Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dk. Haji Mwemvura akimkaribisha Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed kuzindua Bodi hiyo katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Mkemia Mkuu Maruhubi.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati akiizindua rasmi Bodi hiyo katika Ofisi ya Mkemia Mkuu Maruhubi.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Afya na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya uzinduzi uliofanyika Ofisi ya Mkemia Mkuu Maruhubi. Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezo
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashidi Mohamed ameishauri Bodi ya mpya ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuangalia uwezekanao wa kuvitumia vifaa vya Tiba vilivyopo kwa ajili ya kazi nyengine za Tafiti za Kisayansi. Amesema Wizara ya Afya inavyo vifaa vingi vya Tiba ambavyo havijatumika kikamilifu na vinaweza kusaidia kwa shughuli nyengine mbali mbali za maendeleo zikiwemo za Utafiti.
Waziri Hamad alieleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Pili ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyofanyika jengo jipya la Ofisi hiyo eneo la Maruhubi.
Alisema kitu muhimu kwa Bodi hiyo ni kuongeza ubunifu na kuzaa mawazo mapya ambayo yataweza kusaidia kuongeza matumizi kwa baadhi ya vifaa ambavyo vimekuwa vikitumika kwa muda mchache na uwezo wa kutumika ni mkubwa.
Hata hivyo Waziri wa Afya aliitaka Bodi ya Ushauri ya Maabara ya Mkemia Mkuu kutoa kipaumbele suala la rasilimali watu kwa kuwatafutia masomo wafanyakazi wanaosimamia mashine za maabara hiyo kwani Teknolojia inabadilika kwa haraka sana. Aliitaka Bodi kujiandaa kutoa elimu kwa wananchi na muhimu zaidi ni kuipeleka kwa wananfuzi wa Skuli ili waelewe umuhimu wa Sayansi tunayoendelea nayo katika maendeleo ya Taifa.
Katika kujenga utashi wa kisiasa, Waziri wa Afya ameishauri Bodi hiyo kutoa elimu kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na makundi mengine ya kisiasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Aidha amesisitiza umuhimu kwa Bodi kusimamia matumizi bora ya mashine ya maabara hiyo ili ziweze kudumu muda mrefu ujao.
Alisema Serikali imetumia fedha nyingi kununu mashine za maabara hiyo, ikiwemo ya kuchunguza vinasaba vya watoto wanaozaliwa ambayo kwa miaka mingi ilikosekana Zanzibar. BMwenyekiti wa mpya wa Bodi hiyo Dk. Haji Mwemvura Haji alimuhakikishia Waziri wa Afya kwamba watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipolifungua jengo hilo hivi karibuni.
Dk. Mwemvura alimshukuru Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi hiyo Dk. Yussuf Nuhu kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Akitoa shukrani zake, Mwenyekiti aliemaliza muda Dk. Yussuf Nuhu aliishauri Serikali kuandaa utaratibu kwa taasisi zinazoendesha tafiti za kisayansi kufanyakazi kwa pamoja kwani baadhi ya taasisi hizo zina mashine za kisasa lakini zimekuwa hazitumiki kikamilifu na zinaweza kusaidia katika taasisi nyengine.
No comments :
Post a Comment