Fundi Mkuu Renny
NANI ANASEMA LISSU ANAICHAFUA NCHI?
By Malisa GJ
Tundu Antiphas Mughwai Lissu ameanza kupasua mawimbi katika anga za kimataifa. Majuzi alikua BBC Swahili, kisha akaalikwa kwenye kipindi chenye heshima sana duniani cha BBC HardTalk. Inakadiriwa karibu watu milioni 350 walimfuatilia LIVE achilia mbali wale waliofuatilia marudio ya kipindi.
Siku chache zijazo atakuwa Marekani kwa mwaliko wa kituo kikuu cha habari nchini humo cha CNN. Atafanya mahojiano pia na Radio Umoja wa mataifa, na mashirika mengine ya utangazaji. Zipo taarifa pia kwamba amealikwa kuhutubia mkutano mkuu wa umoja wa mataifa utakaoanza September 17 hadi 24 mwaka huu.
Hizi ni platform kubwa sana kimataifa na ambazo baadhi ya viongozi hawajawahi kupata fursa hata ya kualikwa tu. Wapo viongozi pamoja na kukaa madarakani miaka kadhaa hajawahi kuhojiwa hata na BukedeTV ya Uganda. Wakisemwa kwenye BBC HardTalk wanaenda kujibu kwenye Kapu la TBC au Chereko.
Ni wazi heshima hii aliyopewa Lissu ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa akili ambao Mungu amemjalia, na kama watanzania tunapaswa kujivunia hilo.
Sasa kuna watu wameweweseka kumuona Lissu akipata platform kubwa kiasi hicho. Wameanza kunena kwa lugha. Chakubanga anaongea, Spika anaongea, Msukuma anaongea, hadi Bashite na zero zake anaongea, utadhani alielewa chochote katika hayo mahojiano ya Lissu na BBC 🤣🤣.
Kwahiyo wameanza propaganda kwamba Lissu anaichafua nchi huko nje. Hebu tujadili. Je ni kweli Lissu anachafua nchi?
Kuchafua (defame) ni kutoa madai ya uongo (false allegations) kuhusu mtu/kitu fulani. Kama umepata division one, mtu akasema umepata zero hapo amekuchafua. Lakini kama umepata zero (kama Bashite) na mtu akasema umepata zero, hapo hujachafuliwa. Umeelezwa ukweli. Kwahiyo kuchafua ni lazima utoe madai ya uongo. Principle number moja ya defamation (whether Libel or slander) ni lazima iwe uongo.
Sasa je, Lissu ametoa madai yoyote ya uongo kuhusu serikali ya Tanzania? Lissu amesema watu wanaoikosoa serikali wanakamatwa na kufungwa. Je ni uongo? Yericko Nyerere ni mhanga, Henry Nkya ni mhanga, Bob Chacha Wangwe ni mhanga. Hawa ni wachache walioonja jela kwa kuikosoa serikali ya JPM. Sasa uongo wa Lissu uko wapi?
Lissu amesema kipindi cha utawala wa JPM watu wengi wamepotea katika mazingira yanayotilia shaka. Ben Saanane alipotea wiki chache baada ya kukosoa PhD ya Rais. Mwandishi Azory Gwanda alipotea akiwa anafuatilia habari za mauaji ya Kibiti. Na wengine wengi wamepotea ktk mazingira ya kutatanisha. Sasa uongo wa Lissu uko wapi? Hawa watu wamepotea au hawajapotea?
Lissu anasema serikali ya JPM ina double standards katika kufanya kazi. Inatoa fursa kwa chama chake kufanya shughuli za kisiasa lakini vyama vingine vinazuiwa. Hapo kuna uongo gani?
Kila mara tunawaona CCM wakifanya mikutano, vikao na maandamano tena kwa kulindwa na jeshi la polisi. Lakini wapinzani hata wakifanya vikao vya ndani tu wanakamatwa. Kule Geita wafuasi wa Chadema walikamatwa kwenye kikao cha ndani wakapigwa sana, na kukaa mahabusu kwa miezi 13 kabla ya mahakama kuwaachia huru baada ya kuwakosa na hatia.
Lissu amesema Polisi wa Tanzania wanaua watu na hawachukuliwi hatua zozote. Kule Mwanza polisi walimuua mtoto mchanga baada ya kumkamata mama yake na kukataa asimpeleke hospitali kupata matibabu. Hapa Dar polisi walimuua Aquilina kwa kumpiga risasi bila hatia yoyote. Hivi ukatili huu ukisemwa hadharani ndio kuchafua nchi? Kwahiyo ili tusiichafue nchi inabidi watu wakifanyiwa ukatili tukae kimya? What a shame!!
Kukaa kimya katikati ya uovu ni kuunga mkono uovu huo. Viongozi wa dini walipokutana na Rais, nchi nzima ililalamika kwanini hawakumueleza kuhusu watu kutekwa na kupotea, kwanini hawakumueleza kuhusu watu kuuawa na kutupwa kwenye sandarusi, kwanini hawakumueleza kuhusu vyombo vya dola kukiuka haki za binadamu? Kwanini hawakumueleza kuhusu kudumaa kwa demokrasia. Watu walilalamika sana wakasema viongozi wa dini wametuangusha.
Sasa amepatikana mtu wa kuyaeleza hayo katika media za kimataifa ambazo Rais mwenyewe atasikia na dunia itajua, halafu mnasema anachafua nchi? Hivi anayechafua nchi ni anayeteka na kuua watu au anayesema watu wanatekwa na kuuawa? Yani kila mara tunaokota maiti kwenye sandarusi hatuoni tatizo, lakini anayesema maiti zinaokotwa ndio anaonekana tatizo. Malabuku.!!
Dr.Chriss Cyrilo anahoji "Hivi anayeua watuhumiwa ndani ya vituo vya polisi kwa kipigo ni Lissu? Aliyetishia kuwapiga Shangazi za watu ni Lissu? Aliyekataza mikutano ya kisiasa kwa vyama vya upinzani na kupendelea chama chake ni Lissu? Anayetumia fedha za umma kama pochi yake bila idhini ya bunge ni Lissu? Aliyemteka Mo Dewji ni Lissu? Aliyempoteza Ben Saanane na Azory Gwanda ni Lissu? Sasa Lissu anachafuaje nchi?"
Halafu kuna tofauti kati ya nchi na serikali. Nchi yetu haijachafuka ila serikali ndio imejichafua. Serikali sio nchi. Hata Shetani ana serikali yake lakini hana nchi. Zipo serikali zinazoongozwa na magaidi, waasi, misukule na hata mapepo. Serikali ya Somalia imekua ikiongozwa na vikundi vya waasi tangu kuangushwa kwa utawala wa Rais Siad Barre. Serikali ya Ujerumani imewahi kuongozwa na gaidi Adolph Hittler, serikali ya Afrika kusini imewahi kuongozwa na makaburu.
Kwahiyo Lissu hajaichafua nchi, bali serikali ya imejichafua yenyewe kwa matendo yake. Anachofanya Lissu ni kurudia tu, na hiyo haimaanishi kuchafua bali kutangaza uchafu. Na kutangaza uchafu sio kuchafua. Ni sawa na mlevi mlevi ajikojolee halafu watoto wakimzomea aanze kuwatuhumu kwamba wanamchafua. Wanamchafua au kajichafua mwenyewe na mikojo yake?
Kwahiyo wanaosema Lissu anachafua nchi ni watu wenye upeo mdogo wa akili, wasioweza hata kutofautisha serikali na nchi. Serikali sio nchi.
Nyerere alipokosoa serikali ya kikoloni aliambiwa anachafua nchi, Mandela alipokosoa serikali ya kikaburu aliambiwa anachafua nchi. Wanaharakati wa haki za binadamu walipokosoa utawala wa Hittler waliambiwa wanaichafua Ujerumani. Ni kawaida kwa serikali za kidikteta, kigaidi, kikaburu na za kikoloni kuhusianisha tawala zao na nchi. Kwamba ukikosoa serikali unaambiwa unachafua nchi. Shame.!
Serikali sio Nchi. Serikali zote duniani zinapita, lakini nchi zinadumu. Na uzalendo ni kuipenda nchi yako, uzalendo sio kujipendekeza kwa serikali yako.
Cyrilo anasema 'Wanaodai Lissu anaichafua nchi wajitazame wao kwanza. Waache ulevi wa kulewa chakari na kujikojolea halafu wakizomewa wanasema watoto wanawachafua'
Malisa GJ
No comments :
Post a Comment