WIVU WA KUPITA KIASI NI HATARI!
Msichana aliyeshuhudia anaeleza:
Nilikuwa nasali Masjid Haram (Makka) , nikamuona mwanamke mzee analia sana, akiomba dua na kulia... Pembeni yake kulikuwa na kijana aliyekuwa akimjia mara kwa mara kumjulia na kumuhudumia.
Nilimtizama sana mama yule na nikasema moyoni: "Bila shaka ana jambo linalomliza hivi." Basi nikamsogelea na kumuuliza:
"Mama, mbona unalia hivyo, kitu gani kimekusibu?
Mwanzo alisita kunijibu, lakini baada ya kuwa kimya kwa muda hivi, akasema:
"Sina neno, hakuna lolote baya!"
Lakini kwa jinsi nilivyomuona, nilijua kuna kitu kinamtatiza, kwa hiyo nikam-bana hadi akanieleza. Akaanza:
"Mimi nilikuwa nimeolewa na mume mzuri Ma Shaa Allah, aliyenipenda, kunikirimu, kunijali na kuniheshimu, isipokuwa mimi nilikuwa na ila moja; nilikuwa sizai.
Baada ya kuishi miaka mingi na mume wangu katika hali hiyo, huku akiwa hana furaha, hatimaye nikamshauri mume wangu aoe mke wa pili. Kwanza alikataa. Lakini nikamsihi mpaka akakubali".
"Nikamtafutia binti, nikamposea na hatimaye akamuoa.
Lakini baada ya muda mfupi tu, nilianza kufanya wivu, kwani mume wangu ambaye hapo awali tulipendana kwa dhati, alianza kulemea upande wa bi mdogo! Mambo yaliniwia vigumu baada ya hiyo mkewe kushika ujauzito kwani nilzidi kuwa na wivu kama mwenda-wazimu
Baada ya bi. mdogo kujifungua, mume alikuwa na furaha kwa kupata mtoto wa kiume, nami nikabaki kufikiri "ilikuaje nikaamua kumwambia aoe?"
Siku moja akanijia na kuniambia anasafiri na mke wake mdogo na wataniachia mtoto wao nikae naye mpaka watakaporudi!
Ulikuwa wakati wa majira ya kusi ambapo jioni moja nikawa nimeweka makaa ya moto kwenye chetezo cha kufukizia. Mtoto akiwa na umri wa mwaka na miezi kadhaa, akausogelea moto ule nami nikiwa nachemka kwa wivu, nasema na nafsi yangu: "Wamekwenda zao huko kula raha wananiachia mimi mtoto kama yaya!”
Mtoto yule alisogelea makaa ya moto na badala ya kumzuia kuyashika, nilimshika mkono hasa nikauweka kwenye makaa ya moto na kumuunguza sana.
Baada ya kufanya hivyo ndio nikahisi joto la moyoni limepungua. Tukalala usiku huo, mara tukapata habari ya kufariki kwa mume wangu na mkewe katika ajali ya barabarani wakati wakirudi kutoka safari yao!
Nikabaki peke yangu na Mola wangu kisha na mtoto huyu tu ambaye umemuona akinihudumia hapa. Na Ma- Shaa-Allah, ndiye anayenihudumia na kunitimizia mahitaji yangu yote.
Kila nikimtizama mkono wake roho yangu yaniuma kwa uchungu na hasa pale anaponiita yumma; na mpaka sasa sijamwambia kama mimi siye niliyemzaa na ndiye niliyemuunguza mkono wake!!
Jambo hili linaniadhibu moyoni mwangu mpaka hii leo?!!
Hapa unaponiona mwanangu ndiyo namuomba Mola wangu anisamehe dhambi yangu hii niliyoifanya! Halafu mwanangu, tazama hikma ya Allah! Kama si Allah kisha huyu kijana, ningekuwa kwenye hali gani!?
ALLAH ATUAMBIA KATIKA KITABU CHAKE KITUKUFU
CHA AL-QUR'AN KWAMBA "HUENDA MKACHUKIA KITU KUMBE NACHO KINA KHERI KWENU" SURATIL BAQARA - 2:216
Hapo hapo baada ya huyo mama kuniambia maneno hayo, yule kijana akatokea hali akiuficha mkono wake, akaja na kum-busu mama yake kwenye paji la uso wake na kumwambia: "Sasa mpenzi wangu, tunakwenda zetu au bado?"
No comments :
Post a Comment