzazi wa mpango.

“Mimi Ulaya nimekaa, nafahamu madhara ya kutokuzaa, nchi gani sijakwenda, Japan nimekaa, Uingereza nimekaa mwaka mzima, Ujerumani nimekaa, Canada nimekaa na nikachaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mawaziri Ardhi Duniani, nimekaa Denmark, Norway, China nimefika sasa utanidanganya wapi,” alisema.

Mwaka huu serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetenga Sh. bilioni 14 kwa ajili ya huduma ya uzazi wa mpango.


No comments :

Post a Comment