Mke wa Mdhamini wa Chinjio Binafsi la Kisakasaka Bwana Kheir Juma, Bibi Khadija Abdulla akielezea hatua zinazochukuliwa katika chinjio hilo za harakati za Uchinjaji wa Ng’ombe.
Afisa Mifugo wa Baraza la Manispaa la Wilaya ya Magharibi “B” Bibi Hawa Said Kassim akimtembeza Balozi Seif sehemu mbali mbali za Chinjio la Kisakasaka alipoifanya ziara ya kushtukizia.
Baadhi ya maeneo ya ndani ya Chinjio la Kisakasaka ikiwa katika hatau za mwisho za kukamilishwa ujenzi wake.
Afisa Mifugo wa Wilaya ya Kaskazini “B” Dr. Hassan Ibrahim Khamis Kulia akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya harakati za Uchinjaji Ng’ombe katika Chinjio la Donge alipofanya ziara ya kustukizia.
Balozi Seif akiagiza umuhimu wa usafi wa mazingira katika maeneo ya Machinjio ili kuwa na bidhaa salama ya nyama kwa matumizi ya Wanaadamu.
Na.Othman Khamis OMPR.nA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali haikatai kuruhusu Machinjio Binafsi katika baadhi ya maeneo Mitaani, lakini kinachohitajika na kuzingatiwa zaidi ni taratibu zilizowekwa zinazofuatwa na usafi wa mazingira.
Alisema Mwananchi au mfugaji ye yote aliyeamua kuweka chinjio kwa ajili ya Mifugo yake anaweza kufanya hivyo kama atakamilisha maelekezo atakayoagizwa na Taasisi zinazosimamia Mifugo, Mazingira na Halmashauri ya Wilaya anayowekeza.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mapema asubuhi alipoamua kufanya ziara ya kushtukizia katika Machinjio ya Serikali ya Kisakasaka na Donge pamoja na yale Binafsi ya Kisakasaka na Aneani Donge kuangalia hali hasili ya Kimazingira inayoyazunguuka Machinjio hayo.
Alisema licha ya jitihada kubwa za usafi wa mazingira zinazochukuliwa na wasimamizi wa Machinjio hayo hasa yale ya Serikali lakini bado ana mashaka kwa yale machinjio Binafsi ambapo Uongozi wa Halmashauri husika unapaswa kufuatilia kila wakati kujua mazingira halisi ya maeneo hayo.
Balozi Seif alisema Nyama inayotayarishwa katika maeneo hayo baada ya shughuli za uchinjaji inalazimika kuwa safi muda wote ili kwenda kwa mtumiaji katika mazingira salama ya Kiafya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba atakuwa tayari kufanya ziara za ghafla wakati wowote ili kujiridhisha na mazingira ya Maeneo hayo yanayopaswa kuwa katika hali inayokubalika kiafya muda wote.
Mapema Mafisa Mifugo wa Baraza la Manishaa Wilaya ya Magharibi “B” Bibi Hawa Said Kassim ambae alikutwa akisimamia harakati za matengenezo za Chinjio la Kisakasaka alimueleza Balozi Seif kwamba hatua za kukamilisha Jengo hilo zimefikia hatua njema.
Bibi Hawa alisema kazi ya uchinjaji wa Ng’ombe inatarajiwa kurejea tena kuanzia Usiku wa Kuamkia Ijumaa ili kuondoa usumbufu wanaoupata wa kazi hiyo iliyokuwa ikifanywa katika chinjio la muda la Mtu Binafsi liliopo Kisakasaka kufuatia ushauri wa Bodi ya Dawa na Kumlinda Mlaji.
Alisema Chinjio hilo la Kisakasaka linahudumia uchinjwaji wa Ng’ombe 50 kwa siku kazi inayoanza saa sita usiku na kuendelea hadi alfajiri baada ya Madaktari kuwafanyia uchunguzi ng’ombe wanaohitaji kuchinjwa, uchunguzi unaoendelea tena baada ya kupatikana nyama.
Alieleza kwamba idadi hiyo ya Ng’ombe wakati mwengine huongezeka mara dufu kutegemea wakati wa siku kuu unaozunguukwa na mahitaji mengi ya utumiaji nyama katika mapishi tofauti.
Naye Afisa Mifugo wa Wilaya ya Kaskazini “B” Dr. Hassan Ibrahim Khamis alisema Uongozi wa Wilaya kupitia Watendaji wake wanaosimamia masuala ya Mifugo na Mazingira wamekuwa na utaratibu wa kufanya ziara za kushtukizia kuangalia hali ya mazingira ya maeneo ya Machinjio.
Dr Hassan alimueleza BaloziSeif kwamba yapo Machinjio ndani ya Wilaya hiyo ambayo yamefungwa kutokana na kutokidhi viwango vilivyowekwa na mengine kuagizwa kufanya marekebisho baada ya wakaguzi kutoridhika na hali hiyo.
Alisema Chinjio la Serikali la Donge hivi sasa linaendelea kutoa huduma kama kawaida ya uchinjwaji wa ngombe wasiopungua 21 kwa siku licha ya upungufu wa ng’ombe unaosababishwa na baadhi ya wafugaji kuamua kupeleka Machinjio binafsi kwa kuepuka gharama.
No comments :
Post a Comment