Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein, akijumuika na Waumi wa Kiislam Zanzibar katika sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa Mtume (S.A.W) akiitikia dua ikisoma na Mufti Mkuu wa Zanzibar kulia Sheikh Saleh Omar Kabi, yaliofanyika katika viwanjavya maisara suleiman Zanzibar jana usiku.19-11-2018.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Mdhamini wa Maulidi ya Mfungo Sita. Sheikh Sherali Champsi, alipowasili katika viwanja vya Maisara Suleiman kuhudhuria Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad(S.A.W) yaliofanyika jana usiku 19-11-2018, kaitika viwanja hivyo.
Na.Abdi Shamnah.Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, jana amejumuika na mamia ya waumini wa Dini ya kiislamu kutoka Mikoa yote ya Unguja, kuadhimisha uzawa wa Mtume Muhammad (SAW).
Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Maisara mjini hapa, ambapo Viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali, Mabalozi na wanafunzi kutoka Madrasa na Vyuo vya Qraaan walishiriki.
Uzawa wa Mtume Muhammad (SAW), huadhimishwa kila ifikapo mwezi 11, Rabi - Ul -Awal ya kila mwaka.
Akitoa waadhi kwa waislamu waliohudhuria Maulid hayo, Mstahiwa Naibu Kadhi Mkuu Khamis Othman Kombo alitowa wito kwa waumini wa Dini hiyo kuendeleza wajibu wa kufuata maadili na mwenendo mwema aliokuja nao Mtume, akibainisha kuwa hatua hiyo ni ukamilifu wa imani.
Alisema kuja kwa utandawazi Duniani, kumeifanya jamii ya Wazanzibari na hususan vijana kujiingiza katika mambo maovu, ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia na hivyo kwenda kinyume na miongozo wa dini .
Aliwakumbusha waislamu wajibu wa kutekeleza kwa dhati yale yote aliyokuja nayo Mtume kwa kuwa yeye ndio kigezo chema kutoka kwa Mola muumba.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kudumisha amani n utulivu nchini muda wote, hali inayotowa nafasi kwa wananchi kupata fursa adhimu ya kuabudu.
Nae, Sheikh Mohammed Kassim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, alikemea tabia iliojengeka miongoni mwa waumini ya kushindwa kufuata maadili na tabia njema alizokuwanazo Mtume Muhammad (SAW).
“Inatupasa kubadili nyendo na tabia zetu na kufuata maadili na mwenendo mwema aliokuwa nao mtume wetu”, alisema.
Alisema jamii ya kizazi kiliopo imeyapa kisogo mafunzo aliyokuja nayo Mtume kwa kushindwa kuwaheshimu na kuwatii wazee, hivyo kwenda kinyume na mwenendo aliodumu nao ikiwa ni kigezo cha unyenyekevu.
Alibainisha kuwa Mtume Muhammad (SAW) amesifiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa na tabia nzuri, hivyo aliwataka waumini kufuata mwenendo wake pamoja na kushinda changamoto mbali mbali zinazotokana na utandawazi.
Aidha, Sheikh Kassim aliwataka waislamu kujikita katika utamaduni wa kumsalia Mtume pale anapotajwa, kuvuta tasbikh pamoja na kufanya istifar ili kupata fadhila, huku akiwaonya baadhi ya waumini (walioibuka katika siku za hivi karibuni) wanaopinga ibada hizo.
Maadhimisho ya Maulid ya uzawa wa Mtume Muhammad (SAW), yalifunguliwa kwa Qoraan tukufu, iliyosomwa na Ustadhi Mtumwa Juma Kombo kutoka Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja .
Aidha, yaliambatana na usomaji wa Milango sita (6) ya Barazanji, Maulid ya Homu kutoka Mtendeni mjini Unguja pamoja na usomaji wa Kaswida kutoka Madrsa mbali mbali.
No comments :
Post a Comment