Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, November 6, 2019

FORMER ZANZIBAR ATTORNEY GENERAL (OTHMAN) WRITES - "HILI LA CAG NI FEDHEHA KWA TAALUMA YA SHERIA TANZANIA"!

Anaandika Muheshimiwa *Othman Masoud Othman* aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa FBI nchini Marekani, James Comey, ameandika katika kitabu chake A HIGHER LOYALTY maneno ya kuleta tafakuri kubwa. Amendika _“it is very hard to leave a group of people who are committed only to doing the right thing”_. Alikuwa anaeleza ugumu wanaopata watu waadilifu katika utumishi wa umma kutenda mambo kwa kufata sheria na taratibu. Mara 
 nyingi hujikuta wapo peke yao. Athari ya wanayokutana nayo ni kuzidisha hofu 
 kwa wengine wenye ujasiri na hatimaye kuendelea kuporomoka kwa maadili ya utendaji wa umma.

Katika hili la CAG, imeonyesha wazi kwamba wanasheria katika ngazi mbali mbali hawakutimiza wajibu wao. 

Ibara ya 144 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeeleza wazi kama ifuatavyo:

*_"144 (1) bila ya kuathiri masharti mengine yaliyomo katika ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Jamhuri ya Muungano atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka siti au umri mwingine wowote utakaotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge”_*

*_“(2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aweza tu kuondolewa katika 
 madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake(ama 
 kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,  na hataweza kuondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya [4] ya ibara hii”_*

Ibara hiyo ya Katiba inaeleza wazi kwamba umri wa kuacha kazi wa Mdhibiti na 
 Mkaguzi Mkuu ni miaka 60. Hata hivyo Bunge limepewa uwezo wa kubadili umri na sio muda wa kazi wa Mdhibiti na Mkaguzi. Ni kanuni ya msingi ya kutafsiri sheria kwamba neno linapokuwa na maana mahsusi, haliwezi kutaftiwa tafsiri nyengine mbadala inayopingana na maana mahsusi ya neno hilo. Ibara ya 
144 (1) ilikusudia kuweka umri wa kustaafu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kama ulivyowekwa umri wa kustaafu wa Majaji chini ya ibara ya 110 ya Katiba ambao nao ni miaka 60.

Ibara ya 144 haitoi mwanya kwa Bunge kutunga Sheria ya kuweka muda wa 
 kuendelea na kazi kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ambao utamfanya aondolewe kazini kabla ya muda uliowekwa na Katiba au kuongezwa na Sheria [miaka 65].
Hili linathibitishwa zaidi na ibara ya 144 (6) ya Katiba inayosema: 

*_“ Mtu ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu au aliyepata kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hawezi kuteuliwa kushika au kushikilia madaraka ya kazi nyingine yoyote katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano”_*

Kwa ibara hiyo, Profesa Musa Assad hawezi hata kukaimu nafasi yoyote katika utumishi wa umma, na hivyo atakuwa amestaafishwa katika utumishi wa umma kabla ya umri wa kustaafu. Hakuna kiumbe cha namna hiyo katika utumishi wa umma. Ikitokea hivyo, tafsiri sahihi ni kuwa mtu huyo amefukuzwa au kukatishwa utumishi wake. Na hilo, ni batili ya wazi kwa vile inakiuka masharti ya ibara ya 144(2) na (3) ya Katiba.

Sheria au tafsiri inayotoa mwanya kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuondolewa kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kisheria na kwa matakwa ya Rais bila ya kufuata masharti ya wazi ya utaratibu wa kumuondoa kabla ya kufikiksha umri wa kustaafu chini ya ibara ya 144(3) na (4), inavunja msingi wa kinga ya kikatiba [security of tenure].

Inasikitisha sana unapoona wanasheria katika mazingira kama haya, ambapo kuna mgongano baina ya Katiba na Sheria, wanaanza kutafsiri Sheria kuipindua Katiba na sio kutafisiri Katiba ili kuipindua Sheria inayopingana na Katiba kama inavyoelekezwa na ibara ya 64(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mwanasheria yeyote aliyemshauri Rais kumuondoa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kutumia Sheria inayoweka masharti ya vipindi bila kuzingatia masharti ya wazi ya ibara ya 144(1) ya Katiba amemkosea sana Rais, amewakosea sana Watanzania na ameifedhehesha sana taaluma ya Sheria.

Fedheha kubwa zaidi kwa taaluma ya sheria ni pale wanasheria watapoanza kutofautiana katika kutafsiri masharti hayo ya wazi ya Katiba kwa itikadi au mirengo ya kisiasa au kwa baadhi kufanya hivyo kwa kupotosha ili kumfurahisha mteuzi.

Athari ya jambo hili haitokuwa kwa Profesa Mussa Assad. Athari kubwa ni katika mfumo wetu wa kikatiba, utawala wa sheria na matumizi ya mamlaka ya umma. 

*OTHMAN MASOUD OTHMAN*

No comments :

Post a Comment