Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya siku ya Uhuru, Disemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha shamrashamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma ambayo itaitwa Uhuru Hospitali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Amesema hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa mkoani humo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. “Wanaweza kutumia siku hiyo kwa kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali.”
Kufuatia maagizo hayo, Waziri Mkuu amewataka wananchi katika maeneo yote nchini wajiandae kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazopangwa na wakuu wao wa mikoa na wilaya kufanyika katika maeneo yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments :
Post a Comment