Watu wanaoishi pembezoni mwa pwani ya nchi ya Marekani wameanza kupatwa na mshtuko mkubwa baada ya upepo mkali ambao unatokana na kimbunga Florence kuanza kupiga kwenye maeneo hayo.
Maafisa wa serikali wamesema kuwa huenda mawimbi makubwa ya baharini na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zitaharibu maeneo mbalimbali ya Kaskazini na Kusini mwa Jimbo la Carolina ambalo linapatikana mjini Columbia.
Maafisa hao wameongeza kuwa upepo wa kimbunga hicho unavuma kwa kasi ya maili 100 kwa saa (155 km/h) huku nyumba takribani 100,000 zimeharibiwa miundombinu yake ikiwemo huduma ya umeme na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.
Pia inadaiwa kuwa kimbunga hicho kinaweza kikauwa watu wengi sana huku wasiwasi mkubwa umetawala uwezekano wa kutokea mafuriko makubwa. Wakati huo huo watu zaidi ya milioni moja katika maeneo ya pwani ya Kaskazini na Kusini mwa Carolina na Virginia walikuwa wametakiwa kuyahama katika makazi yao.
Hata hivyo maelfu ya watu walitafuta hifadhi katika vituo vya muda vya huduma za dharura Alhamisi usiku wakati hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi huku upepo ukiongeza nguvu kiasi katika maeneo ya pwani hizo.
Watabiri wa hali ya hewa wametahadharisha kwamba maji ya mafuriko huenda yakafikia kina cha futi 13 (mita 4) na katika baadhi ya maeneo, huenda upepo mkali ukasababisha maji ya mito kuanza kurudi nyuma.
Safari 1,400 za ndege zimefutwa kwa mujibu wa mtandao wa FlightAware.com kutokana na viwanja vingi vya ndege maeneo ya pwani vitaathiriwa. Pia wakazi katika maeneo ya Hawaii wametahadharishwa kuhusu kimbunga kingine kinachofahamika kwa jina Olivia.
Watabiri wa hali ya hewa wanasema kimbunga cha Olivia ambacho kina upepo unaovuma kwa kasi ya maili 65 kwa saa, kitafikia maeneo ya bara Jumatano asubuhi na kusababisha mvua kubwa.
No comments :
Post a Comment